Mdude Chadema: Mkosoaji wa serikali ya Tanzania aliyetekwa na watu wasiojulikana ni nani?

MDUDE NYAGALI Haki miliki ya picha MDUDE NYAGALI/ FACEBOOK
Image caption Mdude amekuwa akikosoa utendaji kazi wa serikali katika mitandao ya kijamii

Mdude Nyagali tangu mwaka 2016 amekuwa mkosoaji wa serikali ya Tanzania katika mitandao ya kijamii.

Inaarifiwa ni mzaliwa wa kijiji cha Isongole Wilaya ya Ileje katika mkoa wa Mbeya mnamo 25 Agosti 1987.

Binafsi katika blogu yake mdudenyagali.simplesite, anajitambulisha kama mpiganiaji uhuru wa kujieleza na uhuru wa kuwepo mdahalo wa kisiasa.

'Changamoto tunazopitia wapinzani katika taifa hili ndio changamoto walizozipitia wanafunzi wa YESU wakati wakieneza ukristo. Sasa tusife moyo tupambane kulitetea taifa. Tunaweza kufungwa, kupotezwa au kuuwawa lakini itakuwa heshima tutakumbukwa vizazi na vizazi' anasema katika blogu hiyo.

Alijiunga na chama cha siasa cha upinzani cha CHADEMA mnamo mwaka 2008 na amekuwa akijihusisha katika siasa ikiwemo kusimamia kampeni kisiasa za wagombea katika chama hicho cha upinzani Tanzania.

Mdude amekuwa akikosoa utendaji kazi wa serikali ya chama tawala CCM kwenye majukwaa ya kisiasa pamoja na katika mitandao ya kijamii.

Ametumia mitandao ya kijamii kama twitter kuikosoa serikali kama katika ujumbe huu wake wa mwisho wiki iliyopita kabla ya taarifa za kupotea kwake kuchipuka.

Amewahi kushtakiwa kwa kosa la uchochezi dhidi ya serikali.

Image caption John Mrema aeleza mtiririko wa matukio yaliomkabili Mdude tangu mwaka 2016

Kwa mujibu wa Chadema, mtiririko wa matukio haya yalioorodheshwa na John Mrema, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, ndiyo yanayowapa mashaka kwamba vyombo vya dola vinahusika katika yaliomkuta Mdude:

Agosti 26 2016: Mdude akamatwa Vwawa

Agosti 28 2016: Ahamishiwa kambi ya FFU Mbeya

Agosti 29: Apelekwa Dar es Salaam na kuwekwa Osterbay polisi

Septemba 1 2016: Apelekewa hospitali ya Mwananyamala Dar Es Salaam kufuatia madai ya kuteswa

Septemba 13: Polisi wamuondoa hospitali Mwananyamala na kumepeleka Vwawa.

Septemba 14: Afunguliwa kesi ya mashtaka ya kuandika uongo.

Aprili 2017: Mdude ashinda kesi.

Novemba 2017: Akamatwa tena Vwawa na kupelekwa Dar Es Salam ambako aliwekwa kituo cha Polisi cha Central kwa siku 21. Baada ya hapo arudishwa Vwawa ambako afunguliwa kesi ya uchochezi

Novemba 2018: Kwa mara nyingine Mdude ashinda kesi Novemba 2018.

Januari 2019: Mdude aandika notisi ya kulishtaki Jeshi la polisi

Machi 2019: Afungua kesi mahakama kuu kanda ya Mbeya na kumshtaki Inspekta Jenerali wa polisi, RPC wa Songwe, Mwanasheria mkuu wa serikali na askari polisi watatu.

Hatahivyo, Polisi wamekanusha kuhusika na kutekwa kwake na wanaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo.

Chama kikuu cha upinzani Chadema wamevitaka vyombo vya usalama kutoa taarifa awali kuhusiana na madai ya kutekwa, kuteswa na kisha kukutwa akiwa ameumizwa Mdude Nyagali.

Inaarifiwa wanakijiji walimpata ametupwa katika kijiji cha Makwenje , wadi ya Inyala katika jimbo la Mbeya.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii