Mwanahabari wa Tanzania aliyetoweka Azory Gwanda aorodheshwa miongoni mwa visa 10 vya wanahabari duniani vinavyohitaji dharura

Azory Gwanda Haki miliki ya picha Azory/ facebook

Mwandishi wa Tanzania aliyetoweka Azory Gwanda ameorodheshwa miongoni mwa visa kumi vya dharura na kudi moja la muungano wa uhuru wa vyombo vya habari duniani.

Kulingana na gazeti la The Citizen nchini Tanzania Mwandishi huyo ambaye hajaonekana tangu Novemba 2017 ameshirikishwa katika orodha ya mwezi Mei ya uhuru wa vyombo vya habari na muungano unaopigania umoja wa vyombo huru vya habari.

Muungano huo unashirikisha umoja wa zaidi ya makundi 30 ya wahariri na wachapishaji kikiwemo chombo cha habari cha Reuters, Quartz, The financial times , India Today, TIME na Washington Post miongoni mwa mengineyo.

Kundi hilo linatumia ukubwa wake duniani kuleta muamko kuhusu visa vya wanahabari alio katika tishio.

Kulingana na gazeti hilo kamati ya kuwalinda wana habari na wakfu wa kimataifa wa wanahabari wanawake pia ni washirika katika muungano huo.

Bwana Gwanda anadaiwa kutekwa katika operesheni iliofanyika katika pwani ya wilaya ya Kibiti ambapo mauaji ya kiholela yalikuwa yakifanyika.

Mamlaka yatakiwa kuwajibika

Kwa kumuorodhesha miongoni mwa visa 10 vya dharura duniani, muungano huo umeangazia tena habari za mwanahabari huyo kwa lengo la kuishinikiza mamlaka kuwajibika kwa kutoweka kwake.

Orodha hiyo ni ya wanahabari ambao uhuru wao unakandamizwa naa ambao wanapigania haki.

Mwandishi huyo wa Tanzania alikuwa akiifanyia kazi kampuni ya Mwananchi wakati alipotekwa katika mazingira ya kutatanisha.

Alikuwa akiripoti kesi za mauaji ya kiholela katika eneo la kibiti katika mwezi uliopelekea kupotea kwake.

Serikali imedai kuchunguza kesi yake na za watu wengine waliotoweka lakini hakuna kilichoafikiwa hadi sasa.

Kuna shinikizo kutoka kwa makundi ya haki za kibinaadamu , waandishi na mashirika ya habari kama vile kamati ya kuwalinda wanahabari CPJ zikitoa wito kwa mamlaka ya Tanzania kuipatia kipau mbele kesi ya Gwanda na kutoa majibu kuhusu hatma yake kupitia hashtag WhereIsAzory na hashtag MrudisheniAzory zikisambazwa katika mitandao ya kijamii.

Kesi yake hivi karibuni imewasilishwa katika majukwaa ya umma kuhusu haki za raia na 2018 alishinda tuzo ya 'Daudi Mwangosi' bila ya yeye kuwepo ili kuheshimu kazi yake na ujasiri.

Hatma ya Gwanda ni ipi?

Kuhusiana na mustakabali wa mwanahabari huyo , Waziri wa Habari wa Tanzania hivi karibuni aliliambia Bunge la nchi hiyo kuwa: "Tunaongelea kesi ambayo ni dhaifu sana, mwandishi huyu amepotea eneo ambalo mamia ya Watanzania wengine wamepotea, hawauliziwi hao ila mmoja huyo ndiyo dhahabu."

"Halafu inaulizwa Serikali ambayo imeshughulikia kwa kiasi kikubwa na maofisa wa Serikali wengi wamekufa pale, najua mnawalisha Wazungu na wafadhili matangopori, hatujakosa chochote acha tushushwe madaraja, sisi tunaheshimu uhuru wetu kwanza," alisema.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii