Wezi waiba vito vya dhahabu katika jumba la Mengi Tanzania

Mke wa Mengi akiwa pamoja na watoto katika ibada ya mwisho ya mazishi ya mume wake Dr.Reginald Mengi
Image caption Mke wa Mengi akiwa pamoja na watoto katika ibada ya mwisho ya mazishi ya mume wake Dr.Reginald Mengi

Siku mbili baada ya mfanyabiashara tajiri wa Tanzania marehemu Reginald Abraham Mengi kuzikwa, wezi wameibia familia yake ambayo bado inaomboleza vifaa vya thamani na fedha taslimu mjini Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa Gazeti la Mwananchi vitu vinavyodaiwa kuibiwa ni pamoja na mikufu ya dhahabu, kompyuta pamoja na fedha taslimu ambazo kiwango chake hakijaelezwa.

Vitu hivyo vinasemekana kuwa ni mali ya familia na waombolezaji na zilikuwa katika jumba la kifahari la mjane wake, Jacqueline Mengi ambako mwenyekiti huyo wa kampuni za IPP alizikwa Alhamisi iliyopita.

"Ni kweli nyumbani kwa Mengi kumeibiwa," alisema Kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah na kuthibitisha kuwa wanawashikilia watu wawili wanaoshukiwa kuhusika na wizi huo.

Kamanda Issah pia ameongeza kuwa tukio hilo huenda limefanywa na watu wanaodaiwa kuwa wa ndani na familia hiyo na kwamba taarifa zaa awali za uchunguzi zinaonyesha walitokea jijini Dar es Salaam.

"Suala hilo ni la ndani na tukianza kulishughulikia kikamilifu litahusisha watu ambao ni wa ndani. Sasa sijui tutakuwa kwenye msiba au tutakuwa tunakamatana, maana tumeongeza huzuni juu ya huzuni''.

Akizungumza na Gazeti la Mwananchi Kamanda Issah alisema kuwa kulitokea watu mchanganyiko wakati wa mazishi ya Bw. Mengi na kila mtu alisema yeye ni mwanafamilia na ''kila mtu anaingia mahali ambako hahusiki na matokeo yake ni wizi."

Image caption Mamia ya watu waliyojitokeza katika mazishi yamfanyibiashara Reginald Abraham Mengi

Alisema baadhi ya watu ambao hawakutaka majina yao yatajwe, walidai baadhi ya waliohusika walikuwa wamevalia vitambulisho vilivyoandikwa IPP.

Msemaji wa familia hiyo, Benson Mengi alisema kwa sasa hawawezi kuzungumzia jambo hilo kwa kuwa bado uchunguzi unaendelea.

"Bado uchunguzi wa polisi unaendelea," alisema Benson, mtoto wa mdogo wa marehemu Reginald Mengi.

Reginald Mengi Mengi ambaye alikuwa mwanzilishi wa makampuni ya IPP alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 77 na ameacha mke na watoto wanne.

Haki miliki ya picha IPP

Mengi alizaliwa wilayani Machame, Kilimanjaro, Tanzania mwaka 1942, akiwa mmoja wa watoto saba wa Bw Abhraham Mengi na Bi Ndeekyo Mengi.

"Familia yetu ilikuwa masikini sana, kila siku ilikuwa ni vita ya kupambana na umasikini. Tulimiliki sio zaidi ya ekari moja tukiishi kwenye vibanda vya udongo tukichanganyika na ng'ombe wachache na kuku. Ninaporudisha fikra na kutazama nyuma ni vigumu napatwa na ugumu wa kufikiri namna tulivyoweza kuishi katika hali ile," alipata kusema kwenye uhai wake.

Alianza safari yake kielimu shule katika shule ya msingi Kisereny Village Bush School, kisha akajiunga Nkuu District School, kisha Siha Middle School, na baadaye Old Moshi Secondary School.

Kwa ufadhili wa Chama cha Ushirika kilichokuwa na nguvu ya kifedha ushawishi KNCU Mengi alisomeshwa masomo yake ya shahada ya kwanza ya uhasibu nchini Uingereza.

Baada ya masomo ughaibuni, Mengi alirudi Tanzania 1971 na kuajiriwa na kampuni ya Cooper and Lybrand Tanzania ( sasa Prince water house Cooper) mpaka mwaka 1989 alipoamua kujikita kwenye ujasiriamali.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii