Je vyombo vya usalama vimeshindwa kudhibiti uhalifu mtandaoni?

Usalama mtandaoni Haki miliki ya picha SOPA Images

Uhalifu wa mitandaoni sasa ni tatizo linaloikabili dunia zikiwemo nchi za Afrika Mashariki.

Katika kukabiliana na tatizo hilo baadhi ya nchi zimetunga sheria za kukabiliana na uhalifu mitandaoni lakini bado inaonekana tatizo linazidi kuendelea.

Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya watu kwamba wamekuwa wakidhalilishwa na wengine kupoteza na kuibiwa pesa nyingi kufuatia kutapeliwa na wahalifu wa mitandaoni.

Je vyombo vya usalama mitandaoni vimeshindwa kudhibiti uhalifu mtandaoni?

Tanzania mtandao salama kiasi gani?

Joshua Mwanagasa, Mrakibu msaidizi wa polisi katika kitengo cha kushughulika na uhalifu wa mtandaoni nchini Tanzania anasema uhalifu wa mtandao ni uhalifu uliokuja kwa sura mpya, anaeleza ni utendaji wa makosa uliokuja kwa mtindo mpya na utendaji wake sio kama utendaji ambao umezoeleka.

Akizungumza na BBC Swahili, anaeleza kwamba inatokana na teknolojia iliyotufikisha katika kiwango hicho, na teknolojia inazidi kukuwa kadri siku zinavyoendelea.

Haki miliki ya picha Getty Images

'Anga la kimtandao wa Tanzania ni salama kutokana na kuchukulia hatua nyingi na hasa sheria ya mtandao ya mwaka 2015 ilipotungwa tu, imesaidia kupunguza makosa kwa asilimia kubwa kwasababu ya kukabiliana na makosa.

'Sheria inatoa mamlaka makubwa licha ya kwamba sheria hiyo ilikuwa na matatizo katika siku za nyuma' anasema Kamanda Mwanagasa.

Sheria ya makosa ya mtandaoni iliyoidhinishwa Tanzania mnamo Septemba mosi 2015, inaeleza kwamba kusambaza taarifa zisizo sahihi, zenye kupotosha unaweza kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha jela au kulipa faini.

Kumekuwepo na upinzani mkubwa kutoka kwa vyombo vya habari na wamiliki wa mitandao ya kijamii kuhusiana na sheria hiyo.

Moja kati ya malalamiko ni mamlaka inayowapatia wasimamizi wa sheria hiyo.

Polisi wana mamlaka ya kuchukua na kukagua simu, kompyuta na kukagua taarifa mbalimbali katika vifaa binafsi vya mawasiliano bila waranti.

Sheria hiyo pia inawataka watoa huduma za simu kukabidhi taarifa za wateja wao kwa mamlaka.

Serikali inasema sheria hiyo inahitajika kuzuia matumizi mabaya ya mitandao na kulinda makundi mbalimbali ya watu kama watoto.

Kasi ya muitikio wa matukio ya uhalifu?

Changamoto inaelezewa kutokana na kwamba mawasiliano ya mtu ni faragha - na kisheria ni haki ya kimsingi ya mtu kuwa na faragha.

'Utaratibu unavyokuwa ni kwamba maafisa hawaingii katika mawasaliano binafsi ya mtu, ila tunafuatilia mawasiliano katika majukwaa ya wazi.'

Na ni kupitia 'online patrol' - kuingia mtandaoni na kushughulikia sio tu kutokana na kesi zilizoriptowa au kutokana na kutendeka kosa, kwa hivyo hutokea 'ukamataji na upekuzi ukafanyika hata kabla ya kosa kutokea' anasema Mwanagasa.

Teknolojia: silaha kwa makundi yenye itikadi kali

Hali nchini Kenya sio tofauti sana na nchini Tanzania, maana kuna sheria zilizotungwa kukabiliana na uhalifu huo.

Tatizo wataalamu wanasema ni kwamba kila kukicha teknlojia mpya inazuka na vijana wengi wanajihusisha na uhalifu wa mtandaoni. Na ni mtihani mkubwa kwa vitengo vya usalama kujizatiti katika kukabiliana na tatizo hilo kwasababu wengi wanajihusisha na uhalifu huu.

George Msamali ni mchambuzi wa masuala ya Usalama nchini Kenya, anasema ni mbinu mpya inayotumika na makundi yenye itikadi kali ili kuleta tisho duniani, katika kuleta tofuati za kidini na anaeleza kwamba hatua zinapaswa zichukuliwe ili kuhakikisha mashambulio kama hayo hayashuhudiwi tena.

Je uhalifu huu unaweza kudhibitiwa kwa kiasi gani?

Msamali anakiri kwamba 'ni vigumu kudhibiti uhalifu huu kwa 100%. Maanake unapata mhalifu anakuwa hatua moja au mbili mbele ya vitengo vya usalama kwasbaabu anajua yeye anachokifanya, na anajua mpangilio anaotumia kutekeleza uhalifu huo.

'Kilicho muhimu ni kuhakikisha tunachukua hatua za ziada, kwamba tuwahusishe pia wale watuamiaji wa mtandao na kuwaeleza kwamba mbinu zinazoweza kutumika ili kukabiliana na uhalifu ni kadha wa kadha na wengi wahusishwe isiwe ni jukumu la vitengo vya usalama peke yake'.

Haki miliki ya picha NurPhoto

Mabenki yamelengwa, wananchi wanatapeliwa katika mitandao, uhalifu unatendeka katika mitandao na ni muhimu kuwa na uhamisho kuhusu mbinu hii mpya ya uhalifu.

Ni hatua gani unazoweza kuchukua uli usiathirike na uhalifu huu?

  • Jilinde mwenyewe kwanza, maana ulinzi unaanza kwako binafsi.
  • Zingatia sheria za mtandao ambazo zimetumika kuainisha makosa mengi.
  • Zingatie usiathirike kwa kujilinda wewe na mawasiliano yako- kama vile kuhakikisha hakuna anayefahamu nywila yako.
  • Hoji simu au ujumbe unaopokea katika simu yako - jiulize ni halali au ujumbe unatoka mahali sahihi? Jiridhishe kabla ya kutoa taarifa.

Licha ya kwamba wataalamu wanasema tatizo hili haliwezi kumalizwa kikamilifu, Kamanda Mwanagasa anakiri kwamba cha msingi na muhimu ni elimu itolewe kwa wananchi wengi.

Kwasababu ananukuu matokeo ya utafiti mdogo anaosema, 'imebainika kwamba mtu akielemishwa kuna asilimia kubwa sana ya kupunguza uhalifu kwa 90%'.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii