Utindio wa ubongo au Cerebral Palsy ni ugonjwa wa aina gani?

Maria Njeri Haki miliki ya picha Maria Njeri
Image caption Maria Njeri

Maria Njeri alizaliwa miaka 26 iliyopita akiwa na tatizo la utandio wa ubongo, kwa lugha ya kimombo cerebral palsy (CP).

Njeri alitembea akiwa na umri wa miaka minne na alikuwa akitembea na kuanguka mara nyingi.

''Nilijiunga na shule ya chekechea nikiwa na miaka 6 katika shule ya kawaida bila kupatwa na matatizo yoyote na baadaye nikajiunga na shule ya msingi ya kawaida na hapo ndipo nilianza kugundua kwamba mimi ni tofauti.'' Maria Njeri alisema

Lakini wakati huo wote nilikuwa chini ya uangalizi mkubwa wa mamangu kwani nilikuwa nikiugua mara kwa mara na kulazwa hospitalini.

Nilipokuwa katika shule ya msingi watoto wengine walikuwa wakiniambia kwa nini mimi huongea hivyo? Mbona mimi hutembea hivyo? Na jibu langu kila wakati lilikuwa 'mimi hutembea hivyo na hata kuongea kwani sikujua nilikuwa tofauti.' anasema Njeri.

Maswali hayo Njeri anaeleza kuwa yalizidi na alianza kutengwa huku watoto wenzake wakikataa kucheza na hata kutembea na yeye na hapo anasema akaanza kujiuliza 'kwa nini niko hivi?'

Haki miliki ya picha Maria Njeri

Maswali hayo yote kutoka kwa wanafunzi wenzake anasema yalimuumiza sana kwa sababu hakutaka kuwa tofauti na kwa muda huo, alikuwa haelewi na hajui namna ya kuishi na palsy.

'Hapo ndipo nikamwambia mamangu kwamba sitaki kuwa na celebral palsy na akanijibu kwamba kama sio mimi nani atakuwa nayo?'

Hapo Njeri anaeleza ndipo alipopata sababu ya kuishi.

Lakini hayo yote yalipita na akamaliza shule ya msingi na kujiunga na shule maalum ya watu wenye ulemavu.

Shule hiyo maalum ilikuwa ikiwashugulikia watoto kila mmoja jinsi anavyoweza kuelewa masomo tofauti.

'Mimi nilikuwa na kasi ndogo ya kushika mambo tofauti darasani lakini pindi tu ninapoelewa basi mimi huwa sawa na wanafunzi wengine, kwani masomo hayo hayakuwa tofauti na masomo yanayofunzwa katika shule za kawaida'.

Anasema ugonjwa huo haukumzuia kujiunga na chuo kikuu na kutimiza ndoto yake ya kuisaidia jamii kwa kuhitimu na shahada ya ustawi wa jamii.

'Sina uhakika ni umri gani ambapo mzazi wangu aliniarifu kwamba niko tofauti na watoto wengine lakini hakuniambia nina celebral palsy, lakini akasisitiza kwamba hali hii haitayatatiza maisha yangu ya kawaida kama vile kwenda shule au kucheza'.

Haki miliki ya picha Maria Njeri
Image caption Njeri amehitimu na shahada ya ustawi wa jamii.

Utindio wa ubongo au Cerebral Palsy ni ugonjwa wa aina gani?

•Ni tatizo la ubongo ambalo huathiri watoto na husababishwa wakati damu inapovuja kwenye ubongo.

•Mtoto anapoanza kupoteza fahamu punde baada ya kuzaliwa au mwezi wa kwanza wa kuzaliwa.

•Jeraha kwenye ubongo linaweza kusababisha matatizo ya kuongea na ugumu wa kufahamu mambo.

Aina tofauti za utindio wa ubongo

Kuna aina tofauti za utindio wa ubongo lakini inayofahamika zaidi ni Spastic cerebral palsy ambayo husababisha viungo na misuli kuganda.

Hali hii humfanya mtoto kuwa na uchungu mwingi na mifupa hushindwa kulainika hivyo huchukua muda kabla ya mtoto kutembea.

'Mimi ningependa kuwashukuru wazazi wangu kwa kunipenda kama mtoto mwengine yule hawakuona tofauti yoyote'.

Baada ya kuyapitia yote Njeri aliamua kuanzisha wakfu ili aweze kuihamasisha jamii na kuwafahamisha kwamba mtoto anayezaliwa na tatizo la utindio wa ubongo anaweza kuishi kama mtoto mwengine yule.

Njeri amesisitiza kwamba jamii inastahili kuwapokea watoto wanaozaliwa na hali hiyo na hata wazazi wao na kwamba utindio wa ubongo ni kama ugonjwa wowote ule.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii