Kwanini Tanzania inataka 'kunadi' maeneo maalum ya uwindaji?

Simba Haki miliki ya picha Getty Images

Makampuni yanayoendesha shughuli za utalii nchini Tanzania kuanzia mwezi ujao yatalazimika kutafuta hati miliki ya uwindaji katika maeneo maalum.

Hii ni baada ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kutangaza mpango mpya wa kunadi maeneo yatakayotengwa kwa uwindaji wa wanyama pori.

Hatua hiyo inalenga kuleta uwazi ili kuepusha visa vya rushwa katika sekta kubwa ya utalii nchini humo.

Mamlaka hiyo imesema kuwa maeneo 26 yatatengwa kwa shughuli hiyo na kwamba kila kampuni itapewa nafasi isiyozidi tano.

Baadhi ya maeneo hayo yanapatikana katika hifadhi ya wanyama ya Selous, iliyo na sifa ya kuwa na wanyama kama vile tembo, simba, punda milia na twiga.

Mwanasayansi na mwanaharakati wa kutoa hamasa kwa wadao wote wanaofanya kazi katika masuala ya uhifadhi nchini Kenya, Jim Nyamu anasema karibu 70% ya wanyama pori hawako kwenye hifadhi na kuna sababu nyingi sana za kiekolojia ambazo zinawafanya kutoka katika makazi yao asilia.

Hatua hiyo itakua na athari gani?

''Tunaposema sehemu hizi ambazo wanyama wanaishi tuzitoe au tuziuzeama tufanye biashara kando na uhifadhi ama utalii itakua ni vibaya sana'' alisema Bw. Nyamu.

Pia anasema kuwa mbuga za wanyama zinakabiliwa na changamoto za kiekolojia kwasababu wanyama wamekua wengi kupita kiasi katika hifadhi zao, maji yamekua haba na malisho au chakula chao pia kimepungua.

Hali hiyo huwafanya wanyama kutoka na makazi yao asilia na kuanza kutangamana na watu kwasababu ya kutafuta maji na usalama.

''Tunapobadilisha dhana halisi ya uhifadhi tunawaweka wanyama wetu katika hatari ya kuangamia zaidi ya hali ilivyo sasa kwasababu watalii wanaokuja sio wa kupiga picha bali ni wa kupiga bunduki.''alisema mwanaharakati huyo wa uhifadi wa wanyama.

Haki miliki ya picha Getty Images

Wanyama kama vile Twiga wamepungua sana duniani katika kipindi cha miaka 30 iliyopita na kwa sasa wanakabiliwa na hatari ya kuangamia.

Idadi ya twiga duniani imeshuka kutoka 155,000 mwaka 1985 hadi 97,000 mwaka 2015 kwa mujibu wa shirika la kimataifa la uhifadhi wa mambo asilia (IUCN).

Idadi ya wanyama hao imepungua sana kutokana na kuharibiwa kwa maeneo wanamoishi, uwindaji haramu na migogoro ya kisiasa katika maeneo mengi Afrika.

Akizungumzia suala la kutenga maeneo maalum ya uwindaji kama ilivyoamua Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) mwanaharakati wa uhifadhi kutoka Kenya Jim Nyamu amesema, biashara kama hizo zinapofanyika inamanisha wale waliyopewa leseni wanatumia bunduki katika shughuli zao hali ambayo inaweza kuchangia ukosefu wa usalama.

''Tutakuwa tumefungua mlango kwa wahalifu kutumia silaha kwa sababu ni vigumu kutofautisha mlio wa bundiki ambayo ni halali na mlio wa bunduki ambayo si halali'' , alisema.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Shughuli za kibinadamu katika makazi asilia ya wanyama ni changamoto kubwa

Bw. Nyamu pia aliongeza kuwa mpango huo huenda ukafungua biashara kwa wezi ambao watatumia fursa hiyo kujiendeleza kwa njia haramu hali ambayo itaathiri usalama.

''Hakuna watalii wanaotembelea nchi bila kufanya utafiti wa kina eneo wanalokwenda, wanajua kwa mfano wakija Kenya wanajua nini kinafanyika huko na wakiamua kwenda Ngorongoro wanajua kile wanachotarajia kuona'' anasema Bw. Nyamu.

Mpango wa serikali ya Tanzania wa kutengia makampuni ya utalii maeneo hayo umekumbwa na madai ya ulaghai na ulaji rushwa hali ambayo imechangia kupotea kupungua kwa ushuru.

Sekta ya utalii mwaka jama ilichangia dola milioni 2.4 kwa uchumi wa Tanzania huku watu karibu milioni 1.5 wakizuru taifa hilo mwaka jana ikilinganishwa na milioni 1.33 mwaka uliyotangulia.

Rais John Magufuli amesema serikali yake inapanga idadi ifikie milioni 2 kufikia mwaka 2020.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii