Je unaweza kujikinga vipi na maambukizi ya homa ya dengue Tanzania?

Image caption Homa ya dengue inaambukizwa na virusi vya mbu aina ya Aedes ambao ni weusi wenye madoadoa meupe yenye kung'aa.

Watu 12,000 wamegundulika kuugua ugonjwa wa homa ya Dengue nchini Tanzania toka Januari mpaka mwanzoni mwa Mei 2019.

Taarifa ya serikali ya Tanzania kupitia wizara ya Afya inaeleza kuwa jumla ya wagonjwa 1,237 wamegundulika na ugonjwa huo katika kipindi tajwa huku jiji la Dar es Salaam likongoza kwa kuwa na wagonjwa 1,150, Tanga wagonjwa 86 na Singida mgonjwa mmoja.

Gazeti la Mwananchi limemnukuu mganga mkuu wa serikali ya Tanzania Profesa Muhammad Kambi akithibitisha kutokea kwa vifo viwili vilivyosababishwa na ugonjwa huo, japo marehemu hao pia walikuwa na maradhi mengini pia.

Takwimu zilizotolewa mwanzoni mwa mwezi wa nne na Naibu Waziri wa Afya Dkt Faustine Ndugulile zilionesha kuwa mpaka wakati huo watu 307 waligundulika na virusi vya homa hiyo, 252 wakiwa Dar es Salaam na 52 Tanga.

Wizara ya Afya imeshatoa tahadhari kwa mamlaka za miji na majiji yote juu ya kuchukua tahadhari ya kusambaa kwa maambukizi ya ugonjwa huo.

Tayari jiji la Dar es Salaam limeshaanza jitihada za udhibiti kwa kunyunyizia dawa ya viuadudu (Biolarvicides) kwa ajili ya kuangamiza mazalia ya mbu waenenezao ugonjwa huo.

"Wizara inaelekeza mikoa na halmashauri zote nchini kuendelea kuchukua hatua za kudhibiti ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na kufukia madimbwi ya maji, kunyunyizia dawa ya kuua viluwiluwi, kuondoa vitu vinavyosababisha mazalia ya mbu, kufyeka vichaka, kufunika mashimo ya maji taka kwa mifuniko pamoja kusafisha gata za paa la nyumba na kutoruhusu maji kusimama," Profesa Kambi amaenukuliwa na Mwananchi.

Pia mpango wa dharula wa miezi sita unaoratibiwa na wizara na kutekelezwa na mikoa yote ya nchi hiyo umewekwa kuanzia Mei mpaka Oktoba.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Moja ya njia ya kupambana na homa ya dengue ni kuangamiza mazalia ya mbu kwa kupuliza dawa

Dalili za homa ya dengue

  • Homa ya ghafla
  • Kuumwa kichwa
  • Uchovu
  • Maumivu ya maungo na misuli
  • Kichefu chefu na kutapika
  • Maumivu ya macho
  • Muwasho na vipele vidogo vidogo

Namna ya kujikinga

  • Kuangamiza mazalia ya mbu
  • Kulala kwenye chandarua chenye dawa
  • Kuvaa nguo ndefu

Maeneo ya Dar es Salaam ambayo yameathirika zaidi na ugonjwa huo ni Ilala, Kariakoo, Upanga, kisutu, Buguruni, Tabata, Mbezi, Ubungo, Kinondoni, Msasani na Masaki.

Homa ya dengue inaambukizwa na virusi vya mbu aina ya Aedes ambao ni weusi wenye madoadoa meupe yenye kung'aa. Dalili za ugonjwa huo huanza kujitokeza siku tatu mpaka 14 toka mtu alipoambukizwa.

Madaktari wanatahadharisha dawa zote zenye diclofenac kuwa si salama kwa afya ya mgonjwa wa dengue. Baadhi ya dawa hizo ambazo hupatikana kwa wingi Tanzania kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa nchi hiyo Profesa Mohammed Kambi ni Ibuprofen, Brufen na Diclopar.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii