Marekani yailaumu Iran kwa kuharibu meli za mafuta katika Ghuba ya Oman

Marekani inailaumu Ira kwa kutekeleza mashambulizi dhidi ya meli nne

Wachunguzi wa Marekani wanaamini kwamba Iran ama makundi inayoyaunga mkono yalitumia vilipuzi kuharibu meli nne karibu na milki za kiarabu UAE siku ya Jumapili, vyombo vya habari vimeripoti.

Wataalam wa kijeshi walitumwa kuchunguza kisa hicho na kugundua mashimo makubwa katika meli hizo. Hakuna ushahidi uliotolewa kuonyesha Iran ilihusika.

Mataifa yalioathiriwa bado hayajatoa lawama zozote. Kisa hicho kimeongeza hali ya wasiwasi kati ya Iran , ambayo iko karibu na mpaka wa Hormuz na Marekani.

Kiwango kikubwa cha mafuta yanayotumika duniani hupitia katika eneo hilo la mpakani .

Mwezi uliopita , Iran ilitishia kuufunga mpaka huo iwapo ingezuiwa kutumia mkondo huo wa maji. Hatua hiyo inafuatia uamuzi wa Marekani kuondoa msamaha wa vikwazo kwa wanunuzi wakubwa wa mafuta ya Iran.

Kundi hilo la wachunguzi wa Marekani liligundua mashimo makubwa katika meli zote nne zilizoathiriwa na wanaamini uharibifu huo ulisababishwa na vilipuzi, kulingana na AP, likinukuu maafisa ambao hawakutajwa.

Hawakuelezea ni vipi uhairibifu huo ulihusishwa na Iran. Chombo cha habari cha CBS kilikuwa na ripoti kama hiyo kikiwanukuu mafisa ambao hawakutajwa.

Je tunajua nini kuhusu hujuma hiyo?

Maelezo machache yametolewa kuhusu kisa hicho , ambacho kinadaiwa kufanyika mwendo wa saa kumi na mbili alfajiri siku ya Jumapili katika maji ya milki za kiarabu UAE katika Ghuba ya Oman , mashariki mwa Fujairah.

Wizara ya maswala ya kigeni UAE ilisema kuwa meli nne za biashara zililengwa katika shambulio la hujuma karibu na Bandari ya Fujairah, ikiwa ni nje ya eneo la Hormuz

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Maboti ya wanamaji wa UAE yamepigwa picha karibu na Al Marzoqah, meli ya mafuta ya Saudia ambalo lilihujumiwa

Hakukuwa na majeraha lakini Saudia inasema kuwa meli zake mbili ziliathirika pakubwa.

Waziri wa kawi wa Saudia , Khalid al-falih alisema kuwa mojawapo ya meli hizo za mafuta ilikuwa inaelekea kujazwa mafuta ya Saudia ambayo yalitarajiwa kupelekewa wateja nchini Marekani.

Meli nyengine ya mafuta ilikuwa na usajili wa taifa la Norway huku ya nne ikidaiwa kuwa na bendera ya UAE.

Haki miliki ya picha HANDOUT
Image caption Kampuni ya meli ya Norway Thome Ship ilisema kuwa meli yake moja ilishambuliwa

Runinga ya Saudia ilionyesha picha za meli zilizoharibiwa, huku picha iliotolewa na UAE ikionyesha meli ya Norway yenye bendara kwa jina Andrea ikiwa na uharibifu mkubwa upande wa chini.

Kampuni ya usimamizi wa meli ya Thome Ship management kutoka Norway ilisema katika taarifa kwamba iliharibiwa na kifaa kisichojulikana katika eneo la chini lililopo majini.

Ni jaribio la makusudi kuongeza wasiwasi?

Ukilinganisha na shambulio la hapo awali dhidi ya meli mashariki ya kati - meli za USS Cole mwaka 2000, ile ya mafuta ya Limburgh 2002 na hivi majuzi mashambulio ya Yemen, uharibifu uliofanywa kwa meli nne katika pwani ya UAE siku ya jumapili ni mdogo.

Hakujaripotiwa kumwagika kwa mafuta , hakuna moto na hakuna majeraha. Lakini wakati ambapo tukio hilo lilifanyika ni hatari na kutilia shaka kubwa.

Yeyote aliyetekeleza shambulio hilo lazima alikuwa ana ufahamu kuhusu hali ya wasiwasi katika Ghuba , huku Marekani ikipelekea vikosi vya ziada katika eneo hilo.

Inaonekana kwamba aliyetekeleza kitendo hicho alitaka kuchochea wasiwasi na hata kusababisha mzozo.

Huku Saudia na UAE zikionekana kumlaumu adui, maafisa wa , Iran, Marekani wamesema kwamba hapo ndipo ulipo wasiwasi wao.

Lakini Iran imeshutumu mashambulizi hayo kuwa mabaya huku msemaji wa bunge la nchi hiyo akisema kuwa Iran inaishuku Israel.

Iran imesema nini?

Iran imetaka uchunguzi wa kisa hicho unachokitaja kuwa cha kutia wasiwasi kufanywa . Katika Ikulu ya Whitehouse siku ya Jumatatu , rais wa Marekani Donald Trump alitoa onyo kwa Iran.

Iwapo watafanya chochote itakuwa makosa makubwa ..iwapo watafanya chochote watakiona cha mtema kuni. Lakini rais wa Iran Hassan Rouhani alikuwa moja kwa moja , akisema kuwa taifa hilo ni kubwa sana kutishiwa na mtu yeyote.

''Mungu akipenda tutapita kipindi hiki kigumu kwa ushindi na kuwashinda maadui'' , alisema katika mkutano na viongozi wa dini siku ya Jumatatu.

Maelezo machache, lakini maswali maengi

Mtandao wa maswala ya baharini dunini umehoji maelezo kuhusu kisa hicho. Orodha yenye ushawishi ya Lloyds List Maritime ya ujasusi ililaumu mamlaka kutokana na maelezo machache.

Ikinukuu kampuni ya usalama wa majini Dryad Global, ilisema: Kushindwa kwa Saudia kutoa ,malezo na ushahidi pamoja na vile ilivyoripoti kisa hicho kunazua maswali mengi kuhusu shambulio hilo.

Mtandao wa Fleetmon ulisema: Ni nini kilichotokea haswa, je milipuko hiyo ilikuwa mibaya kwa kiwango gani iwapo kuna yoyote ilioshuhudiwa.

Je ni yapi matukio ya awali?

Marekani hapo awali ilionya kwamba Iran ama washirika wake huenda ikazilenga safari za majini katika eneo hilo na katika siku za hivi karibuni kupeleka meli za kivita kukabiliana na tishio kutoka kwa taifa.

Kaimu waziri wa ulinzi Patrick Shanahan ameweka wazi mipango ya serikali ya Iran kuvishambulia vikosi vya Marekani , kulingana na New York Times.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais Hassan Rouhani amesema kuwa Iran ni kubwa sana kutishiwa

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii