Je, ni kweli usipokuwa na wake wawili eSwatini unafungwa?

Mfalme Mswati Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mfalme Mswati wa eSwatini akiwa na wapambe wake.

Serikali ya eSwatini imepuuzilia mbali taarifa zinazodai kuwa mfalme Mswati ameagiza wanaume nchini humo kuoa wanawake wawili la sivyo wafungwe jela.

Taifa hilo limesema taarifa hizo ni ghushi ni 'tusi' kwa mfalme huyo ambaye yeye mwenyewe ana wake 14 na watoto zaidi ya 25.

Mfalme huyu ana sifa ya kuishi maisha ya kifahari huku 63% ya watu katika Ufalme huo uliyokuwa ukijilikana na kama Swaziland wakiishi kwa umasikini.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Afrika Kusini (SABC) taarifa hiyo ghushi ambayo awali ilichapishwa katika gazeti la Zambian Observer na kuchukuliwa na machapisho mengine kadhaa ya magazeti ya mtandaoni, ilisema kuwa wanaume Waswazi watalazimika kuoa wanawake wengi kuanzia mwezi Juni mwaka huu.

Taarifa hiyo iliyochapishwa mara ya kwanza siku ya Jumatatu wiki hii ilidai kuwa serikali itafadhili sherehe za harusi na kuwapatia nyumba wanaume watakao waoa wake zaidi ya mmoja.

"Mfalme ameagiza kuwa wanaume wote nchini humo kuanzia mwezi Juni 2019 waoe angalau wanawake wawili la sivyo wafungwe jela," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Msemaji wa serikali ya eSwatini Percy Simelane ametaja taarifa hizo kuwa za "hujuma" na "sumu".

"Mfalme hajatoa tangazo lolote kama hilo wala suala kama hilo halijawahi kusemwa na watu," mtandao wa SABC umemnukuu Simelane akisema.

Aliongeza kuwa taarifa hiyo si tu "tusi kwa ufalme na utamaduni wa eSwatini bali pia ni fedheha kwa tasnia ya habari".

Serikali sasa inataka gazeti lilochapisha taarifa hiyo kuomba msamaha.

Magufuli na wanaume kuoa wake wengi

Hata hivyo, Mswati si kiongozi wa kwanza barani Afrika kulishwa maneno mtandaoni kuhusu suala hilo.

Mwaka jana Rais wa Tanzania John Magufuli alikuwa akihusishwa na taarifa mitandaoni kuwa amewataka wanaume wa nchi yake waoe mke zaidi ya mmoja.

"Wanawake wengi ambao hawajaolewa wanalizimika kushiriki uasherati na waume za watu kwa sababu kuna ukosefu wa wanaume wa kuwaoa," Magufuli alidaiwa kusema maneno hayo na kunukuliwa na mtandao wa nipasheonline.com na kuongeza: "Siwalazimishi, lakini ninawashauri kuoa wake wawilia au zaidi ili kupunguza idadi ya wanawake wasio na waume."

Taarifa hiyo pia ilisambaa kwa kasi ndani na nje ya Tanzania, na mchungaji mmoja nchini Ghana alizinukuu kwenye moja ya mihadhara yake.

Haki miliki ya picha BBC Sport

Hata hivyo, taarifa hiyo pia ilikuwa ghushi. Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu ya Tanzania Gerson Msigwa alilazimika kuikanusha taarifa hiyo kupitia mtandao wake wa Twitter.

Mitandao ya kijamii inazidi kupenya barani Afrika na kurahisisha mawasiliano ya watu na kuchochea maendeleo ya nyanja mbalimbali.

Lakini mitandao hiyo pia imekuwa ikilaumiwa vikali kuwa nyenzo ya kusambazwa kwa taarifa ghushi ama fake news, kwa lugha ya kingereza.

Mada zinazohusiana