Femicide: Kwanini ukatili dhidi ya wanawake na mauaji yanazidi nchini Kenya?

wanawake wauawa kenya
Image caption Familia ya Ivy Wangeci, mwanafunzi wa chuo kikuu cha Moi aliyeuawa kwa kukatwa kwa shoka

Mauaji ya wanawake kwa sababu yeye ni mwanamke - ni tatizo linaloshuhudiwa duniani.

Wanaharakati nchini Kenya wanasema kumekuwa na ongezeko la ukatili au mashambulio dhidi ya wanawake huku 40 wakiripotiwa kuuawa mwaka huu peke yake.

Katika kaunti ya Busia magharibi mwa Kenya, eneo linalotajwa kushuhudia visa zaidi vya aina hii nchini, msalaba wa mbao ya kahawia umetundikwa juu ya kaburi ukiwa umeandikwa maandishi meupe ya jina la aliyezikwa katika sehemu hiyo.

Protus Kapulena mkewe Jesca wanavuta matawi na nyasi zilizomea kutoka kwenye kaburi la binti yao.

Mwaka mmoja uliopita Phylis Kapule aliyekuwa na miaka 16 alizikwa hapa.

Image caption Kaburi la Phylis Kapule, binti wa miaka 16 aliyeuawa mwaka jana

'Ilikuwa siku ya Jumapili , niliambiwa na mvulana mmoja niliyemfahamu kwamba binti yangu amefariki'.

'Katika chumba cha kuhifadhia maiti, wahudumu waliniarifu kwamba kuna mwili wa msichana kwa jina Phylis. Alipoufungua mlango kweli ni binti yangu aliyekuwa amelazwa mezani' anaeleza Jesca Kapule.

Phylis alinyanyaswa kingono, akapachikwa mimba na baadaye akauawa. Mshukiwa ambaye ni mpenzi wake Phylis yupo rumande na amekana mashtaka.

'Ninapoamka asubuhi na nikilitazama kaburi, naingiwa na uwoga mwingi, ninahisi uchungu sana. Sikulitarajia, nilifahamu kwamba binti yangu atamaliza masomo, linaniwacha na mawazo mengi sana', anaongeza Jesca.

Image caption Jesca Kapule mamake Phylis Kapule aliyeuawa akiwa na miaka 16

Katika kijiji kilicho umbali wa nusu saa kutoka nyumbani kwa familia ya Kapule, familia nyingine inakusanyika.

Wanawake wanaonekana wakinong'onezana…. baadhi wanalia.

Ni nyumbani kwa Benta Otieno na anasema siku mbili zilizopita, mwili wa mjukuu wake wa miaka 17 ulitupwa nje ya nyumba yao.

'Walimnyunyizia tindi kali. Mkono mmoja ulikuwa umekatwa, hauko. Hukuweza hata kujua kama ni mjukuu wangu. Tindi kali hiyo iliiharibu ngozi yake mwilini kabisa' anasema Benta.

Inatuhumiwa alibakwa kabla ya kuuawa.

Katika miezi kadhaa iliyopita visa kama hivi vya wanawake kuuawa kutokana na unyanyasaji na ukatili vimekithiri katika vyombo vya habari nchini.

Mashirika ya kutetea haki za binaadamu sasa yamenakili visa 7 vya wanawake kuuawa katika kaunti hiyo ya Busia katika muda wa wiki tatu mwezi Aprili.

Wanakijiji wa Nambale wana hasira kali. Ni hisia inayojitokeza kote nchini.

Baadhi wanahisi kwamba serikali haiwajibiki ipasavyo katika kuvishughulikia visa hivi vya mauaji ya wanawake.

Image caption Benta Otieno anasema mjukuu wake alinyunyiziwa tindi kali na akakatwa mkono mmoja

'Mimi ni mama na nina uchungu kwasababu kila mahali wasichana wetu wanauwa. Na sasa, limefika hapa kwangu. kwain serikali hailishughulikii hili. Kitu gani kinafanyika?' anauliza Sarah Etemesi mkaazi katika kijiji cha Nambale.

Raia wanachukua sheria mikononi na tayari wamechoma nyumba ya mshukiwa mmoja katika mauaji ya mjukuu wa Benta.

Hospitali ya rufaa ya Busia ndio kituo kikuu katika kaunti hiyo. Kila mwezi angalau wanawake 15 hulazwa wakiwa na majeraha mabaya yanayotokana na unayanysaji wa kingono na kimwili.

Irene Akinyi mwenye umri wamiaka 26 na dadake wanalala katika kitanda kimoja katika wodi ya hospitali hiyo.

Wamekuwa hapa kwa wiki tatau sasa.

Mumewe Irene aliwakata kwa panga alipokataa kuchukua mkopo ili ampe muewe. Anauguza majeraha ya mkono na tumboni alikokatika na hata mapajani.

'Nilikuwa ninakufa, sikuweza hata kupumua vizuri. Siwezi kurudi nyumbani bado ninaogopa, Familia yake inaweza ikarudi kunishambulia tena' anasema

Mumewe Irene alijitia kitanzi , alipodhani kwamba amewaua.

Mapema mwezi huu kuliandalia maandamano karibu na mji mkuu Nairobi, kutoa wito kwa wanaume wasiwashambulie wanawake.

Wasiwasi uliopo kwa wengi ni kwamba maafisa kuanzia idara ya polisi mpaka viongozi wakuu serikalini hawalishughulikii ipasavyo suala hili.

Kuna tofuati katika mauaji ya aina hii maarufu femicide, yanayojitokeza kwa kutokuwepo data au utoafuati na mauaji mengine ya kawaida.

BBC imejaribu kuwasiliana na polisi nchini ambao wamekataa kutoa taarifa kuhusu tatizo hili.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii