Spika Ndugai: Hakuna anayejikagua mwenyewe

Haki miliki ya picha NAOT

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ameliibua tena sakata la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof Mussa Assad, safari hii kuhusu mapato na matumizi yake.

Spika Ndugai ameliambia Bunge mapema leo kuwa mhimili huo uliagiza kukaguliwa kwa hesabu za mapato na matumizi ya ofisi ya CAG na tayari mkaguzi wa nje aliyepewa kazi hiyo amekwishawasilisha ripoti.

"Hesabu za ofisi ya CAG zinapaswa kukaguliwa angalau mara moja kwa mwaka na Bunge kupitia kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali ambayo huwa inajukumu la kuteua mkaguzi wa ofisi hiyo. Kwa maneno rahisi, Bunge ndiyo tuna tafuta mkaguzi wa nje ambaye anakagua ofisi hiyo," amesema Spika Ndugai.

"...katika ukaguzi hakuna anayebaki, hakuna anayejikagua mwenyewe," ameongeza Spika Ndugai.

Spika Ndugai na CAG Assad wamekuwa katika mvutano ambao ulianzia mwishoni mwa mwaka jana.

CAG alifanya mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya redio ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York mwezi Disemba 2018 ambapo alisema kuwa Bunge la Tanzania halina meno na hivyo limeshindwa kuiwajibisha ipasavyo serikali.

"…Kama tunatoa ripoti na inaonekana kuna ubadhilifu halafu hatua hazichukuliwi huo kwangu mimi ni udhaifu kwa Bunge. Bunge linatakiwa liisimamie (serikali) na kuhakikisha kuwa pahali penye matatizo basi hatua zinachukuliwa...Sie kazi yetu ni kutoa ripoti tu na huo udhaifu nafikiri ni jambo la kusikitisha lakini ni jambo tunaamini muda si mrefu huenda likarekebishika. Lakini tatizo kubwa tunahisi kwamba bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa," Profesa Assad aliiambia radio ya UN.

Haki miliki ya picha BUNGE

Spika Job Ndugai alilieleza Bunge mwezi Januari kuwa maelezo ya Assad yalioonesha dharau kubwa dhidi ya mhimili huo na kumtaka aende mbele ya kamati kwa hiyari yake, ama apelekwe kwa pingu.

Prof Assad alitokea mbele ya kamati hiyo na kuendeleza msimamo wake, hali iliyopelekea Bunge kuazimia kutofanya kazi naye.

Bado CAG ameendelea na msimamo wake na kuahidi ataendelea klitumia neno dhaifu ambalo Spika Ndugai amesema wanalipinga na hawataki kama bunge wahusishwe nalo.

Ndugai amshukia Masele

Aidha Spika wa bunge Job Ndugai amemsimamisha kwa muda uwakilishi wa mbunge wa Shinyanga Mjini Stephen Masele katika bunge la Afrika (PAP) hadi taarifa rasmi zitakapotolewa.

Kutokana na hilo, amemtaka mbunge huyo kurudi haraka nchini ambako pia atafikia mikononi mwa kamati za maadili za Bunge na chama chake (CCM).

Katika taarifa yake bungeni leo Alhamisi Mei 16,2019, Spika wa bunge Job Ndugai amesema mbunge huyo amekuwa akifanya mambo kinyume na utaratibu na kugonganisha mihimili ya taifa hilo.

"Amefanya mambo ya utovu wa nidhamu huko na taarifa tumezipata na hata kwenye mitandao imeonekana, sasa tumemtaka arudi lakini amegoma hivyo tumeamua kusimamisha kwa muda ubunge wa mheshimiwa huyu hado tutakapotoa taarifa nyingine," amesema Ndugai.

Akizungumzia kugoma kurudi kwa mbunge huyo, anasema alimtaka arudi toka jana lakini bado aliendelea kumgomea akisema Spika hawezi kumuita kwa kuwa ana kibali cha Waziri Mkuu.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii