Jose Mourinho: Meneja wa zamani wa Manchester United amesema hawezi kuwa kibaraka

Jose Mourinho and Paul Pogba Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Jose Mourinho anasema, tatizo linaloikabili timu ya Manchester United ni kubwa zaidi ya hilo la Paul Pogba

Kocha machahchari Jose Mourinho amesema 'mameneja wazuri' katika mpira hugeuka kuwa vibaraka wa timu zao.

Meneja huyo wa zamani wa Manchester United alifukuzwa kazi mwezi Disemba na nafasi yake kuchukuliwa kwa muda na Ole Gunnar Solskjaer, kabla ya Solskjaer kuthibitishwa miezi mitatu baadae.

"Sitaki kuonekana kuwa mtu mzuri "Mourinho ameliambia gazeti la Ufaransa L'Equipe.

"Kwa sababu mtu 'huyo mzuri' baada ya miezi mitatu amekuwa kibaraka ambapo mwisho wake hauwezi kuwa mzuri".

Aliongeza kusema pia :" Kuna wakati mwingine ni kama uko peke yako na hakuna ambaye anakuunga mkono katika klabu, wakati mwingine wachezaji wanatofautiana na kocha , je nani ni mtu mzuri?"

Mchezaji wa zamani wa United, Solskjaer, 46, alianza kibarua chake vyema kwa kushinda michezo 10 kati ya 11 ya mwanzo akiwa kama kocha.

Haki miliki ya picha Getty Images

Hata hivyo, msimu umeisha vibaya kwake huku timu yake ikishinda mechi mbili tu kati ya tisa za mwisho na kumaliza katika nafasi ya sita, mbali kabisa na naasi za kushiriki Klabu Bingwa Ulaya.

Mourinho ambaye aliiongoza United kuwa wapili katika ligi msimu wa mwaka 2017-18 , alisisitiza kuwa hayo yalikuwa mafanikio makubwa sana kwake na sasa watu wameanza kuelewa.

Katika mahojiano na gazeti hilo, amesema "msimu wangu wapili ulikuwa ulikuwa mzuri, ninasema hivyo kwa sababu tulitimiza malengo tuliojiwekea."

"Niliwakamua wachezaji kama machungwa ili tupate matokeo."

Kocha huyo amesema matatizo ya Manchester United ni ya kimfumo na hayaishii tu kwa wachezaji watukutu kama Paul Pogba.

"Matatizo yapo; unaweza kusema kuwa ni wachezaji, taasisi au malengo ya watu" Mourinho alisema.

Lakini pia amekiri kuwa uhusiano wake na Pogba ulikuwa mbaya.

"Lakini si kweli kuwa Pogba ndiye alikuwa chanzo pekee cha matatizo."

Mada zinazohusiana