Waziri Lugola asema video iliyomuhusisha Askofu Gwajima iliundwa

Watu wawili wanashikiliwa kuhusiana na video ya ngono iliyomuhusisha Askofu Josephat Gwajima Haki miliki ya picha GWAJIMA FACEBOOK

Wiki moja baada ya kusambaa kwenye mitandao ya kijamii kwa video ya ngono iliyomuhusisha Askofu Josephat Gwajima, polisi wanasema imethibitisha kuwa video hiyo ilitengenezwa.

Bwana Gwajima alizungumziwa sana wiki iliyopita nchini Tanzania baada ya mkanda wa video ulioonyesha sura inayodaiwa kuwa ni yake kutomwa kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram, kabla ya kusambaa kwenye kurasa za mitandao ya kijamii mbali mbali.

Waziri wa mambo ya ndani nchini humo Kangi Lugola ameliambia gazeti The Citizen nchini humo kuwa watu wawili wanashikiliwa kuhusiana na video hiyo.

''Uchunguzi bado unaendelea, lakini kile ninachoweza kukisema ni kwamba baada ya uchunguzi wetu wa kina uliofanywa na wataalamu wetu, imethibitishwa kuwa video iliundwa'' alisema Lugola.

Kwa mujibu wa Gwajima, video hiyo imetengenezwa na aliowaita maadui zake ambao wanalenga 'kumnyamanzisha'.

Akiongea na wanahabari kwenye viunga vya kanisa lake jijini Dar es Salaam, baada ya kugtumwa kwa video inayomuhusisha kwenye mitandao ya kijamii, Gwajima alisema msimamo wake na maono juu ya nchi ndiyo yamefanya kusingiziwa kashfa hiyo.

"Watu wanafanya haya ili nikose sauti. Wanasema 'tumpige Gwajima ili anyamanze.'" amesema na kuongeza: "Hizi picha zinajaribu kunichafua, lakini hawawezi."

Gwajima, ambaye pia amekuwa kwa namna moja ama nyengine akihusishwa ama kuhusika na siasa alisema: "Uchaguzi unakuja mwaka kesho (2020) na wanajua nina nguvu, hawataki niwe na sauti yoyote."

Hata hivyo, Gwajima hakuwataja kwa majina hao aliowaita kuwa ni maadui zake.

Video hiyo inayodaiwa kuwa ni ya Gwajima inamuonesha aki wa faragha na mwanamke wakifanya tendo la ngono. Na mtu anayedhaniwa kuwa ni Gwajima ndiye alikuwa akiichukua video hiyo kwa kutumia kamera ya mbele ya kifaa ambacho hakionekani.

"Ni mwanaume gani mwenye akili zake timamu anayeweza kujirekodi wakati akifanya tendo la ndoa? Haingii akilini," alijitetea Gwajima na kuongeza, "Zile ni picha za kuunganisha. Wametumia picha yangu moja ya kifamilia nikiwa kifua wazi na kuunganisha na picha nyingine ili wanichafue."

"...mkono wa huyo mtu anayejichukua ile video ni mkubwa, ni mkono wa 'baunsa' sio huu mkono wangu mdogo."

Gwajima pia aliwaambia wanahabari kuwa tayari amesharipoti tukio hilo kwa mamlaka husika na kusema anatumai mtu aliyechapisha picha hizo kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram atakamatwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Askofu huyo aliambatana na viongozi wenzake wa kanisa lake pamoja na mkewe ambaye alieleza kuwa ana imani na mumewe.

"...mimi ni jasiri kama Simba. Ukweli naufahamu. Mume wangu ninamfahamu na ninamwamini. Mungu akiwa upande wetu hakuna wa kutushinda," alisema Bi Gwajima.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii