Siasa Tanzania: Bernard Membe asema yeye na Rostam Aziz wote 'wamekatwa mikia'

Membe vs Magufuli
Image caption Magufuli (kushoto) na Membe (kulia) walikuwa ni miongoni mwa makada wa CCM waliochuana kuwania tiketi ya urais. Je mchuano huo utarudiwa tena 2020?

Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Tanzania Bernard Membe ambaye amekuwa akitajwa kuwa na mpango wa kugombea tiketi ya urais 2020 amesema jina lake si hoja mbele ya masuala ya kitaifa.

Membe ameyasema hayo nje ya jengo la Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam, alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu video iliyoenea mtandaoni ikimuonesha mfanyabiashara na mwanasiasa maarufu nchini Rostam Aziz akizungumzia mjadala wa urais 2020 na kumshauri Membe asijitose kuwania nafasi hiyo ili Rais John Magufuli amalizie awamu ya pili.

Membe amewaambia wanahabari kuwa Rostam hapaswi kuzungumzia mambo yanayomhusu mtu mmoja mmoja na badala yake kutokana na nafasi yake kwenye jamii anatakiwa kuongoza mijadala yenye manufaa kitaifa.

"Napata kigugumizi mno kumjibu rafiki yangu Rostam, lakini Rostam ni mchumi na nitakutana naye nimshauri kuwa anafanya vizuri sana katika jamii ya Watanzania anapozungumzia masuala ya uchumi," amesema Membe na kuongeza "Inabidi azungumze main issues (masuala makuu) ya nchi, siyo personal (watu binafsi), hizi tunaachia watu wa chini, kwa level (hadhi) yetu ni tunazungumzia masuala ya kitaifa ya uchumi. Kwanini uchumi wetu upo hapa ulipo, kwanini wafanyabiashara wadogo na wakubwa wanafunga biashara zao au zile alizozieleza kama economic distortions (upotoshaji wa kiuchumi) tunazijibu vipi."

"Rostam ni mchumi hivyo angejikita katika eneo hilo... asijaribu kuwa Mkristo zaidi ya Warumi ... Yeye (Rostam) ni mwenzetu sisi tumekatwa mkia, ukikatwa mkia hata ujitahidi vipi mkia wako utabaki kuwa mfupi."

Membe pia amewataka wanasiasa kuzungumza vitu ambavyo vinaendana na dhamiri zao, " ...tuwe tunazungumza kitu ambacho binadamu anatuheshimu... Nimshauri tu Rostam akubali status (uhalisia) asijaribu kuwa mtoto mzawa wakati mimi na yeye ni watoto wa kambo."

Membe na Urais

Membe alikuwa miongoni mwa wanachama mashuhuri wa chama tawala Tanzania cha CCM waliojitokeza kuwania tiketi ya urais kupitia chama hicho mwaka 2015.

Machoni mwa Watanzania walio wengi pamoja na wachambuzi wa masuala ya kisiasa, mbio za urais kupitia CCM kwa mwaka 2015 zilikuwa kati ya Membe na Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Edward Lowassa.

Wawili hao walishindwa katika mbio hizo, Lowassa katika raundi ya kwanza na Membe alifikia hatua ya tano bora, mshindi ndani ya chama akaibuka Magufuli.

Baada ya mchakato wa ndani ya chama Lowassa hakuridhika na kutimkia chama cha upinzani Chadema, akagombea urais na kushindwa tena na Magufuli. Lowassa tayari amesharejea CCM.

Membe amesalia CCM, lakini kwa muda mrefu amekuwa akihusishwa na mpango wa kuwania tena tiketi hiyo ya urais dhidi ya Magufuli 2020 ndani ya CCM.

Japo katiba ya CCM haikatazi, lakini imekuwa desturi ya chama hicho kwa mwanachama wake ambaye anahudumu kama rais wa nchi kupita bila kupingwa anapoenda kugombea awamu ya pili na ya mwisho ya urais wa nchi.

Uvumi kuwa Membe amekuwa akipanga kuvunja utamaduni huo ulikolezwa mwishoni mwa mwaka 2018 pale ambapo Katibu Mkuu wa CCM Dkt Bashiru Ali alilivalia njuga suala hilo.

Dkt Bashiru alisema kumekuwa na taarifa kuwa Membe anajipanga kumkwamisha Magufuli ifikapo 2020.

"Iweje watu waseme kwamba wewe (Membe) unafanya vikao vya kutafuta kura za 2020, kwamba unataka kumkomesha Rais Magufuli, halafu unakaa kimya tu?" alisema Bashiru.

Mada zinazohusiana