Msemaji wa waasi waliotangaza vita na Rwanda anaswa

Sankara
Image caption Sankara akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi.

Meja Callixte Sankara aliyekuwa msemaji wa kundi la National Liberation Front lililotangaza uasi dhidi ya Rwanda ameoneshwa mbele ya vyombo vya habari kwa mara ya kwanza toka kukamatwa kwake.

Kiongozi huyo wa waasi alikamatwa nchini Comoro na kupelekwa nchini Rwanda mwezi uliopita.Kwa sasa yuko mikononi mwa idara ya uchunguzi wa makosa ya jinai ya nchi hiyo.

Kundi lake lilidai kuhusika na mashambulio dhidi ya vijiji vilivyo karibu na msitu wa Nyungwe kusini magharibi mwa Rwanda na kudai kuwa bado wapiganaji wake wana ngome katika msitu huo,madai yanayokanushwa na serikali ya Rwanda.

Mwandishi wa BBC Swahili jijini Kigali, Yves Bucyana anaripoti kuwa, Meja Callixte Sankara amefikishwa mbele ya waandishi wa habari akivalia shati la rangi ya samawati na miwani myeusi ya jua na akiwa amepiga miwani ya jua. Alikuwa katikati mwa polisi wawili waliomshika mikono yake na mara kwa mara ameonekana akitabasamu.Hakuzungumza lolote.

Wakili wake Moise Nkundabarashi akazungumza kwa niaba yake kwanza amesema hadi sasa anapozuiliwa anapata huduma zote kama ilivyo haki yake na hana tatizo lolote la afya.

Awali kumekuwa na tetesi kwamba mawakili wengi walikataa kusimama katika kesi hii,waandishi wakata kujua ikiwa mtuhumiwa alijichagulia mwenyewe wakili wake:

''Ni haki ya mtuhumiwa kujichagulia wakili kwa mjibu wa sheria na katiba ya nchi,yeye mwenyewe ndiye aliyenichagua. Kama wengine walikataa mimi sina wasi wasi kwa sababu sheria ya mawakili iko wazi na inatupa uhuru sisi mawakili , hiyo ndiyo inayonilinda."

Kulingana na msemaji wa idara ya uchunguzi Modeste Mbabazi, Sankara anatuhumiwa makosa ya ugaidi na kuunda kundi la kijeshi.

Bwana Mbabazi amejizuia kusema mahali na jinsi mtuhumiwa alivyokamatwa.

''Ninachoweza kusema ni kwamba hakuna mtu anayeweza kukwepa sheria,popote pale anapoweza kujificha tutamnasa.kuwambia kwamba alikamatwa katika nchi fulani au namna gani operesheni ya kumshika ilivyokwenda hayo yote bado yamo katika ngazi ya upelelezi yatafahamika kadri kesi dhidi yake itakavyoendelea."

Sankara ambaye maji yake halisi ni Callixte Nsabimana alikamatwa mwezi wa Aprili katika operesheni iliyoelezewa na vyombo vya habari kuwa ilifanyika visiwani Comoro na kurejeshwa nchini Rwanda.

Alikuwa msemaji wa kundi la National Liberation Front lililotangaza uasi dhidi ya Rwanda na kudai kuhusika na mfululizo wa mashambulio katika vijiji vilivyo kando na msitu wa Nyungwe karibu na mpaka wa Burundi na hadi alipokamatwa bado kundi lake lilikuwa linadai kuwa na ngome katika msitu huo,madai yaliyokanushwa na serikali.

Mada zinazohusiana