Tundu Lissu mashirika ya wanaharakati walalamikia hali ya haki za kibinaadamu Tanzania

Tundu Lissu

Mbunge wa Singida Mashariki kupitia chama cha Chadema na mnadhimu mkuu wa upinzani Tanzania, Tundu Lissu amesema hali ya haki za binaadamu inaendelea kuzorota nchini humo.

Lissu, ambaye yupo nje ya Tanzania toka mwaka 2017 akipatiwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana amechapisha maoni yake na kudai kuwa 'mabolga', wanasiasa, wanahabari, wafanyabiashara, wasanii, wanamuziki — na mtu yeyote anayemkosoa rais wa Tanzania John Magufuli — "wanasakamwa kwa mashtaka mbalimbali."

"Baadhi yao wametekwa na kuteswa, baadhi wamepokonywa pesa. Ni wakati sasa wa rafiki wa Tanzania katika jumuiya ya kimataifa kuungana na kupaza sauti," ameandika Lissu katika maoni hayo yaliyochapishwa mtandaoni na gazeti la Daily Maverick la Afrika Kusini.

Lissu ameeleza kuwa mwanaharakati wa Chadema aliyetekwa na kutupwa porini hivi majuzi mkoani Songwe, Bw Mdude Nyagali ameongea nae na kumweleza kuwa alipata taarifa za kumuonya kuwa maafisa uaslama 'wangemshughulikia' endapo angesalia mkoani humo katika kipindi amabcho Magufuli alikuwa akizuru eneo hilo.

Haki miliki ya picha Mdude/Facebook
Image caption Mdude Nyagali amemwambia Tundu Lissu kuwa hawezi kwenda uhamishoni.

"Pia (Mdude) amegoma kwenda uhamishoni nje ya nchi kwa muda baada ya marafiki zake na baadhi ya wanachama wa Chadema kumtaka afanye hivyo kutokana na kuongezeka kwa matishio dhidi ya maisha yake. Ameniambia kuwa hawezi ihama nchi kwasababu 'bado kuna kazi nyingi za kufanya ndani ya nchi'," ameandika Lissu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Songwe, George Kyando, hata hivyo ameiambia BBC kuwa vyombo vya usalama havihusiki na kilichomtokea mwanaharaki huyo wa upinzani ambaye ni maarufu zaidi mitandaoni.

Asasi 38 zaishtaki Tanzania UN

Wakati huo huo, taasisi 38 za kupigania haki za binaadamu duniani zimeandika barua ya wazi kwa nchi wananchama na waangalizi (waalikwa) wa Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa (UN) wakitaka hali ya Tanzania kuangaliwa kwa mapana yake.

"Japo hatuamini kwa hatua ya sasa, hali ya (Tanzania) inahitaji kupitishwa kwa azimio, (lakini) kuna dalili za hatari juu ya uwepo wa janga la haki za kibinaadamu," imeeleza sehemu ya barua hiyo.

Barua hiyo kwa Tanzania imesainiwa na Kitua cha Haki za Binadamu (LHRC) na Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) na baadhi ya amashirika ya kimataifa yaliyosaini barua hiyo ni Amnesty International, Human Rights Watch, Kamati ya Kutetea Waandishi wa Habari na Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka.

Image caption Wanaharakati hao pia wamegusia kupotea katika mazingira ya kutatanisha kwa mwanahabari Azory Gwanda ambaye Februari 2018 zilitimia siku 100 toka kutoweka kwake na mpaka leo bado hajapatikana.

Kwa mujibu wa barua hiyo, waandishi wa habari, wapinzani na wakosoaji (wa serikali), watetezi wa haki za binaadamu na wapenzi wa jinsia moja, "wote wamo kwenye shinikizo kali huku serikali ikipitisha sheria kandamizi ambazo zinatishia uhuru wa habari na kujieleza."

Serikali ya Tanzania hata hivyo imejibu tuhuma hizo kwa kuziita ni propaganda zinazofadhiliwa na baadha ya nchi za kigeni.

"Tunajua kuwa kuna baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotumika na baadhi ya mataifa makubwa yameandika barua kwenda UN kulalamikia hali ya hakiza binaadamu Tanzzania. Lakini tulichokiwasilisha sisi (ripoti) kitasimama kama msimamo wa serikali kwenye suala lolote la haki za binaadamu nchini," amesema Msemaji wa Serikali ya Tanzania Dkt Hassan Abbas na kunukuliwa na gazeti la The East African.

Mkutano wa 41 wa Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa (UN) unatarajiwa kufanyika kuanzia Juni 20 mpaka Julai 21 mwaka huu. Hii na mara ya pili kwa wanaharakati kulitaka baraza hilo kuiangazia Tanzania, mara ya kwanza ilikuwa mwaka jana 2018.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii