Moise Katumbi: Kiongozi wa upinzani DR Congo arudi nyumbani Lubumbashi kutoka uhamishoni

Moise Katumbi Haki miliki ya picha FISTON MAHAMBA

Kiongozi wa upinzani wa Jamhuri ya Kidmeokrasi ya Congo Moise Katumbi amelakiwa na maelfu ya wafuasi Lubumbashi baada ya kuishi uhamishoni kwa takriban miaka mitatu.

Katumbi amepokewa na maelfu ya wafuasi waliojawa na furaha na shangwe katika uwanja wa ndege wa Luano nchini Congo.

Kiongozi huyo wa upinzani amekuwa akiishi uhamishoni kwa miaka zaidi ya miwili iliyopita baada ya kushtakiwa na serikali ya rais wa zamani Joseph Kabila kwa makosa kadhaa ya uhalifu ukiwemo udanganyifu, kuwajiri maamluki na kujipatia uraia wa pili kinyume cha sheria.

Umati ulionekana ukimsindikiza Moise Katumbi kuelekea katika uwanja wa michezo wa TP Mazembe.

Haya yanajiri wakati rais Tshisekedi anatarajiwa kuhotubia taifa baadaye hii leo.

Image caption Umati wa watu umekusanyika katika barabara kuu kumpokea Moise Katumbi aliyerudi Congo baada ya kuishi uhamishoni kwa zaidi ya miaka miwili

Katika mahojiano na televisheni ya FRANCE 24, Katumbi alisema kwamba anapanga kurudi nyumbani Mei 20 - ikiwa ni takriban miaka mitatu tangu aondoke nchini.

"Ni hakika kwamba Mei 20, nitakuwa Lubumbashi," Katumbi amenukuliwa na katika mahojiano hayo yaliofanyika Mei 6.

Alieleza kwamba baada ya kurudi Lubumbashi anapanga ziara ya kitaifa katika alichotaja kuwa ni 'kuwaliwaza' raia wa DR Congo, hususan "familia zilizoteswa […] na walioishi katika tabu".

Mnamo 2016, Moise Katumbi, alihukumiwa kifungo cha miaka 3 jela kwa kununua nyumba kinyume cha sheria kwenye mji ulio mashariki mwa nchi wa Lubumbashi na pia kutuhumiwa kwa kuwaajiri mamluki wa kigeni ili kupanga njama dhidi ya serikali.

Image caption Rais felix Tchisekedi (kulia) akiwa pamoja na mtangulizi wake Joseph kabila

Wakati wa kuapishwa kwake, Rais mpya wa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Felix Tshisekedi, aliahidi kuwaachilia huru wafungwa wote wa kisiasa wakiwemo watu wote waliofungwa wakati wa maandamano yaliyofanyika kabla ya uchaguzi wa mkuu wa mwezi wa Disemba mwaka jana.

Mashtaka dhidi ya Katumbi mwanasiasa mwenye umri wa miaka 54 yametupilia mbali chini ya utawala wake Tshisekedi, na kutoa fursa leo kwa Katumbi kurudi nyumbani.

Hatahivyo mpinzani huyo ameeleza kwamba uamuzi wa mahakama kubatilisha hukmu ya miaka mitatu dhidi yake sio kutokana na makubaliano na rais Félix Tshisekedi, badala yake mfumo wa sheria ambao sasa hauingiliwi kisiasa.

Moise Katumbi ni nani?

  • Jina lake la mwisho pia Tshapwe
  • Anajulikana kama Moses Katumbi nchini Zambia, ambapo aliishi kwa miaka mingi
  • Tarehe ya kuzaliwa 28 Disemba 1964
  • Eneo la kuzaliwa ni Kashobwe
  • Ni kabila la Babemba
  • Ni kaka wa kambo wa Katebe Katoto, maarufu kama Rafael Soriano, na mfuasi wa Laurent Nkunda
  • Baba yake ni Padre Nissim Soriano, Mitaliano Myahudi kutoka Rhodes
  • Mama yake ni Virginie Katumbi, kutoka familia ya kifalme ya Kazembe
  • Rais wa kalbu ya Soka TP Mazembe Football iliopo Lubumbashi
  • Anajullikana kwa mapenzi yake na kofia za mtindo 'Cowboy'

Katumbi, na Jean Pierre Bemba, kigogo mwingine wa upinzani Congo walimuunga mkono Martin Fayulu, katika uchaguzi mkuu nchini humo ambao Tshisekedi alichaguliwa rais.

Katumbi ni kiongozi wa upinzani ambaye amekuwa uhamishoni kutoka DR Congo baada ya kutengana na Rais Joseph Kabila.

Huwezi kusikiliza tena
Moise Katumbi asema anapanga kurejea DRC

Katumbi, alijiunga na upinzani mnamo 2015 baada ya kukosana na rais Joseph Kabila, wakati huo.

Katumbi ambaye amewahi kuwa Gavana wa jimbo tajiri zaidi nchini humo, Katanga alijiuzulu na kumshtumu rais Kabila kwa uongozi duni.

Moise Katumbi ni kiongozi wa pekee wa upinzani nchini Congo ambaye ana ushawishi mkubwa na ufuasi mkubwa miongoni mwa raia wa Congo.

Alitangaza kutaka kuwania urais mwaka 2016, kabla ya uchaguzi huo kuahirishwa. Na mwaka jana alizuiwa kuingia nchini kugombea urais katika uchaguzi wa Desemba, aliyoushinda Tshisekedi.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii