Mdude Nyagali: Mwanasisa wa Chadema ahusisha kutekwa kwake na siasa Tanzania

Mdude

Mwanaharakati wa chama cha upinzani nchini Tanzania Mdude Nyagali amehusisha matuko ya kutoweka kwake kwa muda wa siku tatu huko Mbeya kuwa ni utekaji unaotokana na masuala ya kisiasa.

"Mimi nilitekwa sikupotea, lile eneo nimeishi kwa miaka 20 siwezi kupotea".

"Ninathibitisha kuwa tukio lililonitokea ni la kisiasa sio la Kijambazi maana maisha yangu ni chini ya dola 100 kwa mwezi" Mdude ameelaza waandishi habari hii leo.

Aliongeza kusema kuwa analihusisha na siasa kwa sababu waliomshabulia na waling'ang'ania nyaraka za chama pamoja na za mahakamani wakati wa tukio hilo.

"Kwanini waliniambia niite Umoja wa Ulaya waje wanisaidie, kwanini waliniambie nimwambie Mbowe na Lissu waje wanisaidie?"

Mdude ambaye aliokolewa na wanakijiji ambao walimpeleka katika hospitali ya eneo hilo alipatikana akiwa mchovu na aliyeteswa wakati wa kipindi chote cha utekaji wake.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo Mei 20, jijini Dar es salaam Mdude alisimulia mkasa wa utekaji wake.

" Wale watu watatu walivyonikamata walisema wao ni askari na kuniambia kuwa ninatuhumiwa kumtukana rais kwenye mitandao ya kijamii".

Hatahivyo, Polisi wamewahi kukanusha kuhusika na kutekwa kwake na kueleza kwamba wanafanya uchunguzi juu ya tukio hilo.

" Nilipiga kelele kuomba msaada lakini walikua wananiziba mdomo.

Mmoja alitoa bastola akaikoki, halafu akageukia wananchi ambao walikuwa wamejaa pale wakati nmepiga kelele ili kuwatisha wananchi", anasema.

"Hapo walifanikiwa kunibeba wakanipeleka kwenye landcruiser wakaniweka kwenye buti.

Wale watu kwenye gari walinishambulia kwa pamoja na chupa za bia na rungu" ameendelea kusimulia Nyagali.

"Nilipigwa kwa muda wa saa moja hivi ndio nikapoteza fahamu. Nilipokuja kushtuka nikajikuta nimelala kifudifudi wameniwekea tape mdomoni na kunifunga kitambaa cheusi Kwenye macho, nilihisi nimekua kipofu Kitu cha kwanza niliomba maji.

Mwisho wa siku wakasema umekula? Nikawaambia nimekula jioni mimi nikijua ni siku ile ile kumbe siku nne zimepita. wakanipa maji na uji.

Mpaka napoteza fahamu sikupigwa sehemu nyingine yeyote zaidi ya kichwa "

Mdude amehusisha matukio yaliomfikana ujumbe aaliyoandika kwenye mtandao wa Tweeter kuhusu alichokitaja kuwa ni wakili ambaye alikuwa akishikiliwa na vyombo vya dola.

Vilevile Mdude amekuwa akikosoa utendaji kazi wa serikali ya chama tawala CCM kwenye majukwaa ya kisiasa pamoja na katika mitandao ya kijamii.

Ametumia mitandao ya kijamii kama twitter kuikosoa serikali kama katika ujumbe huu wake wa mwisho wiki iliyopita kabla ya taarifa za kupotea kwake kuchipuka.

Msemaji wa polisi Tanzania

Kamishina msaidizi wa Polisi, David Misime ameiambia BBC kuwa Mdude alifika katika kituo cha polisi na kuandika maelezo ambayo aliona yanaweza kusaidia jeshi la polisi kufanya uchunguzi, hivyo walichukua taarifa na kufungua jalada la kesi yake huku wakiendelea kufanya uchunguzi na watakapokamilisha uchunguzi huo watatoa taarifa.

"Tunafanya kazi yetu kitaalamu kwa mujibu wa maelezo aliyotoa na tunafanyia kazi na ukweli utabainika na kama kuna hatua za kuchukuliwa zitachukuliwa" Kamishina Misime alisisitiza.

Awali baada ya taarifa za kutekwa Mdude kusambaa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, George Kyando alikanusha katika mahojiano yake na Gazeti la Mwananchi nchini Tanzania kusikika kwa milio ya risasi, siku iliotajwa.

"Mimi ni mkazi wa eneo linalodaiwa kuwa risasi zimepigwa lakini sijasikia na kama unavyojua mji wa Viwawa ni mdogo ambao zikipigwa risasi lazima utasikia," alisema.

Kamanda Kyando aliahidi kwamba ataendelea kufuatilia kwa kina taarifa hizo.

''Nikiwa ndani ya gari lile nilipigwa sana kwa kutumia chupa , walivua viatu nilivyokuwa nimevaa wakanipiga navyo usoni na masikioni na baadaye kunifunga kamba usoni na mdomoni na nikapoteza fahamu'', aliongezea Mdude.

Anasema kwamba alipopata fahamu alijipata katika msitu akiwa hajui aliko.

Je Mdude Nyaghali ni nani?

Kwa mujibu wa Chadema, mtiririko wa matukio haya yalioorodheshwa na John Mrema, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, ndiyo yanayowapa mashaka kwamba vyombo vya dola vinahusika katika yaliomkuta Mdude:

Agosti 26 2016: Mdude akamatwa Vwawa

Agosti 28 2016: Ahamishiwa kambi ya FFU Mbeya

Agosti 29: Apelekwa Dar es Salaam na kuwekwa Osterbay polisi

Septemba 1 2016: Apelekewa hospitali ya Mwananyamala Dar Es Salaam kufuatia madai ya kuteswa

Septemba 13: Polisi wamuondoa hospitali Mwananyamala na kumepeleka Vwawa.

Septemba 14: Afunguliwa kesi ya mashtaka ya kuandika uongo.

Aprili 2017: Mdude ashinda kesi.

Novemba 2017: Akamatwa tena Vwawa na kupelekwa Dar Es Salam ambako aliwekwa kituo cha Polisi cha Central kwa siku 21. Baada ya hapo arudishwa Vwawa ambako afunguliwa kesi ya uchochezi

Novemba 2018: Kwa mara nyingine Mdude ashinda kesi Novemba 2018.

Januari 2019: Mdude aandika notisi ya kulishtaki Jeshi la polisi

Machi 2019: Afungua kesi mahakama kuu kanda ya Mbeya na kumshtaki Inspekta Jenerali wa polisi, RPC wa Songwe, Mwanasheria mkuu wa serikali na askari polisi watatu.

Hatahivyo, Polisi wamekanusha kuhusika na kutekwa kwake na wanaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo.

Chama kikuu cha upinzani Chadema wamevitaka vyombo vya usalama kutoa taarifa kuhusiana na madai ya kutekwa, kuteswa na kisha kukutwa akiwa ameumizwa Mdude Nyagali.

Inaarifiwa wanakijiji walimpata ametupwa katika kijiji cha Makwenje , wadi ya Inyala katika jimbo la Mbeya.