Iran: Wachokozi wote wameangamia na taifa letu limesalia

waziri wa maswala ya kigeni wa Iran Mohammad Javad Zarif (24 April 2019)

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Mohammad Javad Zarif amesisitiza kuwa Iran haitaki vita na Marekani

Waziri wa maswala ya kig ni nchini Iran Javad Zarrif amepuuzilia mbali madai ya rais Donald Trump ya kuiangamiza Iran na kumuonya kutolitishia taifa hilo.

Huku kukiwa na hali ya wasiwasi , bwana Trump alituma ujumbe wa Twitter siku ya Jumapili akisema: Iwapo Iran inataka kupigana hiyo ndio utakuwa mwisho wake.

Bwana Zarif alisema kuwa rais huyo wa Marekani anafaa kutazama historia. '' Iran imeshinda vita vyote dhidi ya wachokozi wake ...jaribu kuwa na heshima -utafanikiwa!

Marekani imeongeza idadi ya meli na ndege zake za kivita katika eneo la mashariki ya kati katika siku za hivi karibuni.

Ujumbe huo wa Bwana Trump unaadhimisha mabadiliko ya matamshi yake baada ya kusema kuwa hakutakuwa na vita kati ya Marekani na Itran.

Alipoulizwa na maripota siku ya Alhamisi iwapo Marekani itaelekea katika vita , alisema: Sidhani.

Vyombo vya habari vya Iran viliripoti siku ya Jumatatu kwamba taifa hilo limeongeza mara nne uzalishaji wa madini ya Uranium ambayo yalikuwa yamepunguzwa hadi kilo 300 na mpango wa kinyiuklia wa 2015 kati ya Iran na mataifa yenye uwezo mkubwa duniani.

Msemaji wa shirika la kawi ya Atomiki Behrouz Kamalvandi, amesema kuwa Iran itazidisha kiwango cha uzalishaji wa madini ya Uranium na kupitisha kiwango ilichowekewa katika siku za usoni.

"Iwapo wanataka sisi kusalia na kiwango tulichokubaliana katika makubaliano ya mpango huo wa kinyuklia , basi itakuwa vyema kwa mataifa ya Ulaya kuchukua hatua inazotaka ili kutekeleza haraka iwezekanavyo.

Bwana Trump aliiondoa Marekani katika mkataba huo ,mwaka uliopita , lakini mataifa ya Ulaya yanasema kuwa bado yanaheshimu makubaliano hayo.

Onyo la rais huyo wa Marekani siku ya Jumapili lilitolewa saa chache baada ya roketi kurushwa katika eneo linalolindwa sana katika mji mkuu wa Iraq, baghdad na kupiga jengo moja yapata mitaa 500 kutoka katika ubalozi wa Marekani.

Marekani hivi majuzi iliwaondoa wafanyikazi wake nchini Iraq katka kile ilichokitaja kuwa tishio kutoka kwa vikosi vinavyoungwa mkono na Iran nchini Iraq.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Roketi ilianguka mita 500 kutoka kwa ubalozi wa Marekani uliopo mjini Baghdad Iraq

Akiandika siku ya Jumatatu , waziri wa maswala ya kigeni nchini Iran alisema kuwa rais huyo wa Marekani alikuwa akishinikizwa na kile alichokiita Kundi B - mshauri wake wa Usalama John Bolton, Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na mwanamfalme wa Saudia Mohammad bin Salman.

''Bwana Trump anataka kupata mafanikio pale ambapo Alexander The Great, Genghis[Khan} na wachokozi wengine walishindwa kufanya. Raia wa Iran wamesimama huku wachokozi wakianguka.

''Uchokizi wa ugaidi wa kiuchumi na uchokozi mwengine wa kuangamiza watu hautaimaliza Iran'', aliongezea.

''Usijaribu kuitishia Iran ,jaribu kuiheshimu utafanikiwa''.

Je chanzo cha uhasama huo ni nini?

Uhasama huo ulianza mapema mwezi huu , wakati Marekani iliondoa msamaha wake wa vikwazo kwa mataifa yanayonunua mafuta kutoka kwa Iran.

Uamuzi huo ulilenga kusitisha uuzaji wa mafuta wa Iran katika mataifa ya kigeni hatua ambayo ingelinyima taifa hilo chanzo cha mapato.

Bwana Trump aliirudishia vikwazo Iran baada ya kujiondoa katika mpango wa kinyuklia wa 2015 kati ya Iran na mataifa yenye uwezo mkubwa duniani ambao anataka ujadiliwe tena.

Siku chache baadaye, rais wa Iran Hassan Rouhani alisema kuwa taifa linasitisha vikwazo ilivyowekewa katika makubaliano hayo na kutishia kuongeza uzalishaji wa madini ya Uranium iwapo mataifa ya magharibi hayatachukua hatua za kulinda mafuta yake na sekta yake ya benki kutokana na athari za vikwazo vya Marekani kwa miezi miwili.

Baadaye ikulu ya Whitehouse ilitangaza kwamba Marekani ilikuwa inatuma meli ya kubeba ndege za kivita B-52 pamoja na kifaa cha kutungua makombora angani katika eneo la mashariki ya kati kutokana na vitisho vya Iran.

Je mataifa mengine yanasema nini?

"Ningeishauri Iran musidharau ari ya Marekani , alisema waziri wa maswala ya kigeni wa Uingereza Jeremy Hunt.

''hawataki vita na Iran. lakini iwapo maslahi ya Marekani yatashambuliwa , watalipiza kisasi''.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Meli ya kubeba ndege ya marekani USS USS Abraham Lincoln

"Tunataka hali ya wasiwasi kupungua , kwasababu huu ni ulimwengu ambao mambo yanaweza kuchochewa kwa urahisi'' ,aliongezea.

Waziri wa maswala ya kigeni nchini Saudia Adel al-Jubeir alisema kuwa Ufalme wa Saudia hautaki vita na utatumia kila njia kusitisha vita.

"lakini upande mwengine iwapo utataka vita , Ufalme huo utajibu na nguvu zake zote kujitetea na kulinda maslahi yake''.

Waziri wa maswala ya kigeni nchini Oman ambayo ilisimamia mazungumzo ya kisiri hapo zamani kati ya Marekani na Iran, alizuru Iran ili kujadiliana kuhusu maswala ya kieneo na waziri wa maswala ya kigeni nchini Iran Javad Zarif siku ya Jumatatu.