Ni nani asiyepaswa kufunga mwezi wa Ramadhani?

waumini wa kiislamu Haki miliki ya picha MOHAMED EL-SHAHED

Wakati mwezi wa Ramadhani umejigawanya nusu tayari kuna changamoto kwa baadhi ya watu ambao inafanya kuwa vigumu wao kukamilisha funga zao. Swali kuu linaloulizwa ni je ninapswa kuendelea na saumu?

Katika mwezi huu ambao ni mtukufu kwa waumini wa kiislamu, waislamu wanahimizwa kujiepusha na maovu na kutekeleza mema.

Dhamira sio tu kuacha kula chakula na maji, lakini pia kutumia muda huu kama kujikumbusha manufaa ya kujiepusha na mambo yanayokatazwa mfano hasira, kugombana, vita, kijicho, matamanio na zinaa, masimango na kusengenya na kadhalika.

Badala yake waumini huhimizwa kujaribu kuishi kwa amani na kusikizana zaidi ya inavyokuwa kawaida.

Hatahivyo wakati waumini wote wanajizuia kula na kunywa katika kipindi hiki, kuna wanaoruhusiwa au wasioshurutishwa kufunga na kwa sababu tofuati.

Hawa ni baadhi ya watu walio na hiari ya kutofunga au wanaoruhusiwa kuvunja saumu zao katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Haki miliki ya picha Eric Lafforgue/Art in All of Us

1. Wazee

Wazee wasiojiweza wameruhusiwa kutofunga au hata wale wanaofunga kwa tabu pia wana hiari ya kuacha kufunga katika mwezi wa Ramadhan.

Hatahivyo baadhi ya viongozi wa kidini wanaeleza kwamba ni wajibu kwao kulipa 'fidyah' au kibaba kama kinavyofahamika na wengi kilicho sawa na kiasi ya kilo moja na nusu ya chakula. Msaada unaotolewa kwa masikini kufidia kila siku ambayo hakuifunga. Viongozi wengine wanasema sio lazima ila inapendekezwa kwao kulipia siku hizo ambazo hawakuzifunga.

Haki miliki ya picha STEFAN HEUNIS

2. Wanawake kwenye hedhi/damu ya uzazi

Ni lazima kwa mwanamke wa kiilsmau anayefunga kuvunja saumu yake punde anapoingia katika hedhi au anapovuja damu ya uzazi (Nifas).

Inakwenda kinyume cha dini kwa mwanamke kuendelea kufunga wakati akiwa katika hedhi.

Na saumu yake huwa haifai. Hivyo ni kama kufunga njaa tu. Hatahivyo anatakiwa kuzilipia siku alizokosa kufunga wakati wa Ramadhani kutokana na hedhi katika siku za mbele na inapendekezwa azikamilishe kabla ya mwezi mwingine ujao wa Ramadhani.

Mengine muhimu kuhusu funga ya Ramadhan 2019

Haki miliki ya picha Monique Jaques

3. Wanawake waja wazito na wanaonyonyesha

Wanawake waja wazito na wanaonyoNYesha wanaweza kutofunga katika Ramadhan, iwapo wanahisi watakuwa wanahatarisha afya zao au za watoto wao.

Imewasilishwa katika ayah ya Quran:

"na kwa yoyote aliye mgonjwa au kwenye safari, idadi ya siku (ambazo hawakufunga) walipie katika siku nyingine" [al-Baqarah 2:185]

Hatahivyo iwapo mwanamke mja mzito anajihisi kuwa na afya nzuri na nguvu na kwa ushauri wa daktari wake anaweza kuendelea na saum yake,

Na iwapo watakapoweza kulipiza basi wafanye hivyo pasi kuhitajika kulipa 'fidyah'.

Haki miliki ya picha Eric Lafforgue/Art in All of Us

4. Wasafiri

Wasafiri wa muda mrefu wanaruhusiwa kuvunja saum yao iwapo:

  • Safari ni ndefu mno kiasi cha kulazimika kuchanganya na kuzifupisha swala.
  • Iwapo msafiri hana dhamira ya kuishi katika sehemu anakoelekea
  • Safari isiwe na dhamira za kukiuka dini, bali kwa madhumuni ya maana.

Ni kinyume cha sheria za dini kutofunga iwapo safari ni ya masafa au umbali mdogo.

Haki miliki ya picha FLORENT VERGNES

5. Wagonjwa

Ugonjwa - wakati mtu anapokuwa katika hali ya afya isio nzuri. Mfano ni magonjwa ya kudumu au ya muda mrefu kama kisukari, mgonjwa anaruhusiwa kutofunga, hata hivyo watatakiwa kulipia fidya ya kila siku ambayo hawakufunga maarufu 'kibaba'.

Kwa wanaogua magonjwa ya muda mfupi, mfano homa au maambukizi, wanaruhusiwa kutofunga iwapo afya zao haziwaruhusu kwa wakati huo lakini watatarajiwa kuzilipa siku hizo walizokula kabla ya Ramadhani nyingine kuingia.

Kwa baadhi ya wasomi, kuvunja saum mtu anapozidiwa kwa ugonjwa ni sunna - mafundisho ya Mtume Muhammad (SAW) na wengine huona ni makruh tendo linalokirihisha iwapo mgonjwa ataendelea kufunga licha ya afya kutomruhusu.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii