Kwanini bado Afrika mashariki na kati zinaendelea kushuhudia majanga ya majini?

ajali hiyo ya kivuko cha MV Nyerere.
Image caption Ajali ya kivuko cha MV Nyerere ambayo iliua zaidi ya watu 200

Ni miaka 23 tangu kisa cha ajali ambayo inatajwa kuwa mbaya zaidi katika karne kutokea barani Afrika katika ziwa victoria nchini Tanzania.

Ni janga ambalo lilisababisha idadi kubwa ya watu wapatao 1000 kupoteza maisha baada ya meli ya Mv Bukoba kuzama.

Sababu ambayo ilitajwa kusababisha ajali hiyo ilikuwa idadi ya abiria kuzidi, chombo kuwa na itilafu, pamoja na vifaa vya ukozi kuwa vichache.

Pamoja na ajali hiyo kubwa kuacha simanzi kwa baadhi ya familia hadi sasa, ni fundisho gani kwa kisa cha namna hiyo kutotokea tena?

Lakini bado Tanzania na Afrika mashariki na kati zinaendelea kushuhudia ajali ambazo sababu ya kutokea au watu kupoteza maisha zikiwa zinafanana.

Mwaka jana, Septemba 2018 jumla ya watu 224 walifariki na watu wengine 41 wakiokolewa wakiwa hai katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere.

Tanzania iliweza kushuhudia pia ajali za maji ikiwemo za bahari ya hindi Mv Skagit na Mv Spice Islander nazo ziliweza kupoteza idadi kubwa ya watu.

Ni wiki hii tu (Mei 20) ambapo ajali nyingine ya maji imetokea na kuua watu 16 huku wengine wakiwa hawajulikani walipo huko nchini Uganda.

Boti iliyokuwa imebeba wacheza mpira 50 wakiwa na mashabiki wao huko Magharibi mwa Uganda.

Huku ikikumbukwa kuwa mwaka 2016 , wachezaji 30 wakiwa na mashabiki wao walizama katika ziwa Albert na watu 20 walifariki.

Mwaka 2018 nchini Uganda, watu 29 walifariki kufuatia ajali ya mashua iliyotokea ziwa Victoria.

Mashua hiyo iliyokuwa na watu zaidi ya 90 waliokuwa wanaelekea sherehe, ilipata ajali katika kaunti ndogo ya Mpatta wilaya ya Mukono.

Wasanii kadhaa na watu wengine mashuhuri waliaminika kuwa kwenye mashua hiyo..

Maafisa walisema kwa mashua mbili za uvuvi ambazo ziliwasili kuokoa nazo zilifurika watu na kuzama.

Mwaka 2014, Umoja wa Mataifa ulisema kuwa takriban watu 98, wamekufa maji baada ya boti walimokuwa wanasafiria kuzama katika Ziwa Albert Magharibi mwa Uganda.

Boti iliyozama ilikua imebeba zaidi ya wakimbizi 100.

Aliyekuwa anaendesha boti hiyo alikamatwa na jeshi la polisi na inadaiwa kuwa alikua mlevi.

Hii sio mara ya kwanza ajali ya boti kuua watu katika Ziwa Albert kutokana na kujaza abiria na mizogo kupita kiasi.

Watu 50 wamefariki nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya boti kuzama kwenye mto kaskazini mwa nchi hiyo.

Mwaka 2010, ajali ya boti nchini Uganda iliuwa watu zaidi ya 70 baada ya mashua waliokuwa wakisafiria kuzama katika ziwa Albert nchini Uganda.

Ajali hii ilitokea eneo lijulikanalo kama Kakoma katika kijiji cha Runga, Wilaya ya Hoima.

Mwaka huu, Aprili 2019, takriban watu 150 wametoweka baada ya boti kuzama katika ziwa moja mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na watu 33 wakaokolewa katika ajali hiyo.

Kulingana na Reuters mwaka uliopita , boti moja lilipinduka katika mto kaskazini mwa DR Congo , na kusababisha watu 49 kufa maji huku idadi kama hiyo ya watu wakiokolewa.

Mwaka wa 2015, zaidi ya watu 100 walitoweka baada ya maboti mawili kugongana katika mto Congo nchini DR Congo kulingana na shirika la afya duniani WHO.

Mnamo mwezi Julai 2011, zaidi ya watu 100 walifariki baada ya boti mbili kugongana katika mto katika eneo la mkoa wa Equateur la DR Congo.

Swali kuu kutokana na visa hivi vyote kieneo ni je, funzo gani linalotokana na majanga haya majini?

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii