Timu ya La Liga Sevilla FC kutua Tanzania kwa mpambano wa kirafiki dhidi ya Simba SC

Sevilla celebrate Haki miliki ya picha EPA

Timu ya La Liga Sevilla FC ipo njiani kuelekea Tanzania kwa mpambano wa kirafiki dhidi ya vinara wa ligi ya Tanzania Simba SC.

Mapema leo, timu hiyo ya ligi ya Uhispania imeondoka kuelekea Tanzania kwa mchuano wa kirafaiki dhidi ya timu ya Tanzania Simba SC Alhamisi wiki hii.

Mpambano huo ni sehemu ya kampeni ya 'LaLiga World Challenge' inayonuiwa kusambaza soka ya Uhispania duniani kutokana na kuongezeka kwa ushabiki wa ligi kuu ya Uhispania LaLiga.

Mashabiki sugu wa soka Tanzania wanasubiria mchauno huo kwa shauku kubwa.

Katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii Instagram kikosi cha Sevilla kimetuma ujumbe kwamba kipo njiani:

Kikosi hicho inaarifiwa kinajumuisha Vaclík, Juan Soriano, Sergi Gómez, Kjaer, Gnagnon, Jesus Navas, Aleix Vidal, Escudero, Arana, Amadou, Roque Mesa, Banega, Franco Vazquez, Nolito, Promes, Bryan, Ben Yedder na Munir.

Simba SC ni mabingwa mara 19 Tanzania na wamefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika baada ya kusubiri kwa miaka 25.

Moja ya chachu ya ushindi kwa Simba wakiwa nyumbani ni nguvu kubwa ya mashabiki wao ambao wamekuwa wakiujaza Uwanja wa Taifa unaoingiza mashabiki 60,000.

Baadhi wakionekana tayari kunoa makali kufuatia kuwadia kwa mchuano huo wiki hii katika uwanja wa taifa Dar es Salaam.

Sevilla FC ni klabu ya kwanza ya Uhispania kuizuru Tanzania kucheza mechi ya kirafiki na ni ya pili Ulaya baada ya Everton kushuka pia mnamo 2017 ilipochuana na timu bingwa Gor Mahia kutoka Kenya katika mashindano ya Sport Pesa.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii