Raia wa Uchina, Uturuki na Uhispania wafukuzwa Kenya kwa kuendesha kisiri biashara za kamari

Wengi wanatumia simu kuweka dau

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Wengi wanatumia simu kuweka dau

Raia 17 wa kigeni wamefukuzwa kutoka nchini Kenya kufuatia mpango wa serikali wa kukabiliana na uraibu wa mchezo wa kamari.

Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya waziri wa usalama wa kitaifa Fred Matiang'i kumuagiza katibu wa kudumu wa uhamiaji kuchunguza kuwachunguza raia wa kigeni ambao wameomba leseni ya biashara lakini wakaishia kuwekeza katika kampuni za kamari au mchezo wa bahari nasibu.

Wale waliyofukuzwa kutoka nchini humo wanatokea mataifa ya China, Uturuki na Uhispania.

Kenya kwa sasa ina zaidi ya kampuni 30 za kamari na kasino ambazo zimeidhinishwa lakini ni chache kati ya hizo ambazo zinahudumu.

Chanzo cha picha, Getty Images

"Hatuwezi kutumia kigezo cha kukusanya kodi kuidhinisha sekta iliyojaa mashaka.. zaidi ya 90% ya wadau wakuu wa mchezo huo ni raia wa kigeni na wengi wao wanatuma fedha nyingi sana katika mataifa yao'' Waziri Matiang'i aliviambia vyombo vya habari nchini humo.

"Inashangaza kuwa umaarufu wa mchezo wa kamari nchini Kenya umeathiri sana maisha ya kijamii na kiuchumi kuwanufaisha watu wachache amabo wengi wao si wakenya na wanaishi nje ya nchi,"aliongeza Bw. Matiang'i.

Sekta ya mchezo huo siku za hivi karibuni imepata umaarufu mkubwa kutokana na matangazo ya biashara yanayojumuisha wachezaji mashuhuri.

Inakadiriwa kuwa mchezo huo unaipatia Kenya kima cha dola milioni saba kila mwezi na karibu dola milioni 100 moja kila mwaka, kwa mujibu wa asasi inayodhibiti mchezo wa kamari.

Ripoti ya hivi karibuni ya kampuni ya Price water house Coopers inaonesha kuwa thamani ya kampuni zinazoendesha biashara ya kamari nchini Kenya imefikia dola milioni 20 kwa mwaka na thamani hiyo inatarajiwa kufikia dola milioni 50 ifikapo mwaka 2020.

Ripoti hiyo pia ilisema kuwa Kenya ni taifa la tatu nyuma ya Afrika Kusini na Nigeria kukusanya kodi kubwa kutokana na uchezaji kamari.

Waziri Matiang'i alilalamikia jinsi kampuni hizo zinavyoendelea kuwafunza watu ambao tayari wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha hususan vijana.

Je ni kweli vijana ndio wanaocheza kamari zaidi?

Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa katika mji mkuu wa Uganda, Kampala, umegundua kwamba wengi walioshiriki kamari walifanya hivyo kupata kipato, kujikimu maisha na sio kwasababau za starehe.

Utafiti huo wa taasisi ya Economic Policy Research Centre, imeashiria kwamba 45% ya wanaume Uganda walio na umri wa kati ya miaka 18-30 walijihusisha zaidi na aina fulani ya kamari, ikilinganishwa na takriban robo ya watu wazima wote.

Utafiti huu, umegundua kwamba "wanaocheza kamari kukabiliana na umaskini wanakabiliwa na uwezekano mkubwa wa kuwa waraibu kuliko wale wanaocheza kwa starehe".

Kwanini jamii ina wasiwasi kuhusu mchezo wa kamari?

Shutuma zinazoelekezwa kwa biashara hiyo zinazidi kuongezeka, huku kukiwa na lawama kwamba inaathiri maisha ya vijanakatika eneo zima la Afrika Mashariki.

"Hamu ya kutaka akupata pesa haraka kutoka kamari inawashinikiza vijana kujiingiza katika kamari kiasi kwamba baadhi wanatazama mchezo huo kama njia ya kujikimu kimaisha badala ya kutafuta ajira," watafiti wamesema.