Je, Samatta kucheza Klabu Bingwa Ulaya na Genk ama kutimkia England msimu ujao?

Samatta na tuzo Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Samatta amefunga zaidi ya magoli 30 msimu huu akaiwa na klabu ya Genk.

Mshambuliaji nyota wa mabingwa wa ligi ya Ubelgiji klabu ya Genk na nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania Mbwana Samatta huenda akatua Ligi Kuu ya England (Primia) msimu ujao.

Samatta, maarufu kama Samagoal, amedokeza kuwa kuna vilabu sita vya Ligi ya Primia ambavyo vinapigana vikumbo kumsajili.

"Kwa sasa sipo katika nafasi nzuri ya kuelezea ni klabu gani lakini pia kuna klabu nyingine mbili kutoka Hispania ambazo zimekuwa zikiisaka saini yangu. Hata hivyo, mimi ndoto zangu ni kucheza katika Ligi Kuu ya England," Samatta ameliambia gazeti la Mwananchi.

Hii si mara ya kwanza kwa Samatta kuhusishwa na uhamisho wa kwenda Ligi ya Primia, lakini inaonekana kuwa safari hii mambo yameiva.

"Ndiyo, nitaondoka mwishoni mwa msimu huu...(klabu ya England) moja inanifukuzia sana na imekuwa ikipiga simu kwa wakala wangu kila siku," amesema Samatta.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Samatta amechezea klabu ya Genk kwa misimu mitatu sasa.

Katika dirisha dogo la usajili la mwezi Januari mwaka huu, klabu ya Cardiff ilituma ofa ya Pauni milioni 13 kumng'oa Genk, lakini uhamisho huo ukakwama.

Klabu ya hata hivyo Cardiff imeshuka daraja.

Ukiachana na Cardiff, vyombo vya habari vya Uingereza mwaka jana viliripoti klabu nyengine tatu za nchini humo amabazo zilikuwa zikihusishwa na kutaka huduma ya ushambuliaji kutoka kwa Samatta.

Klabu hizo ni Everton, WestHam na Burnley.

Kipenzi cha mashabiki Genk

Samatta ameendelea kuwa kipenzi cha mashabiki wa Genk msimu huu baada ya kuongoza safu ya ushambulizi wa timu hiyo na kunyakuwa ubingwa wa ligi hiyo baada ya kuukosa kwa miaka nane.

Streka huyo mwenye miaka 26, ameifungia Genk magoli 23 na kumaliza kama mshambuliaji bora wa ligi. Pia ameifunga magoli 9 kwenye michuano ya ligi ya Europa.

Jina la Samatta limekuwa likiimbwa na mashabiki wa Genk, na wamekuwa wakimuomba mshambuliaji huyo kusalia klabuni hapo kucheza ligi ya Mabingwa Ulaya. Samatta ameiambia Mwananchi kuwa moyo wake upo England japo kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi ya Mabingwa ni kitu cha kutamanisha pia.

Haki miliki ya picha @SAMATTA77
Image caption Samatta alipohamia KRC Genk 2016

Hata akihamia England, bado atakuwa ameweka rekodi ya kuwa mtanzania wa kwanza kufanya hivyo. Pia amekuwa Mtanzzania wa kwanza kucheza Ligi ya Europa.

"Hawa jamaa (Genk) hawajacheza Ligi ya Mabingwa tangu mwaka 2011 enzi za akina (Kevin) De Bruyne, najua wanataka nicheze msimu ujao lakini Ligi Kuu ya England ina heshima yake...ni ligi ambayo tayari imepiga hatua kubwa sana kulinganisha na Ligi Kuu ya Ubelgiji. Ni ligi ambayo inapendwa na watu wengi duniani, Ligi inayoonekana sehemu kubwa duniani. Yaani kwa vitu vingi iko mbali."

Huwezi kusikiliza tena
Mbwana Samatta: Kauli ya 'Haina Kufeli' imenifaa maishani na katika kandanda

Samatta alijiunga na Genk akitokea TP Mazembe Januari 2016 ambapo alitia saini mkataba wa kumuweka katika klabu hiyo hadi msimu wa 2019/20.

Amesalia na miezi 12 kabla ya mkataba wake kumalizika.

Samatta alihamia Ubelgiji mwaka mmoja baada ya kutawazwa mchezaji bora wa mwaka Mwafrika aliyekuwa anacheza ligi za barani Afrika mwaka 2015.

Alishinda vikombe sita vikuu akiwa na TP Mazembe ikiwa ni pamoja na kushinda Ligi ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 2015 kabla ya kuondoka.

Samatta aliichezea Simba kabla ya kujiunga na TP Mazembe mnamo mwaka wa 2011.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii