Callixte Sankara: Msemaji wa waasi Rwanda akiri mashtaka ya ugaidi na kutishia usalama wa taifa

Meja Callixte Sankara
Image caption Meja Callixte Sankara aliyekuwa msemaji wa kundi la waasi dhidi ya Rwanda la National Liberation Front

Nsabimana Callixte maarufu Sankara aliyekuwa msemaji wa kundi la waasi dhidi ya Rwanda la National Liberation Front amefikishwa mbele ya mahakama mjini Kigali na kukiri mashtaka dhidi yake .

Sankara alifikishwa mbele ya mahakama mjini Kigali ambapo amekiri mashtaka 16 dhidi yake na kuomba radhi.

Sankara amefikishwa mahakamani asubuhi ya leo akiwa pamoja na wakili wake Moïse Nkundabarashi ambaye mara kwa mara ameonekana wakipiga soga na kutabasamu.

Ulinzi Mahakamani ulikuwa mkali, polisi waliojihami kwa silaha wameonekana wakizingira mahakama na katika kila kona ya chumba cha mahakama ya mtaa wa Kacyiru.

Mwendesha mashtaka amesoma mashitaka 16 dhidi ya mshtakiwa ambayo yana uhusiano na ugaidi, ujambazi wa kutumia silaha na ushirikiano na nchi ya kigeni kwa lengo la kuishambulia Rwanda.

Mashitaka hayo yana uhusiano na kauli zake alizotoa akiwa msemaji wa kundi la National Liberation Front, walipokiri kuhusika na mashambulizi katika vijiji vilivyo karibu na msitu wa Nyungwe kusini mwa Rwanda mwaka jana ambapo kulingana na mwendesha mashtaka, watu 3 waliuwawa na wengine wengi kujeruhiwa na kuchoma moto magari.

Kwa mjibu wa mwendesha mashtaka, nchi za Burundi na Uganda kuunga mkono harakati za kivita za kundi la National Liberation Front dhidi ya Rwanda akisema Burundi ilitoa njia na kuwapa ngome wapiganaji wa kundi hilo waliotumia msitu wa Kibira ambao unapakana na msitu wa Nyungwe waliopitia hadi kuishambulia Rwanda huku Uganda ikiwapa silaha na kusaidia wapiganaji waasi na kuwasaidia kwenda katika ngome zao zilizoko DRC.

Alipopewa nafasi Sankara ameiambia mahakama kwamba hana mengi ya kuzungumza isipokuwa kujutia yaliyotokea.

''kile ambacho sikutekeleza mwenyewe, kilitekelezwa na wapiganaji wa kundi nililokuwa msemaji wake'' ameeleza Sankara.

Amesema kwamba wapiganaji wake walimtelekeza na kufanya kinyume na malengo yake wakati wa shambulio dhidi ya vijiji vinavyopakana na msitu wa Nyungwe kwa kuuwa raia wa kawaida.

''kutokana na sababu hiyo,kwa moyo mkunjufu naomba radhi wananchi wa Rwanda waliopoteza watu wao katika mashambulio hayo na kuuwa raia kinyume na malengo niliyokuwa nayo.''

Ametangaza kujitenga na harakati zozote la kundi la National Liberation Front.

Je, huyu kiongozi wa kundi jipya la waasi Meja Callixte Sankara ni nani?

Ni machache yanayojulikana kuhusu Callixte Sankara:

  • Mtu aliyejitangaza kama naibu kamanda na msemaji wa kundi jipya la waasi la Rwanda Movement for Democratic Change.
  • Meja Callixte Sankara, kama avyojitambulisha kwa vyombo vya habari, ni Mtutsi ambaye alinusurika maauji ya kimbari ya 1994 nchini Rwanda.
  • Wazazi wake na jamaa wake wote waliuawa na wanamgambo wa Kihutu- Interahamwe.
  • Kwa sasa ana umri wa miaka 37.
  • Hakuwahi kuwa mwanajeshi wa RPF kwa kuwa RPF ilishika madaraka akiwa na umri wa kama miaka 10 tu.
  • Baada ya kuhitimu sheria katika chuo kikuu cha Rwanda- Butare, Callixte Sankara, alizozana na serikali ya Rwanda, akakimbilia Afrika ya kusini ambako alijiunga na NRC- Rwanda National Congress, ambayo ilibuniwa na Kayumba Nyamwasa, jenerali na mkuu wa zamani wa majeshi ya Rwanda.
  • Alikamatwa nchini Comoro mapema mwezi wa 4.

Alikamatwa vipi?

Kiongozi huyo wa waasi alikamatwa nchini Comoro na kupelekwa nchini Rwanda.

Mwezi uliopita Aprili alikamatwa katika operesheni iliyoelezewa na vyombo vya habari kuwa ilifanyika visiwani Comoro na kurejeshwa nchini Rwanda.

Kundi lake lilidai kuhusika na mashambulio dhidi ya vijiji vilivyo karibu na msitu wa Nyungwe kusini magharibi mwa Rwanda na kudai kuwa bado wapiganaji wake wana ngome katika msitu huo,madai yanayokanushwa na serikali ya Rwanda.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii