Stephen Masele: Naibu spika wa bunge la Afrika aomba radhi baada ya kuitwa katika kamati ya maadili

Stephen Masele ambae pia ni naibu spika spika wa Bunge la Africa Haki miliki ya picha PanAfricanParliament
Image caption Stephen Masele ,Naibu spika wa Bunge la Africa

Mbunge wa Shinyanga mjini nchini Tanzania, Stephen Masele ambae pia ni naibu spika spika wa Bunge la Africa hii leo amesimama bungeni na kuomba msamaha kwa kile kinachodaiwa kuwa ni utovu wa nidhamu na uchonganishi.

Hatua hii ya mbunge Masele inakuja baada ya kuitwa katika kamati ya maadili na spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai.

Ndugai alisimama na kulieleza Bunge kuwa taarifa hiyo imekuwa fupi kwa kuwa kuna mambo ya kulinda hadhi ya Bunge na masuala yanayohusu nchi, hivyo isingewezekana kuweka kila kitu.

Ndugai alimtaka Masele kusimama na ajieleze mbele ya kamati ya maadili pamoja na bunge.

"Naomba kukuomba radhi spika na familia yako kwa usumbufu wowote ulioupata kupitia sakata hili. Ninawaomba radhi wabunge wenzangu kwa usumbufu mlioupata.

Ninawaomba radhi viongozi wangu wakuu, mwenyekiti wa chama changu Rais John Magufuli, Waziri Mkuu kwa usumbufu wowote walioupata kutokana na jambo hili." Masele aliomba radhi.

Aidha Masele ambaye amewahi kuwa naibu Waziri wa Nishati na Masini amebainisha kuwa katika kuhudhuria vikao vya kamati ya maadili, huwa wanapeleka taarifa baada ya kupokea barua ya mwaliko wa kushiriki mikutano hiyo.

Haki miliki ya picha BUNGE
Image caption Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai

Amesema uamuzi wa Ndugai kumuandikia barua ya kusimamisha uwakilishi wake katika Bunge hilo ilitaka kutumika kama kigezo cha kumtoa kwenye wadhifa wake wa makamu wa rais .

"Nilitafakari sana maslahi ya wabunge, Taifa na kijana ninayekua. Nilifikilia haraka kama Spika ananisimamisha bila kunisikiliza ndio sababu ya kukata rufaa kuwasiliana na viongozi wa CCM na Waziri Mkuu."

Ninasikitika kwamba sikuchonganisha mihimili, nisingeweza kupeleka jambo hili kwa waziri," amesema mbunge huyo wa Shinyanga Mjini huku akionyesha barua hiyo.

Akizungumzia video iliyosambaa mitandaoni ikimuonyesha akizungumza katika Bunge hilo lililokuwa likiendelea Afrika Kusini na kumalizika Ijumaa Mei 17, 2019, Masele amesema rais huyo wa kamati ya nidhamu alitaka kumng'oa katika madaraka kwa kutumia barua aliyotumiwa na Ndugai.

Baada ya Masele kumaliza kuzungumza, Ndugai amesema, walimuita Masele nyumbani (Tanzania) kwa kuwa aliwaandikia viongozi wa juu kabisa ujumbe wa ajabu, "Akigonganisha mihimili na ndio sababu tulimtaka arudi lakini alikaidi."

"Tatizo lako ni uongo, kugonganisha viongozi, fitina na uchonganishi. Binafsi nimesononeka sana na naendelea kusononeka. Hata wewe huelewi," amesema Spika Ndugai.

"Ameniambia aombe radhi halafu anasema mengine. Hatujakuita kwa hayo ya PAP, tumekuita kwa haya ya nyumbani. Acha tabia hizo, acha, ujanja ujanja wa kuzungusha maneno."

Baada ya maelezo hayo, Ndugai aliliomba Bunge kumpuuza Masele hoja iliyoungwa mkono na wabunge waliosimama na kushangilia.

Haki miliki ya picha BUNGE

Masele amepata misukosuko hii akiwa katikati ya sakata jengine katika Bunge la Afrika ambapo anaiwakilisha Tanzania baada ya kuingia katika mgogoro kati yake na spika wa Bunge hilo ambae anakabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo ya rushwa ngono na upendeleo.

Tanzania inawakilishwa na wabunge wanne katika Bunge hilo la Afrika.

Hatua hii ya Masele inaondoa hali ya hewa chafu iliyokuwa imetanda kati yake na spika wa Bunge la Tanzania, baada ya kuvuka kigingi hiki, shauku ya watanzania ni kuona hatma ya mgogoro unaoendelea huko nchini Afrika kusini.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii