Simba 4-5 Sevilla: Licha ya kushindwa mabingwa hao wa Tanzania walionyesha mchezo wa kiwango cha juu

Huwezi kusikiliza tena
Mashabiki wa Simba SC

Mabingwa wa soka Tanzania, Simba almanusura iandike Historia kwa kuitandika Sevilla ya Hispania iliyosheheni nyota wake kibao.

Katika mchezo wa kirafiki uliovuta hisia za mashabiki wengi Afrika Mashariki, Simba imelala kwenye uwanja wa nyumbani jijini Dar es Salaam kwa kufungwa mabao 5-4 dhidi ya Sevilla.

John Bocco, nahodha wa Simba aliitanguliza timu yake kwa bao la mapema la dakika 8 kabla ya Mieddie Kagere kuongeza la pili dakika ya 15 kutokana na makosa ya beki wa Sevilla.

Sergio Escudero alifungua kalamu ya mabao kwa Sevilla kwa bao la dk ya 24 kabla ya Bocco tena kuipeleka Simba mapumziko ikiwa na ushindi wa mabao 3-1.

Kipindi cha pili Simba iliendelea kushambulia kwa kasi, ikiacha Sevilla ikimiliki mpira kabla ya kumsahau mkongwe Nolito kupunguza uongozi wa Simba kwa bao lake la dakika ya 49.

Kuingia kwa bao hilo kuliongeza hamasa ya wachezaji wa Sevilla walioongozwa na nyota wake Wissam ben Yeder, Ever Banega, Aleix Vidal, Jesus Navas na Sergio Escudero.

Licha ya Clatous Chama kuongeza bao la nne kwa Simba, mabao matatu ya lala salama ya Promes, Munir na Nolito yakazima ndoto za Simba za kusheherehesha ubingwa wao wa ligi kuu ya Tanzania, walioutwaa Jumanne wiki hii.

Pamoja na kufungwa mabao 5-4, Simba imedhihirisha mabadiliko makubwa kwa kuonyesha kiwango bora karibu muda wote wa mchezo.

Umiliki wa Mpira vs Mabao

Mpaka kipindi cha kwanza kinakamilika, Simba ilikuwa mbele kwa mabao 3-1. Sevilla ikimiliki mpira kwa asilimia 54 dhidi ya 46 ya Simba, lakini Simba ilionekana hatari zaidi golini kwa Sevilla, na ilitengeneza nafasi kama 6 katika kipindi hicho cha kwanza ikiwemo ya mwanzoni kabisa mwa mchezo, ambapo Mzambia Cloutus Chama, alipoteza akiwa umbali wa mita mbili tu golini.

Kwa namna ilivyocheza, Simba inastahili pongezi kubwa kwa kuweza kupata angalau magoli 4 langoni mwa Sevilla, ambayo ni miongoni mwa timu iliyoruhusu mabao machache kwenye ligi ya Hispania (La liga), ikiruhusu mabao 47 tu msimu huu, ikishika nafasi ya 9.

Barcelona yenye washambuliaji wakali duniani wakiongozwa na Lionel Messi na Luis Suarez, ukiacha ushindi wa 6-1 iliyoupata dhidi ya Sevilla mwezi Januari kwenye kombe la Mfalme (Copa del Rey).

Katika mechi sita zilizopita, imepata ushindi kwa tofauti ndogo ya bao moja ama mawili dhidi ya Sevilla.

Hii ni kuonyesha kwamba washambuliaji wa Simba, wamefanya kazi kubwa kupata mabao hayo manne kwenye mchezo huo, ambayo watayakumbuka katika maisha yao.

Kipindi cha kwanza kilikamilika Simba ikuwa mbele kwa mabao 3-1, huku ikicheza mpira wake wa siku zote wa pasi na kasi. P

amoja na Sevilla kurejesha bao moja, Simba ilikuwa mbele kwa mabao 4-2 mpaka dakika ya 84.

Kwa timu yenye uzoefu wa kucheza na wachezaji wakubwa wa Ulaya, kwa dakika sita zilizobaki, ingeweza kubadili aina yake ya uchezaji kwa kulinda zaidi uongozi wake.

Lakini Simba ilikosa umakini na uzoefu huo, huku Sevilla ikitumia Uzoefu wa nyota wake kama Ever Banega na mkongwe Manuel Nolito, aliyewahi kuichezea Manchester City ya England.

Image caption Baadhi ya mashabiki waliingiwa na hofu Sevilla ilivyoanza kuonesha uzoefu wake

Kasi ya mchezo wa Simba ilipungua kadri muda wa mchezo ulivyokwenda hasa dakika 30 za mwisho za mchezo huo uliohudhuriwa na wa melfu ya mashabiki wa Soka nchini Tanzania.

Pengine uchovu wa kucheza mechi nyingi za ligi kwa muda mfupi umeiangusha Simba kuweka historia.

Katika wiki tatu zilizpita Simba imecheza mechi 8 Sawa na wastani wa mechi moja kila baada ya siku mbili na Jumanne tu ya wiki hii imetoka kucheza na Singida Utd mkoani Singida ikasafiri Jumatano kurudi Dar es salaam, Alhamisi inacheza na Sevilla, mabingwa wa zamani wa Europa League.

Wakati huo Simba ikicheza michezo yote hiyo, Sevilla yenyewe kwa kipindi hicho imecheza mechi 3 pekee, dhidi ya Leganes, Atletico Madrid na Jumamosi hii dhidi ya Athletic Bilbao.

Kwa sababu ya Uchovu, Simba ililazimu kufanya mabadiliko ya kuwatoa nyota wake muhimu, akiwemo nyota wa mchezo huo aliyeonekana kucheza vyema John Bocco, hali iliyobadilisha hali ya mchezo huo, na kuwapa mwanya zaidi Sevilla na kupata mabao mawili katika dakika za lala salama.

Nyota wa mchezo

John Raphael Bocco, nahodha wa wekundu hao wa Msimbazi, ndiyo nyota wa mchezo huo, akifunga mabao mawili na kutengeneza bao moja.

Alikuwa na utulivu mkubwa langoni, akimiliki mpira vyema katika eneo lote la ushambuliaji akisaidiwa na Meddie Kagere na Mganda, Emanuel Okwi.

Bocco ambaye ni tegemeo pia la timu ya taifa ya Tanzania, na anatarajia kuwa miongoni mwa nyota watakaoingoza Tanzania kwenye Fainali za Afcon mwaka huu zinazofanyika huko Misri mwezi ujao, hakuwa na papara kwenye utoaji wa pasi na hata kulenga goli, akionekana mshambuliaji mkamilifu licha ya umri wake kuanza kumtupa mkono.

Kagere atalala na Viatu vyake mwaka mzima:

Meddie Kagere, ambaye anaongoza kwa ufungaji wa mabao kwenye ligi ya Tanzania inayokamilika mwishoni mwa wiki hii, akiwa na mabao 23, sasa ameweka historia ya kuzifunga timu mbili za Ulaya zilizokuja Afrika Mashariki hivi karibuni na kucheza katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Image caption Mshambuliaji wa Simba,Meddie Kagere akionesha umahiri wake uwanjani.

Ukiacha bao lake dhidi ya Sevilla, Kagere pia aliifunga Everton katika Uwanja huo huo wa Taifa Mwaka 2017, Everton Ikiwa na nyota wakubwa akiwemo Wayne Rooney aliyecheza kwa mafanikio timu ya Manchester United na timu ya taifa ya Uingereza.

Kwa mshambuliaji yeyote kufumania nyavu ni jambo zuri sana, lakini jambo zuri zaidi la kukumbukwa ni la kuzifumania nyavu za timu kubwa. Kagere kafanya hivyo na kwa vyovyote vile itabaki kwenye kumbukumbu yake. Atavikumbuka viatu alivyotumia na kuviheshimu kwa kumsaidia kufunga, ni rahisi kusema atalala navyo mwaka huu kuvipa thamani.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems: "Tuliongoza mara mbili kwa mabao mawili, lakini tulifanya makosa mwishoni tukafungwa. Kuhusu mabadiliko nililazimika kufanya kwa sababu ya timu na wachezaji, hii ni mechi kubwa wanahitaji kufurahia na kujenga kikosi cha baadae huku washabiki wakiburudika".

Kocha wa Sevilla, Joaquin Caparros: "Soka ni mchezo wa heshima, tunaiheshimu Simba, ni mabingwa wa ligi kuu, kwa sababu hiyo ndiyo maana mchezo huu umekuwa mgumu sana".

Mchezo huo ulikuwa wa kirafiki tu, kudumisha uhusiano wa Ligi ya Hispania Laliga na timu za ukanda wa Afrika Mashariki kupitia Kampuni ya kubashiri ya SportPesa. Pamoja na kukonga nyoyo za mashabiki, kwa wachezaji mchezo wa aina hii ni fursa kwao kujiunza.

Zaidi ya watu nusu bilioni waliushuhudia mchezo huo mkubwa kuwahi kuchezwa Afrika Mashariki katika miaka ya hivi karibuni, ukiacha ule wa Gor Mahia dhidi ya Everton wa mwkaa 2017. Baadhi ya Mawakala wa wachezaji Afrika na nje ya Afrika walikuwa kazini pia kuangalia vipaji vya wachezaji hasa wa Simba.

Mchezo wa aina hii hutoa fursa kwa nyota wengi kujitangaza, kwa mfano Meddie Kagera amesajiliwa Simba baada ya kuonyesha makalai kwenye mchezo aliouchezea Gormahia dhidi ya Everton mwaka juzi.

Wachezaji kama Clatous Chama, Kagere anayewindwa na Al Ahaly ya Misri, Haruna Niyonzima, Mohamed Hussein na Aishi Manula huenda wakabadilishwa upepo baada ya mechi hii.

Lakini pia, kwa kiwango walichokionyesha samba, wamejitangaza vyema kwenye uso wa wanasoka na wawekezaji. Huenda pia ikavutia nyota wengi hasa wa Afrika kutaka kusajiliwa na Simba, ambayo mwaka huu imeingia robo fainali ya Klabu bingwa Afrika.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii