Mambo unayostahili kuyajua Tanzania ikielekea kupiga marufuku mifuko ya plastiki

Mfuko Haki miliki ya picha Getty Images

Kuanzia Juni 1, 2019 itakuwa ni kosa la jinai kutengeneza, kuagiza, kusambaza na kutumia mifuko ya plastiki nchini Tanzania, na wote watakao kaidi marufuku hiyo watakutana na mkono wa sheria.

Marufuku hiyo inahusisha maeneo yote ya Tanzania Bara, upande wa pili wa muungano Visiwa vya Zanzibar vinatekeleza marufuku hiyo kwa miaka kadhaa sasa.

Tanzania Bara pia imekuwa katika harakati za kupiga marufuku mifuko ya plastiki kwa zaidi ya mwongo mmoja huku harakati hizo zikikwama mara kadhaa.

Safari hii serikali ya nchi hiyo imeonekana kujidhatiti kutekeleza marufuku hiyo kama wafanyavyo nchi jirani za Rwanda na Kenya.

Marufuku hiyo haitahusisha vifungashio vya plastiki vya bidhaa mbalimbali.

Mifuko ya plastiki inalaumiwa pakubwa kwa uchafuzi wa mazingira duniani, na harakati za kukomesha matumizi yake yanalenga kulinda mazingira.

Makosa na adhabu

Kwa kupitia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (Environmental Management Act) serikali ya Tanzania imetunga kanuni za mwaka 2019 za kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki.

Kifungu cha nane cha kanuni hizo kinaorodhesha makosa matano ambayo ni; kuzalisha na kuagiza mifuko ya plastiki, kusafirisha nje ya nchi mifuko ya plastiki, kuhifadhi na kusambaza mifuko ya plastiki, kuuza mifuko ya plastiki na mwisho kumiliki na kutumia mifuko ya plastiki.

Kila kosa lina adhabu yake kwa mujibu wa kanuni hizo kulingana na uzito wa kosa lenyewe.

Haki miliki ya picha Getty Images

Kwa kosa la kwanza la uzalishaji na uagizaji adhabu yake ni mosi,faini isiyopungua TSh milioni 5 na isiyozidi TSh milioni 20, pili kifungo kisichozidi miaka miwili jela, adhabu ya tatu ni mjumuiko wa adhabu zote mbili za awali faini na kifungo.

Adhabu za kosa la pili amabalo ni kusafirisha mifuko nje ya Tanzania ni sawa na za kosa la kwanza.

Kwa kosa la tatu la kuhifadhi na kusambaza mifuko adhabu zake ni mosi faini isiyopungua TSh milioni 5 na isiyozidi TSh miioni 52, pili kifungo kisichozidi miaka miwili, tatu faini na kifungo kwa pamoja.

Ukipatikana na hatia ya kuuza mifuko ya plastiki adhabu ambazo utakumbana nazo ni mosi, faini isiyopungua TSh laki moja na isiyozidi laki tano, pili, kifungo kisichozidi miezi mitatu jela na tatu yawezekana ukahukumiwa adhabu zote mbili za awali kifungo na faini.

Ukiendelea kutumia na kumiliki mifuko ya plastiki kuanzia Juni 1 nchini Tanzania, basi jiandae kulipa faini isiyopungua TSh30,000 na isiyozidi laki mbili, kifungo kisichozidi siku saba ama faini na kifungo.

Vipi kuhusu shehena zilizopo?

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mifuko ya plastiki imelaumiwa kwa kuchangia uchafuzi wa mazingira.

Katika kuhakikisha kuwa hakuna anayeonewa ama kuathirika kibiashara na katazo hilo, marufuku ilitangazwa Aprili 10 ili kuwapa watu na wafanyabiashara muda wa kujiandaa.

Hivi karibuni, Waziri wa Maazingira wa Tanzania Januari Makamba ametoa mwongozo wa kile kinachotakiwa kufanyika kwa wafanyabiashara ambao watakuwa wangali na shehena kubwa ya mifuko hiyo pale tarehe ya marufuku itakapowadia.

Gazeti la Mwananchi limemnukuu waziri huyo akisema mifuko hiyo yaweza kusafirishwa nje ya nchi kwa kibali maalumu ama kubaki nayo hapo hapo ili ibadilishiwe matumizi.

"Baadaye utafanyika utaratibu wa kurejerezwa (recycle) na kutengenezwa bidhaa nyingine kama sahani, viti na kadhalika," alisema na kuongeza, "Kwa mfano Sudan hawajakataza mifuko, tutawasaidia wale waliopata soko wasipate hasara lakini kwa kibali maalum na itasindikizwa hadi mpakani kwa gharama za msafirishaji."

Mwongozo wa Ukaguzi wa Mifuko

Tayari serikali ya Tanzania imekwisha toa tangazo la katazo ya mifuko kwa wageni wanaotarajia kuingia nchi hiyo kuanzia Juni 1.

"Wageni wanaoingia (Tanzania) wanashauriwa kutobeba vifungashio vya plastikivya aina yoyote ile. Katika maeneo ya mipaka ya kuingilia nchini kutakuwa na dawati maalumu kwa ajili ya kutupa mifuko hiyo," ilisema taarifa ya serikali.

Serikali ya Tanzania inasema lengo lao si kuwafanya wasafiri kutofurahia safari yao, bali kushiriki katika kutunza mazingira.

Namna ukaguzi utakavyofanyika Tanzania kwa mujibu wa serikali ya Tanzania:

  • Ukaguzi utafanyika tu madukani, magengeni, masokoni, kwenye 'supermarkets', maghalani, mipakani, viwandani na maeneo mengine ziuzwapo bidhaa.
  • Wakati wote wakaguzi wajitambulishe na kuonesha vitambulisho vyaokwa wahusika kwenye maeneo wanayoyakagua.
  • Hairuhusiwi kumsimamisha mtu na kumpekua au kupekua mizigo yake ili kutafuta mifuko ya plastiki.
  • Hairuhusiwi kuingia kwenye makazi ya watu ili kutafuta mifuko ya plastiki.
  • Iwapo chombo cha usafiri kitasimamishwa na kukaguliwa kwa sababu nyengine na kukutwa na shehena ya mifuko, adhabu itatolewa kwa mujibu wa sheria.
  • Atakayekutwa na mifuko ataelekezwa pa kuipeleka mifuko, kisha atapigwa faini, atasainishwa fomu na kupewa muda wa kuilipa. Atakapokataa kusaini fomu au kulipa faini, atafunguliwa mashtaka.
  • Watakaotozwa na kulipa faini, watapatiwa risiti za serikali.
  • Hairuhusiwi matumizi ya nguvu katika utekelezaji wa katazo ikiwemo kuwapiga au kuwabeba na kuwaweka ndani watu.
  • Watakaokaidi kutoa ushirikiano, ama kufanya hujuma dhidi ya utekelzwaji wa sheria kuchukuliwa hatua kali zaidi.

Mifuko mbadala

Waziri Makamba amebainisha kuwa kuna viwanda 70 ambavyo vimejitokeza kutengeneza mifuko mbadala, ambapo kati ya hivyo sita ni vikubwa na 30 vya kati.

Umoja wa watengenezaji wa mifuko hiyo nchini Tanzania umebainisha kuwa bidhaa zao zitakuwa zimeshaingia mtaani ifikapo Juni 1.

Umoja huo unadai kwa sasa bidhaa zao hazionekani sana kwa sababu bado mifuko ya plastiki imo katika mzunguko mtaani.

Mada zinazohusiana