Mahakama kuu Kenya imekataa kufutilia mbali kifungu 162 cha sheria inayoharamisha mapenzi ya jinsia moja

wapenzi wa jinsia moja kenya Haki miliki ya picha SIMON MAINA

Mahakama kuu nchini Kenya imeamua sheria inayopinga mapenzi ya jinsia moja itaendelea kutumika nchini kinyume na ilivyotarajiwa na wanaharakati waliotaka ifutiliwe mbali.

Katika uamuzi huo, majaji wameamua kwamba sheria inayopingwa, maarufu kanuni 162 hailengi makundi yoyote maalum ya watu na badala yake inaeleza kwamba ni makosa kwa yoyote kushiriki katika uhusiano wa aina hiyo.

Mahakama imeeleza kwamba inatambua umuhimu wa haki za binaadamu hatahivyo, imeeleza kwamba sheria imeweka mpaka au ukomo kwa baadhi ya haki hizo.

Uamuzi huo uliosubiriwa kwa muda mrefu umetazamwa kwa umuhimu mkubwa kwa jamii ya wapenzi wa jinsia moja (LGBT) nchini.

Wanaharakati wamekuwa wakilalamika kwamba sheria hiyo, inakiuka katiba ya mwaka 2010 nchini inayohakikisha usawa, heshima na faragha kwa raia wote.

Kwa mujibu wa sheria nchini Kenya, mtu anayepatikana kujihusisha katika mahusiano ya jinsia moja anaweza kuhukumiwa miaka 14 gerezani.

Katika utangulizi wake Hakimu Roselyn Aburili ameeleza kwamba ni muhimu na ni jukumu la mahakama kuheshimu maadili ya kitaifa na kwamba vifungu vya sheria ni muhimu viambatane na katiba nchini.

Mahakama imeeleza kwamba kwa kutazama mifano ya kesi za aina hiyo katika mataifa ya nje, ikiwemo India ambayo mwaka jana iliruhusu mapenzi ya jinsia moja, wametathmini mifano hiyo kwa misingi ya kuangalia namna zilivyoshughulikiwa.

Hatahivyo mahakama imesema ni muhimu kuelewa kwamba kesi hizo hazitoi ufafanuzi wa wazi wa namna ya kutathmini katiba ya nchi, na hivyo ni muhimu kuwa na muongozo binafsi wa taifa katika kushughulikia kesi za aina hiyo.

Uamuzi huo umeeleza kwamba hakuna ushahidi wa kuthibitisha kwamba wawasilishaji kesi wamenyanyaswa na haki zao kukiukwa.

Mawakili wa pande zote walikuwepo katika kikao cha leo mahakamani kilicho anza kuchelewa kinyume na ilivyoatarjiwa awali, na uamuzi ulisomwa na majaji watatu wa mahakama hiyo kuu, Hakimu Roselyn Aburili, Hakimu John Mativo na Hakimu Chacha Mwita.

Image caption Msongamano mkubwa wa watu ulishuhudiwa nje ya mahakama kabla ya kuanza kusikilizwa kwa hukumu ya kesi hiyo

Nchini Kenya, kama ilivyo katika mataifa mengi barani Afrika, uhusiano wa jinsia moja haukubaliki kwa jamii.

Uamuzi wa leo uliahirishwa mwezi Februari mwaka huu, mahakama ikieleza kwamba inahitaji muda wa ziada kutokana na uwingi wa nyaraka zilizowasilishwa katika kesi hiyo.

Wanaharakati wanasema kwamba kuwepo kwa sheria hii kumezidisha ubaguzi, huku watu wakifurushwa kutoka nyumba walizokodisha, kunyimwa nafasi za kupata matibabu na pia kuhangaishwa na polisi, yote kwa sababu ya jinsia zao.

Aidha wanaharakati wanasema kutolewa sheria hii kumechangia dhuluma za aina nyingi.

Kenya mfano kwa mataifa ya Afrika

Wadadisi wanatathmini kwamba uamuzi wa leo ni muhimu kwa mataifa mengine Afrika yalio na sheria kama ya Kenya zilizoundwa katika utawala wa kikoloni na huenda zikatoa muelekeo sasa kwa kesi za aina hii Afrika.

Kenya ni nchi ya kwanza ya Afrika chini ya sheria kusikiliza mahakamani ombi la kutaka kufutiliwa mbali kifungu cha sheria inayopinga mapenzi ya jinsia moja.

Nchi ya kwanza ilikuwa India mnamo 2018 na ilifutilia mbali sheria iliyokuwa inasema ni kosa la jinai kushiriki mapenzi ya jinsia moja nchini humo.

Mahakama ya upeo India ilifanya maamuzi ya kihistoria, yaliotengua maamuzi yaliyofanywa mwaka 2013 ambayo yalidumisha matumizi ya sheria ya kikoloni, maarufu kama kanuni ya 377 ambayo ilitia hatiani vitendo vya ushoga.

Kadhalika mahakama iliamua kuwa kuwabagua watu kutokana na mahusiano yao ya kimapenzi ni ukiukaji wa haki za binaadamu.

Angola pia ilibadili sheria kama hiyo kupitia maamuzi ya bunge Januari mwaka huu 2019.

Wanaharakati wanasema licha ya uamuzi wa leo, huenda historia ikabadilika kutokana na kupatikana fursa ya kuchagua haki, usawa na ubinaadamu.

Chini ya sheria za Kenya zilizoandikwa enzi za ukoloni, mapenzi ya jinsia moja yametambuliwa kama kitendo kisicho cha kawaida, na kuwekwa katika kitengo kimoja na hatia ya kufanya mapenzi na wanyama.

Wanaharakati na watu wanaojitambulisha kama wapenzi wa jinsia moja sio tu kutoka Kenya, lakini pia nchi jirani kama Uganda walifika mahakamani leo kwa idadi kubwa kufuatilia uamuzi huu.

Image caption Ugandan refugees also in court. They fled to Kenya because of their orientation.

Brian na Yvonne ni wanaharakati wa kutetea haki za jamii ya watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, pamoja na wale waliojibadilisha jinsia na hisia nchini Kenya.

''Tunadharuliwa, tunakabiliwa na ghasia, tunaumia, tunateswa, tunakosewa. Tukienda kutafuta huduma za afya tunaangaliwa kwa dharau, tunatukanwa, tunatemewa mate, tunafanywa kama sisi sio Wakenya, na kama sisi sio Binaadamu, ni kama sisi ni viumbe wasiotoka katika dunia hii', wameieleza BBC.

Msongamano mkubwa wa watu ulishuhudiwa nje ya mahakama kabla ya kuanza kusikilizwa kwa hukumu ya kesi hiyo leo:

Katiba ya Kenya inasema nini?

Katiba ya Kenya inaonya dhidi ya ubaguzi wa aina yoyote, ikiwemo ubaguzi wa kijinsia.

Wasemaji wa jamii hii wanahoji kuwa hata kama kuondoshwa kwa sheria hii haingesitisha kabisa ubaguzi, angalau walikuwa na matumaini ya kuwa itawanyang'anya polisi nguvu za kuwakamata kiholela.

Lakini wanaounga mkono sheria hii, wakiwemo baadhi ya makundi ya dini, wanasema kuwa kuondolewa kwa sharia hii huenda ikatoa fursa ya kuhalalisha ndoa kwa watu wa jinsia moja.

Mnamo 2016, shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu limegundua kwamba wapenzi wengi wa jinsia moja wanaoishi nchini Kenya wanakabiliwa na 'wasiwasi wa usalama kila siku'.

Kumekuwepo na shinikizo kutoka mataifa mengi duniani kwa taifa la Kenya kuhalalisha mapenzi ya jinsia moja.

Lakini wakenya wengi, akiwemo rais Uhuru Kenyatta , wanahoji kuwa taifa hili lina shida kubwa zaidi za kushughulikiwa, na zinazopaswa kupewa kipa umbele.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii