Jinsi wanawake wa Kiislam wanavyomudu majukumu yao mwezi wa Ramadhan

Mwanamke muislam kazini Haki miliki ya picha Getty Images

Wanawake wanaofanya kazi wanakabiliwa na mambo mengi akilini wakati wanapojaribu kutekeleza majukumu mengine ambayo yana umuhimu kwao.

Wanalazimika kuvaa kofia nyingi ikiwa ni pamoja na ya muajiriwa au muajiri kama kazi ni yake, kuwa mama, kuwa mke, na ua hata kujiendeleza kimasomo.

Kwa wanawake wakiislamu wakati huu wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, wanajipata wakitekeleza majukumu hayo na hata zaidi kwasababu wao pia wamefunga kula na kunywa lakini wanatakiwa kuhudumia familia zao.

Lakini wanawezaje kusawazisha majukumu hayo kazini na nyumbani na pia kutimiza nguzo hii muhimu ya kidini?

BBC imezungumza na wawili kati yao kufahamu wanavyoweza kumudu majukumu yao ya kila siku msimu huu wa mfungo wa mwezi wa Ramadhan.

Fadya Ali Umen- Mmiliki wa mgahawa

Haki miliki ya picha Fadya Ali
Image caption Fadya Ali

Bi Fadya amekuwa akiendesha biashara yake kwa takriban miaka 10 sasa na anasema kuwa kila mwaka amejifunza mawili matatu kuhusu namna ya kusawazisha majukumu yake kama mwanamke wa Kiislam.

''Nashkuru tangu nilipoanza biashara hii kila ramadhan imekuwa tofauti na nyingine nimejifunza mengi.'' anasema Fadya

Lakini anaongeza kuwa mwaka wa kwanza wa pili na watatu haikuwa rahisi kwake hasa wakati wa ramadhan kwasababu ndio mwanzo alikua ameanza biashara yake.

Wakati huu wa mfungo siku yake inaanza saa tisa unusu ambapo familia yake inajumuika pamoja kwa chakula cha kabla kufunga kwa siku hiyo.

Baada ya hapo wanajadiliana masuala ya kifamilia wakisubiri ibada ya alfajiri punde wakimaliza muda huwa umesongo wengine wanaenda kulala lakini yeye anawasaidia watoto kujiandaa kwenda shule.

Anasema watoto wakienda shule na yeye pia anapata muda kidogo wa kujipumzisha kwasababu shughuli ya biashara ya mgahawa wakati huu wa mfungo wa ramadhan inaanza kazi saa tano asubuhi.

''Huwa hatufungui mapema kwa hiyo tunachukua saa hizo za asubuhi kufanya usafi, kupika,kupanga na mambo mengine yote ikifika saa kumi jioni tunaanza kuuza vyakula kwa wateja ambao wanatoka kazini na hawana muda wa kupika'' Bi Fadya aliiambia BBC.

Haki miliki ya picha Fadya Ali

Anasema saa kumi na mbili na nusu anaanza kuandad chakula cha wateja ambao wameamua kufungua hapo mgahawani na shughuli hiyo huendelea kwa muda kwa sababu anawahudumia wateja tofauti.

''Tunamaliza kazi kati ya saa nne hadi saa nne unusu baada ya hapo ukifika nyumbani ni kama saa tano ndio anze tena kutafutana na watototo wale watakuwa wamelala tunapatana alfajiri''

Miaka 10 iliyopita watoto walikuwa wadogo lakini sasa wamekuwa wakubwa, biashara ilikuwa ndogo sasa imekuwa kubwa.'' anasema Fadya.

Anaongeza kuwa familia yake imekuwa na biashara yake na kwamba watoto wamekuwa katika mazigira moja na yeye.

Tofauti na wanawake wengine wanaofanya mbali na nyumbani na ambao mazingira ya kazi haiwaruhusu kuwa karibu na watoto wao saa za kazi anasema anashukuru kazi yake haijamkosesha uhuru huo.

''Biashara yangu haijanizuia kabisa kupata furasa ya kuwalea watoto wangu,wote sita walijua kutamka neno la kwanza hapa kazini kwangu... yaani hapa ni shule ya ''chekechea'' alisema huku akimshukuru Mungu kwa hatua aliyopiga.

Haki miliki ya picha Fadya Ali

Fadya anaongeza kuwa kwa wanawake wanatakiwa kujitole zaidi kuhakikisha familia yake iko imara na ili kufukia lengo hilo anasema mume wake amemsaidia sana.

Wakati watoto walipokuwa wadogu changamoto ilikuwa tofauti na ili kutatua changamoto hiyo tuliamua kutenga sehemu hapa kazini ili tuweze kuwa karibu nao.

''Sasa wamekuwa wakubwa tunajaribu sana kufanya kazi pamoja ili tuweza kudumisha umoja wetu, wale wakubwa wakitoka shuleni hususan siku ya Ijumaa wao huja hapa kazi kunisaidia''

Mpango huo anasema umemsaidia sana kujenga uhusiano wa karibu na mumewake na watoto wake.

Ushauri wake kwa kinanana wanaofanya biashara kama yake anasema ni kujitolea na kumweka Mungu mbele.

''Mungu hawezi kukupatia kazi ambayo huwezi kuimudu'' alisema.

Kamila Hassan Shora -Afisa wa polisi

Bi Kamila amefanya kazi ya polisi kwa miaka 15 sasa na ni mke na mama wa watoto wawili.

Kwake anasema Ramadhan ni wakati wa kujiweka karibu na mwenyezi Mungu zaidi na kwamba kazi yake haijamzuia kutekeleza ibada hiyo muhimu.

Haki miliki ya picha Kamila Hassan

''Nashkuru Ramadhan nafunga na kazini pia natekeleza wajibu wangu ipasavyo wa kwasababu wananchi lazima wahakikishiwe usalama wao.'' alisema Bi Kamila.

Aliongeza kuwa japo wakati mwingine anafanya kazi katika mazingara magumu anajitahidi kuhakikisha anapata wasaa wa kujumuika na familia yake.

''Watoto walipokuwa wadogo tulishauriana na mume wangu tukaonelea ni vyema wakati mwingine tutafute msaada wa jamaa zetu hasa wakati nilipopewa uhamisho wa kazi mbali na nyumbani''

Japo anafaya kazi ya askari polisi akivua sare za kazi anavalia kofia ya mama na mke nyumbani.

Haki miliki ya picha SEYLLOU

Anasema wakati huu wa Ramadhan anajipata akiamka wa kwanza mbele ya kila mtu na kulala wa mwisho baada ya kila mtu amelala.

''Lakini sio kwamba nalalamika manake ni majukumu yangu nayatekeleza kwa hiari''

Uwezo wa kumuachia kazi zote kijakazi wake anao lakini anasema kazi yake imemwezesha kujiamini zaidi.

Kamila anamshukuru Mungu miaka imesonga watoto wamekuwa na anajivunia mika 15 akifanya kazi ya usalama na familia yake ni imara.

Anaongezea kuwa imani imekuwa nguzo ya familia yake.

Kwa wanawake wanaofanya kazi kama yake anasema siri ni kumweka Mungu mbele na kila jambo hata liwe gumu namna gani atamsaidia.

Kingine anawaomba waheshimu kazi zao kwasababu ndipo mahali wanapochumia riziki yao ya kila siku.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii