Hali ya wasiwasi yatanda kati ya Rwanda na Uganda baada ya watu wawili kuuawa mpakani

Hali ya wasiwasi imetanda kati ya mataifa hao mawili
Image caption Rais wa Rwanda kushoto paul kagame na mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni. Hali ya wasiwasi imetanda kati ya mataifa hao mawili

Rwanda imekana madai kwamba wanajeshi wake waliingia katika ardhi ya Uganda siku ya Ijumaa usiku na kuwaua watu wawili.

Hali ya waiswasi imetanda kati ya majirani hao wawili, hatua ilioifanya Rwanda kuzuia usafiri katika mpaka wa mataifa hayo mawili .

Kulingana na mwandishi wa BBC Catherine Byaruhanga, Serikali ya Kigali inasema kuwa watu wawili, mmoja raia wa Rwanda na mwengine wa Uganda , walipigwa risasi nchini Rwanda lakini baadaye wakafariki nchini Uganda.

Inasema walishukiwa kuwa miongoni mwa genge la watu wanaohusika na kuingiza vitu kinyume cha sheria ambalo liliwashambulia maafisa wa usalama wakati walipojaribu kuwakamata.

Inasema kuwa watu hao waliojeruhiwa baadaye walibebwa na kuvukishwa mpakani.

Lakini Uganda inasisitiza kuwa wanajeshi hao wa Rwanda waliingia katika himaya yake wakimtafuta raia huyo wa Rwanda na kumuua pamoja na raia huyo wa Uganda aliyejaribu kuingilia kati.

Kampala amewataka wahusika kuchukuliwa hatua lakini imeongezea kwamba haitafutalia swala hilo iwapo Kigali haitachukua hatua yoyote.

Mnamo mwezi februari, Rwanda ilizuia bidhaa za Uganda kutoingia katika taifa hilo na kuwazuia raia wake kutovuka mpaka huo.

jamii zinazoishi katika eneo hilo zinazoathirika zinasema upitishaji wa bidhaa kinyume na sheria umneongezeka kati ya mataifa hayo mawili na kwamba wanajeshi wa Rwanda huwashambulia raia wa Rwanda wanaojaribu kuingia Uganda.

Hali ya wasiwasi kati ya majirani hao huku kila mmojawapo akiamini kwamba mwenzake anajaribu kuliyumbisha taifa lake.

Kagame afunguka kuhusu mgogoro kati ya taifa lake na Uganda

Katika siku za nyuma Rais wa Rwanda Paul Kagame alielezea kuwa chimbuko la mgogoro baina ya nchi yake na nchi ya Uganda ni la tangu miaka 20 iliyopita nchi ya Uganda ikitaka kuangusha utawala wake.

Akihutubia mkutano wa kitaifa Rais Kagame amesema mgogoro huo ulishika kasi mnamo miaka ya hivi karibuni kutokana na serikali ya Uganda kuunga mkono kundi la RNC linalopinga Rwanda na ambalo linatumiwa na Uganda kuwanyanyasa raia wa Rwanda wanaotembelea au wanaoishi nchini Uganda.

Akihutubia mkutano wa kitaifa unaomkutanisha na viongozi wengine kuanzia ngazi ya mashinani,rais Paul Kagame amezungumzia kwa kirefu mgogoro baina ya Rwanda na nchi ya Uganda na kusema mgogoro huo ni wa tangu miaka 20 iliyopita.

Akifafanua mgogoro huo Rais Kagame amerejelea kitabu kinachoitwa 'From Genocied to continental War'' ambacho kiliandikwa na Gerard Prunier mwanishi wa vitabu kutoka Mfaransa.

Rais Kagame amesema kwamba mwandishi huyo aliandika kwamba alikutana na waziri wa zamani wa mambo ya ndani marehemu Seth Sendashonga mwaka 1998 pmaoja na maafisa wakuu wa jeshi la Uganda na kuzungumzia mipango ya kumsaidia Sendashonga ili kuangusha utawala wa Kagame.Mwandishi huyo katika kitabu chake kulingana na maelezo ya rais Kagame, Uganda ilikuwa imemuahidi kumsaidia kijeshi.

''Sababu ya mimi kurejelea kuzungumza haya nimetaka kuwaonyesha mfululizo wa jinsi mambo yalivyokwenda mnamo miaka 20 iliyopita.Tulijaribu kufanya mikutano ya hapa na pale ili kutafuta suluhu.lakini matatizo hayo hayaishi.Ukweli ni kwamba Seth Sendashonga alifariki dunia kwa kuwa alivuka mstari mwekundu.Sifurahii kusema hivyo lakini pia sijutii kifo chake''

Seth Sendashonga aliuawa katika mazingira ya kutatanisha mwaka 1998 mjini Nairobi alipokuwa uhamishoni baada ya kutofautiana na utawala wa Rwanda.

Rais Kagame amesema mgogoro huo ulishika kasi hivi karibuni kufwatia wananchi wa Rwanda wanaoingia nchini Uganda au kufanyia kazi nchini humo kushikwa na kuzuiliwa sehemu ambazo hazijulikani na kufanyiwa vitendo vya mateso huku akishtumu utawala wa Uganda kutoa nafasi ya ushirikiano kwa kundi la Rwanda National Congress linaloongozwa na mkuu wa zamani wa majeshi ya Rwanda jenerali Kayumba Nyamwasa:

''RNC wanafanya kazi kwa ushirikiano na vyombo vya usalama vya Uganda.kilicho wazi ni kwamba Wanachokifanya ni kunyanyasa wanyarwanda ambao hawataki kuungana nao huku wakiwasingizia a kwamba wametumwa na utawala wa Kigali kuhujumu usalama wa Uganda na kuuwa wanyarwanda wa upinzani.Ni madai yasiyo na msingi.

lakini haya yote yanaonyesha ushirikiano wa dhati uliyopo baina ya serikali ya Uganda na kundi la RNC.''

Je Uganda inasemaje?

Haki miliki ya picha Reuters

Uganda imekuwa ikiishutumu Rwanda kuwatuma majasusi na kufanyia vitendo vya ujasusi kwenye ardhi yake,shutuma ambazo Rwanda inakanusha.

Rais Kagame amesisitiza kwamba mara kadhaa mwenyewe aliwasilisha malalamiko hayo kwa mwenzake Yoweri Museveni na kwamba hakuonyesha utashi wowote wa kuyatatua.

Wiki iliyopita serikali ya Rwanda ilikataza wananchi wake kwenda nchini Uganda na kusababisha mkwamo wa biashara.Rwanda inasema inatoa kipaumbele kwa maiasha ya raia wake zaidi kuliko biashara baina ya nchi mbili.

Mada zinazohusiana