Askwar Hilonga: Mhandisi wa Tanzania atuzwa na shirika la afya duniani kwa uvumbuzi wake

Askwar Hilonga wa tanzania kushoto ametuzwa na WHO kwa uvumbuzi wake Haki miliki ya picha ROYAL ACADEMY OF ENGINEERING

Mhandisi mmoja nchini Tanzania Dkt. Askwar Hilonga ametambuliwa na shirika la afya duniani WHO kwa uvumbuzi wake wa kifaa cha kuchuja maji chenye gharama ya chini ambacho kinalenga kubadilisha maisha ya wakaazi wasio na maji safi ya kunywa.

Dkt. Hilonga ambaye ni mhadhiri wa chuo kikuu cha Nelson Mandela cha Sayansi na Teknolojia alitunukiwa tuzo hiyo wakati wa mkutano wa Shirika la Afya Duniani WHO mjini Geneva Switzerland.

Alikuwa akihudhuria mkutano wa bodi ya Afya Duniani, inayotoa maamuzi ya WHO.

Bodi hiyo huwakilishwa na wajumbe kutoka mataifa wananchama wa WHO na huangazia ajenda maalum zilizoandaliwa na bodi kuu.

Haki miliki ya picha ROYAL ACADEMY OF ENGINEERING

Akisukumwa na ari ya kukabiliana na magonjwa yanayoambukizwa kupitia maji , Hilonga alisomea shahada ya uzamivu ya Nanotechnologia ambayo inashirikisha utumizi wa atoms na molecules kwa utengenezaji wa bidhaa.

Dkt. Hilonga alivumbua kichujo hicho cha maji cha gharama ya chini kinachotokana na teknolojia hiyo ya nano, na tangu wakati huo amepata tuzo katika mashindano tofauti ya kisayansi ambayo yametuza umaarufu wake mbali na kumkabidhi fedha kufadhili kampuni yake ya Gongali Model Company.

Chujio hicho cha cha maji kinachotumia mchanga kusafisha maji ya kunywa kwa kutumia mfumo wa nanoteknolojia tayari kina nembo yake.

"Ninaweka maji kupitia mchanga ili kuzuia uchafu na bakteria," Mr Hilonga aliiambia kipindi cha BBC cha Newsday kuhusu chujio hilo.

"Lakini mchanga hauwezi kuondoa uchafu kama vile fluoride na madini mengine mazito hivyo nitapitisha kupitia vifaa vya nano ili kuondoa kemikali."

Anasema kwamba awali chujio moja lilikuwa likigharimu $130 , lakini akasema kuwa atanunua vifaa na kupunguza bei baada ya kushinda £25,000, .

"Kwa watu ambao hawawezi kununua chujio la maji, tumeanzisha vituo vya maji ambapo watu watakuja kununua kwa bei nafuu'', aliongezea.

Katika kanda yake ya video katika mtandao wa Yu tube bwana Hilonga anelezea kwamba chujio hilo linaweza kuondoa uchafu kwa hadi asilimia 97, lakini lengo lake kuu lilikuwa kutengeza chujio ambalo linaweza kuzuia asilimia 99.9 ya bakteria pamoja na virusi.

Familia yake ilikuwa ikikumbwa na magonjwa yanayoasababishwa na maji nchini Tanzania, hivyobasi alipofuzu shahada yake ya uzamivu katika nanoteknolojia nchini Korea Kusini alianza kukusanya vifaa vya nano ambavyo vitasaidia kusafisha maji.

Taasisi ya wahandisi ya Royal Academy inalenga kuwasaidia wahandisi waliopo katika jangwa la Sahara kutafuta suluhu za changamoto zinazokokumba Afrika kuwa biashara.

Hilonga na wahandisi wengine watatu , walipokea £10,000 kila moja ili kuanzisha mradi wa kibiashara.