Watu 45 wafa maji DRC, mwezi uliopita walifariki 167

Ajali Mai-Ndombe Haki miliki ya picha Blaise Mabala
Image caption Watu wakiangalia shughuli za uokozi zikiendelea

Idadi ya vifo vya ajali ya boti nchini nchini Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) imepanda na kufikia 45 katika eneo la Inongo magharibi mwa nchi hiyo.

Ajali hiyo ambayo ni mwendelezo wa majanga ya majini nchini DRC imetokea usiku wa Jumamosi kwenye ziwa Mai-Ndombe, na bado watu 200 kati ya wale walioabiri boti hiyo hawajapatikana mpaka sasa.

Meya wa Inongo Simon Wemba ameiambia BBC kuwa watoto 11 ni miongoni wa waliofariki.

Boti hiyo pia inaaminika kuwa ilipakiza takribani watu 400 na wengi wao walikuwa walimu wakielekea kupokea mishahara yao.

Walimu 27 tayari wamethibitika kupoteza maisha kwenye ajali hiyo.

Tayari mamlaka zimepiga marufuku boti zenye umri wa zaidi ya miaka mitano kubeba abiria kwenye ziwa hilo.

Janga la majini DRC

Ajali hiyo imetokea ikiwa ni mwezi mmoja tu toka watu 167 walipofariki kwenye ajali mbili za majini kwenye nchi hiyo. Ajali hizo zilimlazimu rais wa DRC Felix Tshisekedi kuamrisha kuwa abiria wote wa vyombo vya majini nchini humo wavalishwe maboya muda wote wa safari.

DRC ambayo ndiyo nchi kubwa zaidi barani Afrika, inategemea mito na maziwa kama njia za usafiri wa watu na mizigo na kuunganisha maeneo kadhaa ya nchi hiyo ambayo ni vigumu kufikika kupitia barabara.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Japo kuna boti chache za kifahari, boti nyingi nchini DRC zina changamoto za kiufundi na hujaza watu na shehena ya mizigo

Hata hivyo, usafiri huo umekuwa wa hatari kwa usalama, na licha ya serikali kuchukua hatua mbadala kutafuta ufumbuzi katika suala hilo bado hali si swari.

Ajali nyingi husababishwa na matatizo ya kiufundi ya vyombo vya majini pamoja kujaza watu na kupita kipimo.

Idadi ya vifo huwa kubwa sababu abiria hawavai maboya ya uokozi, lakini pia raia wengi wa nchi hiyo hawajui kuogelea.

Watu 27 walipoteza maisha baada ya bot yao kuzama Septemba mwaka jana, 26 mwezi Julai, 50 mwezi Mei na 40 mwezi Aprili wakiwa njiani kukimbia mapigano mashariki mwa nchi hiyo.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Usafiri wa majini ni wa muhimu zaidi nchini DRC

Majanga hayo ya majini pia yanatokana na serikali ya nchi hiyo iliyopo mji mkuu wa Kinshasa kushindwa kusimamia vizuri utekelezwaji wa sheria kutikana na maeneo mengi yenye mito na maziwa kuwa mbali na nchi hiyo kukumba wa mapigano.

Majanga Afrika Mashariki

Jumanne wiki iliyopita ilitimia miaka 23 tangu kisa cha ajali ambayo inatajwa kuwa mbaya zaidi katika karne kutokea barani Afrika katika ziwa victoria nchini Tanzania.

Ni janga ambalo lilisababisha idadi kubwa ya watu wapatao 1000 kupoteza maisha baada ya meli ya Mv Bukoba kuzama.

Kwa miaka yote hiyo Tanzania imeendelea kukumbwa na majanga makubwa na madogo ya majini.

Image caption Kivuko cha MV Nyerere kilikuwa kimebeba abiria wengi zaidi ya uwezo wake kilipozama Septemba 2018.

Mwaka jana, Septemba 2018 jumla ya watu 224 walifariki na watu wengine 41 wakiokolewa wakiwa hai katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere.

Mwaka 2011 na 2012 watu zaidi ya 250 walipoteza maisha kwenye bahari ya Hindi baada ya kuzama kwa meli za Mv Spice Islander na Mv Skagit.

Jumatatu iliyopita, Mei 20,2019 ajali ya majini ilitokea na kuua watu 16 huku wengine wakiwa hawajulikani walipo nchini Uganda.

Boti iliyokuwa imebeba wacheza mpira 50 wakiwa na mashabiki wao magharibi mwa Uganda.

Mwaka 2016 , wachezaji 30 wakiwa na mashabiki wao walizama katika ziwa Albert na watu 20 walifariki.

Mwaka 2018 watu 29 walifariki kufuatia ajali ya boti iliyotokea ziwa Victoria, nchini Uganda.

Boti hiyo iliyokuwa na watu zaidi ya 90 waliokuwa wanaelekea kwenye sherehe, ilipata ajali katika kaunti ndogo ya Mpatta wilaya ya Mukono.

Mwaka 2014, Umoja wa Mataifa ulisema kuwa takriban watu 98, wamekufa maji baada ya boti walimokuwa wanasafiria kuzama katika Ziwa Albert Magharibi mwa Uganda.

Boti iliyozama ilikua imebeba zaidi ya wakimbizi 100.

Aliyekuwa anaendesha boti hiyo alikamatwa na jeshi la polisi na inadaiwa kuwa alikua mlevi.

Mada zinazohusiana