Serikali za Tanzania na Kenya zachangamkia fursa ya kupeleka walimu kufundisha Kiswahili Afrika Kusini

magufuli Ramaphosa Haki miliki ya picha IKULU, TANZANIA
Image caption Rais John Magufuli na Cyril Ramaphosa wameazimia kudumisha uhusiano wa Tanzania na Afrika Kusini

Rais wa Tanzania John Magufuli na mwenzake wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa wameafikiana kuhusu kufundisha lugha yaKiswahili, ikiwa ni siku chache toka mawaziri wa Kenya na Afrika Kusini kusaini makaubaliano kuhusu suala hilo.

Rais Magufuli alikutana na Ramaphosa Ikulu ya Pretoria Jumapili, Mei 27 2019, ikiwa ni siku moja tu toka Ramaphosa alipoapishwa kuendelea kuliongoza taifa la Afrika Kusini.

Katika mkutano huo faragha, Magufuli alimpatia zawadi ya vitabu vya Kiswahili mwenyeji wake pamoja na kamusi.

Afrika Kusini iliidhinisha lugha ya Kiswahili kufundishwa katika shule za nchi hiyo Septemba 2018 kuanzia mwaka 2020 na kufungua fursa kwa walimu kutoka ukanda wa Afrika Mashariki amapo lugha hiyo ndipo inapochimbukia na kuzungumzwa.

Taarifa rasmi ya Mkurugenzi wa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Bw Gerson Msigwa inasema kuwa: "Rais Ramaphosa amesema kufuatia uamuzi wa Afirka Kusini kuanza kufundisha lugha ya Kiswahili, nchi yake itachukua walimu wa Kiswahili kutoka Tanzania ili watumike kufundisha somo hilo katika shule za msingi na sekondari."

Katika video fupi ambayo imepakiwa kwenye mtandao wa kijamii wa twitter wa Msemaji Mkuu wa serikali ya Tanzania Dkt Hassan Abbas, Rais Magufuli anasema kuwa makubaliano hayo pamoja na ya ushirikiano katika nyanja nyengine kama uchumi tatatiwa saini katika ziara rasmi ya Ramaphosa nchini Tanzania kabla ya kufanyika kwa mkutano wa ukanda wa SADC mwezi Agosti mwaka huu.

Wakati Marais hao wakifikiana makubaliano hayo, tayari Mawaziri wa Elimu wa Kenya Profesa George Magoha na Afrika Kusini Angelina Matsie Motshekga wametiliana saini makubaliano ya Kenya kupeleka walimu wa somo hilo.

Makubaliano hayo yalisainiwa jijini Nairobi Mei 16.

Profesa Magoha alinukuliwa na gazeti la The Satandard la nchini Kenya akisema makubaliano hayo yanafungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa nchi hizo.

Waziri Motshekga alinukuliwa akisema kuwa asilimia 40 ya wanafunzi nchini Afrika Kusini tayari wanajifunza Kiswahili kwa namna moja ama nyengine.

Gazeti hilo pia liliandika kuwa baada ya kufikiwa kwa makubaliano hayo, Afrika Kusini inaweza kuanza kufundisha Kiswahili.

Kiswahili ndiyo itakuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika inayotoka nje ya Afrika Kusini, kufunzwa katika shule za umma na binafsi za nchi hiyo.

Haki miliki ya picha IKULU, TANZANIA
Image caption Rais Magufuli alikuwa Afrika Kusini kuhudhuria kuapishwa kwa Rais Cyril Ramaphosa

Kifaransa, Kijerumani na hata lahaja ya Kichina ya Mandarin ndio miongoni mwa lugha za nje zinazofunzwa kama lugha mbadala katika shule Afrika Kusini.

Lugha ya Kiswahili ni moja ya lugha yenye wazungumzaji wengi barani Afrika. Ni ya tatu kwa ukubwa ikiwa nyuma ya Kingereza na Kiarabu.

Inakadiriwa kuwa na wazungumzaji takribani milioni 100 wa Kiswahili, kati yao milioni 15 kwao Kiswahili ni lugha ya kwanza.

Kiswahili ni lugha rasmi ya Umoja wa Afrika (AU) na Magufuli amesema kuwa amezungumza na Ramaphosa ambaye ni mwenyekiti wa SADC kuifanya lugha hiyo iwe rasmi pia kwenye umoja huo.

Kiswahili ni lugha ya rasmi na ya taifa nchini Tanzania na Kenya. Ni lugha rasmi pia nchini Rwanda na Uganda.

Kiswahili pia kinazungumzwa kwa wingi nchini Burundi na mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC)