Jinsi mazishi ya waliofariki kwa Ebola yanavyozua hasira DRC

Ebola Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mazishi ya wahanga wa Ebola hayafanyiki kwa misingi ya kidini.

Ni ada ya Waafrika kushiriki mazishi kwa wingi, na endapo watazuiwa kuwazika wapendwa wao, hasira ama ghasia zinaweza kuzuka.

Hali hiyo ndiyo inayoendelea katika maeneo ya mashariki mwa nchi ya Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ambayo yamekumbwa na ugonjwa hatari wa Ebola.

Mazishi ya mtu yeyote aliyefariki kutokana na ugonjwa huo ambao unaambukiza kwa kasi yanafanyika chini ya ulinzi mkali, ikiwa ni sehemu ya kujaribu kupunguza maambukizi.

Mazishi yenyewe huhusisha watu wachache, ndugu na jamaa wa marehemu huwekwa mbali na kaburi. Wanazuiwa kumuona ama kumgusa mpendwa wao.

Wanaozika huwa ni maafisa wa afya ambao huchukua kila aina ya tahadhari kuhakikisha hawapati maambukizi.

"Tunasikitishwa kuona anazikwa namna hii," Dennis Kahambu amenukuliwa akisema na shirika la habari la AFP wakati akiangalia kwa mbali mazishi ya binamu yake, Marie-Rose katika eneo la Butembo.

"Wanasema amekufa kutokana na Ebola."

Awali mlipuko wa ugonjwa huo ulitangazwa mwezi Agosti mwaka jana, na mpaka sasa watu takribani 1,200 wamepoteza maisha -- 200 kati yao wamefariki mwezi huu wa Mei.

Haki miliki ya picha Getty Images

Mlipuko huo ni wapili kwa ukubwa, baada ya ule wa Afrika Magharibi ulioua watu 11,300 kati ya 2014-16.

Mazishi ya Butembo yalifanyika kwa kufuata masharti makali kiafya, AFP inaripoti. Gari aina ya pick-up lilieta jeneza lenye mwili wa marehemu Marie-Rose mpaka makaburini.

Wafanyakazi wa mslaba mwekundu ambao walivalia mavazi maalumu ndiyo walioendesha maziko hayo. Hakukuwa na maombi ya kidini, ndugu walikuwa mbali kabisa na kaburi.

Mwanafamilia ama jamaa wa karibu anaruhusiwa kuchomeka msalaba baada ya kaburi kufukiwa, tena akiwa amaevalia mavazi maalumu pia.

Polisi sita wenye silaha za moto walikuwa wakilinda mazishi hayo wakati wote toka maiti inatolewa hospitali mpaka mwisho wa mazishi.

Wiki iliyopita, misafara miwili ya mazishi ya wagonjwa wa Ebola ilishambuliwa kwa mawe na raia wenye hasira katika miji ya Butembo na Bunia katika jimbo la Kaskazini Mashariki la Ituri.

Mshtuko wa kitamaduni

"Utamaduni wetu ni kuwa, mwili wa marehemu kwanza lazima urejeshwe nyumbani. Na baada ya watu kuomboleza, wanapata fursa ya kuugusa mwili kwa mara moja ya mwisho," Seros Muyisa Kamathe, ambaye ni mkalimani katika ameneo ya Beni na Butembo ameileza AFP.

"Kabla ya kwenda makaburini, unafungua kwanza jeneza ili watu wamuone marehemu kwa mara ya mwisho."

Kwa kawaida huwa ni ndugu na majirani ambao huchukua jukumu la kuchimba kaburi na kuamua kaburi liwe wapi.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Ndugu hukaa mbali wakati wa mazishi, na huruhusiwa kukaribia kaburi baada ya mwili kuzikwa.

Wataalamu wa kupambana na Ebola wanasema kugomewa na watu kuhusu mazishi ilikuwa ni moja ya vikwazo walivyokutana navyo wakati wa kupambana na janga lilozikumba nchi za Afrika Magharibi za Guinea, Liberia na Sierra Leone baina yam waka 2014-16.

Shirika la Afya Duniani (WHO) lina kanuni 12 za kushughulikia mazishi ya watu waliokufa kutokana na ugonjwa wa Ebola.

Lengo la kutunga na kufuatisha kanuni hizo ni kuhakikisha maiti hazisogelewi na kushughulikiwa na watu wengi. Lakini pia kanuni hizo pia zinajali pia heshima ya utu na maombolezo.

"Mazishi ni jambo nyeti kwa familia na jamii na yanaweza kuwa chanzo cha ugomvi mkubwa," inasema sehemu ya kanuni hizo.

Kanuni hizo pia zinataka mazishi yasifanyike bila kupatikana kwa kibali cha familia, na wafanyakazi wa afya wanatakiwa kushirikiana na jamii katika maombezi na kuwaacha wapate muda wa maombolezo.

Ulinzi Mkali

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Utitiri wa makundi ya waasi unafanya kukabiliana na Ebola kuwa kazi ngumu.

Mazishi ni sehemu inayochukua muda mrefu na inahitaji wafanyakazi wengi katika mlolongo mzima wa kupambana na ugonjwa wa Ebola.

Na katika eneo hili la Mashariki ya DRC ambapo kuna utitiri wa makundi ya waasi, ambayo baadhi hushambulia vituo vya kutibu Ebola, shughuli za mazishi huwa ngumu zaidi.

Kuhisiana vibaya, magomvi ya kisiasa katika mji mkuu wa Kinshasa na vita dhidi ya waasi vinafanya eneo hilo kuwa sehemu yenye rutuba kwa kushamiri virusi vya Ebola.

Katika mji wa Butembo, wafanyakazi wa afya huhitaji askari wenye silaha za moto ili kwenda kutafuta wagonjwa wa Ebola kwenye makazi ya watu, mpiga picha wa AFP hivi karibuni alishuhudia moja ya misafara hiyo.

Mkurugenzi mtendaji wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa shirika hilo Jumatatu ya wiki iliyopita (Mei 20) alilitangaza janga la Ebola nchini DRC kama "moja ya dharura kubwa na ngumu za kiafya ambazo kahuna yeyote kati yetu ambaye ameshawahi kukutana nalo."

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mgonjwa wa Ebola akipakiwa kwenye gari kupelekwa kituo cha matibabu

"Labda tuungane katika kulitokomeza ama sivyo tutakuwa hatarini kwa janga kutapakaa zaidi na kuwa ghali zaidi kulitokomeza."

"Hatupambani na kirusi (cha Ebola) tu," Tedros amesisitiza na kuongeza: "Tunapambana na kuzorota kwa usalama. Tunapambana na vurugu. Tunapambana za habari zisizo sahihiā€¦ na pia tunapambana na kutiwa siasa kwa mlipuko (wa Ebola)."

Licha ya changamoto luluki, wafanyakazi wa afya wa eneo hilo wapo mstari wa mbele katika kupigia mstari mafanikio yao.

Zaidi ya watu 118,000 wamepewa chanjo dhidi ya virusi hivyo, na hakuna hata mtu mmoja aliyeambukizwa virusi hivyo katika mataifa jirani ya Rwanda na Burundi.