Uganda na Rwanda zashutumiana kwa mauaji na utekaji nyara

Rais Paul Kagame wa Rwanda (kushoto) na Rais Yoweri Museveni, wamekuwa wakionekana kuwa marafiki hadi ulipotokea mzozo wa hivi karibuni baina ya mipaka ya nchi zao Haki miliki ya picha Getty Images

Mabalozi Saba kutoka Tanzania, Marekani Ufaransa, Urusi , Burundi, Afrika Kusini na Uingereza wamewasili katika wilaya ya Rukiga magraribi mwa Uganda kushuhudia utaratibu wa kuikabidhi Rwanda mwili wa mfanyabiashara aliyeuawa Ijumaa mpakani upande wa Uganda.

Awali mabalozi hao waliwasili Jumatatu katika uwanja wa ndege wa Kabale ambako waliondoka kwa magari kuelekea kwenye mpaka wa Gatuna ambako mwili wa John Batista Kyerengye unatarajiwa kukabidhiwa kwa maafisa wa Rwanda, limeripoti gazeti la kibinafsi la Daily Monitor nchini Uganda:

Wakati huo huo Polisi ya Rwanda imewashutumu maafisa wa ujasusi wa jeshi la Uganda kwa kuwateka Wanyarwanda wawili waliovuka mpaka na kuingia nchini Uganda Juamapili baada ya kualikwa na marafiki wao Waganda.

Uganda haijajibu shutuma za madai ya utekaji nyara unaodaiwa kutekelezwa na wanajeshi wake.

Shutuma hizo ni ishara ya hivi karibuni ya kingia doa kwa uhusiano baina ya nchi hizo jirani.

Jumamosi maafisa wa Uganda walilishutumu jeshi la Rwanda kwa kuwashambulia watu wawili- mmoja Myarwanda na mmoja Mganda- kwenye eneo la mpaka ndani ya ardhi ya Uganda. Rwanda ilikanusha madai hayo.

Serikali ya Kigali inasema kuwa watu wawili, mmoja raia wa Rwanda na mwengine wa Uganda , walipigwa risasi nchini Rwanda lakini baadaye wakafariki nchini Uganda.

Rwanda ilisema walishukiwa walikuwa ni miongoni mwa genge la watu wanaohusika na kuingiza vitu kinyume cha sheria ambalo liliwashambulia maafisa wa usalama wakati walipojaribu kuwakamata.

Inasema kuwa watu hao waliojeruhiwa baadaye walibebwa na kuvukishwa mpakani.

Lakini Uganda inasisitiza kuwa wanajeshi hao wa Rwanda waliingia katika himaya yake wakimtafuta raia huyo wa Rwanda na kumuua pamoja na raia huyo wa Uganda aliyejaribu kuingilia kati.

Kampala amewataka wahusika kuchukuliwa hatua lakini imeongezea kwamba haitafutalia swala hilo iwapo Kigali haitachukua hatua yoyote.

Kutokana na uhasama huu , Rwanda imeamua kufunga mpaka wake na Uganda wa Gatuna kwa usafiri wa bidhaa.

Licha ya kwamba viongozi wa nchi hizo mbili wamekuwa wakidai kufanya juhudi za kuumaliza mzozo huo, umekuwa ukiendelea.

Baadhi ya wananchi wa pande zote wamekuwa wakipaza sauti kwenye mitandao ya kijamii wakiwataka viongozi wao kumaliza tofauti zao ili kurekebisha mahusiano baina ya pande mbili.

Mpaka wa Gatuna ni mpaka ambao kwa kawaida huwa na shughuli nyingi na hatua hiyo inatarajiwa kukwamisha uhusiano wa kibiashara baina ya nchi mbili.

Mwezi Februari Rwanda ilizuwia bidhaa za Uganda kuingia ama kutoka nchini Rwanda lakini Rwanda ikasema kwamba inafanya ukarabati wa ujenzi kwenye mpaka huo.

Mwezi Machi mwaka huu serikali ya Rwanda kupitia waziri wake wa mashauri ya kigeni na ushirikiano wa kimataifa Dkt. Richard Sezibera ilisema kuwa mipaka yote ya Rwanda iko wazi:

Jamii zinazoishi katika maeneo ya mpaka baina ya nchi hizo mbili zinazoathirika zinasema upitishaji wa bidhaa kinyume na sheria umeongezeka kati ya mataifa hayo mawili na kwamba wanajeshi wa Rwanda huwashambulia raia wa Rwanda wanaojaribu kuingia Uganda.

Uganda imekuwa ikiishutumu Rwanda kuwatuma majasusi na kufanyia vitendo vya ujasusi kwenye ardhi yake,shutuma ambazo Rwanda inakanusha.

Rais Kagame amesisitiza kwamba mara kadhaa mwenyewe aliwasilisha malalamiko hayo kwa mwenzake Yoweri Museveni na kwamba hakuonyesha utashi wowote wa kuyatatua.

Wiki iliyopita serikali ya Rwanda ilikataza wananchi wake kwenda nchini Uganda na kusababisha mkwamo wa biashara.Rwanda inasema inatoa kipaumbele kwa maiasha ya raia wake zaidi kuliko biashara baina ya nchi mbili.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii