Uchaguzi Malawi: Rais Mutharika achaguliwa kwa mara ya pili baada ya kushinda kesi mahakamani

Malawi's president casts his ballot in his home town on May 21 Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mutharika alizushiwa kuwa amekufa kabla ya uchaguzi

Rais wa Malawi Peter Mutharika amepata ushindi mwembamba unaomuwezesha kusalia madarakani kwa awamu ya pili.

Kiongozi huyo mwenye miaka 78, alikumbana na upinzani mkali katika uchaguzi uliofanyika Mei 21.

Profesa Mutharika ametangazwa mshindi baada kupata 38.5% ya kura zote.

Matokeo yalicheleweshwa baada ya kinara wa upinzani Lazarus Chakwera aliyepata 35.4% ya kura zote, alipoenda mahakamani kupinga uchaguzi huo akidai ulikuwa na kasoro lukuki.

Matokeo ya uchaguzi huo yametangazwa Jumatatu jioni baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali shauri la upinzani.

Tangazo la Mkuu wa Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC), Jane Ansah, linaonesha kuwa Mutharika wa chama cha DPP kapata ushindi mwembaba kwa kumshinda mpinzani wake mkuu Chakwera wa MCP kwa kura 159,000 tu.

Makamu wa Rais wa Mutharika, Saulos Chilima, alimaliza katika nafasi ya tatu, akifanikiwa kupata 20% ya kura zote. Awali alidai kuwa jina lake halikuwamo kwenye karatasi ya kupigiwa kura kwa wagombea wa urais.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Lazarus Chakwera (kushoto) na Saulos Chilima (kati) walikuwa wakichuana na rais Mutharika (kulia)

Ikiwa inakabiliwa na makali ya umasikini, mustakabali wa uchumi na rushwa ndizo zilikuwa mada kuu za uchaguzi huo.

Uchaguzi huo ulikuwa ndio mgumu zaidi na usiotabirika katika historia ya taifa hilo.

Waliopiga kura ni 74% ya raia milioni 6.8 waliojiandikisha kwenye daftari la wapiga kura.

Malawi ilipata uhuru wake kutoka kwa Mwingereza mwaka 1964.

Huu ulikuwa ni uchaguzi wa sita wa urais nchini humo toka utawala wa chama kimoja kukomeshwa mwaka 1994.

Chama cha MCP kilikimbilia mahakamani kikitaka matokeo yasitangazwe wakidai kuna makosa lukuki, ikiwemo wizi wa kura.

MCP ilitaka kura zirudiwe kuhesabiwa walau kwenye majimbo 10 ya uchaguzi kati ya 28.

Katika baadhi ya maeneo kulikuwa na tuhuma za kubadilishwa kwa kura kwa kutumia wino maalumu.

Zuio la kutangazwa matokeo awali lilikubaliwa na mahakama baada ya tume kupokea ripoti 147 za mapungufu.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Zaidi ya nusu ya wapiga kura walikuwa kati ya umri wa miaka 18 na 34.

Ripoti hizo zilisababisha baadhi ya maeneo, hususani ngome za wapinzani kukumbwa na maandamano, shirika la habari la Reuters linaripoti.

Makamu wa Rais Bw. Chilima pia amesema kulikuwa na mapungufu makubwa katika uchaguzi huo.

Licha ya ripoti hizo, mahakama ilitupilia mbali ombi la upinzani na kuruhusu matokeo yatangazwe.

Rais Mutharika ni nani?

Rais Mutharika, ni mwanasheria na mwanataaluma kwa ngazi ya Profesa. Amekuwa kiongozi wa taifa hilo dogo la kusini mwa Afrika tokea 2014.

Amepata elimu yake nchini Uingereza na Marekani - na amekuwa kwenye ulingo wa siasa za nchi hiyo toka mwaka 2008 ambapo aliteuliwa kuwa mshauri mkuu wa sheria na kaka yake aliyekuwa rais wa nchi hiyo kwa wakati huo.

Alikamatwa mwaka 2013 pamoja na baadhi ya mawaziri kwa tuhuma za kutaka kumpindua mrithi wa kaka yake.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mutharika sasa anajiandaa kuiongoza Malawi kwa miaka mitano zaidi

Katika kuelekea uchaguzi huo umri na afya ya Mutharika viliangaziwa sana, kuna ambao waliozusha kuwa amefariki, ilimbidi akanushe uvumi huo.

Upinzani pia ulidai kuwa ufisadi umetamalaki katika kipindi chote ambacho Mutharika amekuwa madarakani.

Rais huyo alishawahi kuhusishwa na kashfa ya rushwa lakini akasafishwa na mamlaka ya kupambana na ufisadi ya nchi hiyo.

Mada zinazohusiana