'Roho Mtakatifu' amuepusha dereva na faini kwa mbawa zake

Njiwa mweupe Haki miliki ya picha VIERSEN DISTRICT POLICE
Image caption Roho mtakatifu aliingilia kati? Polisi wamemtaka dereva kuzingatia tahadhari hiyo

Dereva aliyekua akiendesha Gari kwa kasi nchini Ujerumani alinusurika kulipa faini ya pauni 93 baada ya njiwa mweupe kumuepusha kutambulika sura yake.

Dereva alinaswa kwenye kamera za mwendo kasi lakini sura yake ilifichwa na mabawa ya ndege huyo alipokua akiruka mbele ya kioo cha gari.

Taarifa ya polisi inasema pengine ''Roho mtakatifu'' aliingilia kati- ishara ya njiwa mweupe kama alama ya uwepo wa Mungu katika imani ya dini ya kikristo.

''Tumeelewa ishara hiyo na kumuacha dereva kwa amani wakati huu.''

Lakini maafisa katika mji wa Viersen, karibu na mpaka wa Ujerumani waliongeza: ''Tuna matumaini kuwa dereva huyo aliyesaidiwa anaelewa 'onyo hili kutoka juu' na kuwa ataendesha vizuri siku za usoni.''

Dereva alikua akisafiri kwa kasi ya kilometa 54 kwa saa katika barabara ambayo alipaswa asafiri kwa kilomita 30 kwa saa, polisi wameeleza

Kutokana na gari pekee kubainika na si dereva, alinusurika kulipa faini hiyo ''ashukuriwe malaika yule mwenye mabawa ambaye mbawa zake zilizuia sura ya dereza''.

Polisi wa mji wa Viersen amesema kuwa Njiwa huyo naye angetozwa faini kwa kupita kwa kasi kwenye eneo asilopaswa kupita.