Copa America: Neymar avuliwa unahodha wa Brazil, Dani Alves kuchukua nafasi yake

Neymar na Dani Alves Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Neymar na Dani Alves wanachezea Paris St-Germain

Neymar amenyang'anywa unahodha wa timu ya taifa ya Brazil katika michezo ya mwezi ujao ya Copa America na badala yake mchezaji mwenzie wa Paris St-Germain Dani Alves atachukua jukumu hilo.

Mchezaji huyo 27, alipewa kazi ya unahodha miezi minane iliyopita lakini amekua katika misukosuko kuhusu masuala ya nidhamu.

Alves, 36, atakiongoza kikosi katika mechi za kirafiki dhidi ya Qatar na Honduras.

Amekiongoza kikosi cha Brazil mara nne, hivi karibuni katika mechi ambayo Brazil iliibuka na ushindi dhidi ya Ujerumani mwezi Machi mwaka 2018.

Valencia yaangamiza ndoto ya Barcelona ya kushinda mataji mawili

Mwezi huu, mamlaka za soka nchini Ufaransa zilimfungia mechi tatu Neymar baada ya kumshambulia shabiki wakati PSG ilipopambana na Rennes katika fainali ya Coupe de France.

Pia aliripotiwa kugombana na wachezaji wenzake kwenye chumba cha kubadili nguo.

Michuano ya Copa America itafanyika nchini Brazil kuanzia tarehe 14 mwezi Juni mpaka tarehe 7 mwezi Julai, Brazil ikiwa kundi moja na Bolivia, Venezuela na Peru kwenye kundi A.