K-Lynn asema yeye na watoto wanamkumbuka sana mumewe Reginald Mengi

Familia ya Mengi

Jumatano wiki hii ilikuwa ni kumbukumbu ya kuzaliwa ya tajiri maarufu nchini Tanzania Reginald Mengi. Hata hivyo, tajiri huyo huyo alifariki wiki nne kabla jijini Dubai, Falme za Kiarabu.

Katika kuadhimisha siku hiyo ya kuzaliwa kwake, mkewe Bi Jacqueline Mengi ametumia mtandao wake wa kijamii wa twitter kumuomboleza mumewe na kusema kuwa yeye na watoto wao wanamkumbuka sana.

Mapenzi baina ya Mengi na mkewe yalishamiri katika siku za mwishoni za mzee Mengi, na walikuwa ni moja ya wapenzi maarufu mitandaoni kutokea Tanzania mpaka nchi jirani ya Kenya.

"Leo (Jumatano) tungelikuwa tukikusherehekea. Nikifumba macho yangu naona namna ambavyo ungetabasamau wakati tukikuimbia mwimbo wa kushereheakea kuzaliwa kwako. Hakuna maneno yanayojitosheleza kueleza jinsi gani mimi na watoto tunavyokukumbuka, tukiamka kila siku bila wewe. Heri ya siku ya kuzaliwa mpenzi wangu wa ukweli, milele mioyoni mwetu."

Ujumbe huo ndio ulikuwa wa kwanza kwa Bi Mengi maarufu kwa jina lake la kisanii kama K-Lynn kuchapisha mtandaoni toka alipofiwa na mumewe mwanzoni mwa Mwezi huu.

Wawili hao walifunga ndoa mwaka 2015 na mwezi Machi mwaka huu waliadhimisha miaka minne ya ndoa yao.

Katika maadhimisho hayo, Mengi aliandika ujumbe maridhawa kwa mkewe akisema anampenda sana.

"Ni furaha kuadhimisha ndoa yetu mpenzi wangu. Imekuwa safari iliojawa na mapenzi na furaha. nakupenda sana," aliandika bilionea huyo kupitia mtandao wake wa twitter.

Ujumbe huo ulimkuna K-Lynn ambaye aliujibu kwa kumhakikishia mapenzi tele: "Wewe ndio mwanamume wa pekee ambaye ningependelea kuishi maisha yangu nawe , mtu ambaye amekuwa rafiki yangu mkubwa , mwamba wangu, mshauri wangu, na mtu ninayejivunia ,tufurahie siku ya ndoa yetu, nakupenda mpenzi. Ahsante kwa kunionyesha jinsi mtu anavyohisi anapopendwa."

Mzee Reginald Mengi ambaye alizaliwa mwaka 1942 ni moja ya wafanyabiashara maarufu na miongozi mwa watu tajiri zaidiwaliopata kutokea Tanzania.

Alitokea katika maisha duni ambayo yeye mwenyewe aliyaita "umasikini wa kutupwa" na kufanya kazi kwa bidii mpaka kutajirika.

Jarida mashuhuri la biashara la Forbes lilikadiria utajiri wake kufikia dola milioni 560 kwa mwaka 2014.

Bi Jacqueline pia alikuwa mtu mashuhuri nchini Tanzania hata kabla ya kuolewa na Mengi.

Aliibuka mshindi wa taji la ulimbwende la nchi hiyo (Miss Tanzania) kwa mwaka 2000.

Kisha akendelea kujizolea umaarufu kama muimbaji, akianza kama moja ya vinara wa bendi ya the Tanzanite na kisha kuwa msanii huru.

Baadhi ya vibao vyake maarufu zaidi ni Nalia kwa furaha alichomshirikisha Bushoke mwaka 2004 na Crazy Over You alichomshirikisha Squizer mwaka 2007.

Wanandoa hao walibahatika kupata watoto wawili wa kiume.

Mada zinazohusiana