Ufilipino yarudisha shehena ya takataka Canada

Nembo inayotoa ujumbe kuwa takataka zirejeshwe Canada Haki miliki ya picha AFP

Ufilipino imerejesha tani za takataka nchini Canada, baada ya mvutano wa kidiplomasia wa majuma kadhaa ambapo Rais wa nchi hiyo Rodrigo Duterte kutishia '' kusafirisha takataka kwa njia ya maji kuelekea Canada''.

Ufilipino imesema takataka hizo ziliwekwa nembo kimakosa kuwa zilikua za plastiki tayari kwa kutengenezwa upya (recycling) zilipofikishwa Manila mwaka 2014.

Canada imekubali kulipa gharama za usafirishaji.

Makontena 69 ya takataka yalirejeshwa yakiwa kwenye meli ya mizigo kutokea ghuba ya Subic, kaskazini mwa mji wa Manila.

''Baaaaaaaaa bye, tusemavyo,'' Waziri wa mambo ya nje wa Ufilipino Teddy Locsin Jr aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter Ijumaa asubuhi.

Waziri, ambaye amekua maarufu kwa mtindo wa kauli zake kwenye ukurasa wake, aliweka picha na video ya meli ikiondoka bandarini.

''Hii ni kuonyesha kuwa tutaendelea kuwajibika kutekeleza jukumu la kimataifa la kushughulikia takataka zinazozalishwa Canada, ''Sean Fraser , katibu wa waziri wa mazingira aliiambia BBC.

Alisema Canada imechukua hatua za haraka katika kipindi cha majuma ya hivi karibuni kushughulikia suala hilo, ambalo limekua katika mvutano kwa miaka kadhaa baada ya Serikali ya Ufilipino kuweka wazi ''kuwa ni jambo wanalipa kipaumbele''.

Nchi nyingi za Kusini Mashariki mwa Asia zimezitaka nchi za magharibi kuchukua takataka zao walizozisafirisha nchini mwao, wakidai kuwa nyingine ziliingia kinyume cha sheria.

Haki miliki ya picha EPA

Kiasi cha takataka kilichosafirishwa na nchi zilizoendelea kilibainishwa baada ya China, ambayo iliingiza shehena za takataka kwa miaka kadhaa, kupiga marufuku kuingizwa ''takataka kutoka ng'ambo''.

Matokeo yake, takataka ambazo wakati mwingine udanganyifu hufanywa na nchi zilizoendelea kuwa takataka zinaweza kutengenezwa tena zilipelekwa katika nchi zinazoendelea ambazo nazo zimeanza kuzikataa shehena hizo za takataka.

Jinsi biashara ya takataka inavyotajirisha watu duniani

Duterte aikemea Canada

Mvutano ulianzaje?

Maafisa nchini Ufilipino walianza kuzungumzia suala la takataka na Canada mwaka 2014,ikisema kuwa makontena yenye nembo zilizowekwa kimakosa yamesafirishwa kuingia nchini Ufilipino kati ya mwaka 2013 na 2014.

Manila imesema kuwa makontena, yaliyowasili katika bandari ya kimataifa ya Manila, yalikua na nembo inayoonyesha kuwa kuna takataka za plastiki lakini kumbe zilikua tani za takataka zilizotoka majumbani.

Image caption Makontena ya takataka za Canada yakipuliziwa dawa kabla ya kusafirishwa

Mwaka 2016, Mahakama nchini Ufilipino iliamuru takataka hizo zirejeshwe Canada kwa gharama za Canada yenyewe.

Mwaka huo huo,Canada ilibadili kanuni zake kuhusu takataka hatarishi ili kuzuia tukio kama hilo lisijitokeze tena.

Mwanzoni mwa mwezi huu, Manila ilimuita Balozi wake aliyekua mjini Ottawa baada ya Canada kushindwa kufikia malengo ya muda uliowekwa wa tarehe 15 mwezi Mei kuchukua takataka zao.

Canada ikasema itaanza maandalizi ya kuzichukua takataka hizo.