Sudan: Yapigwa marufuku na Muungano wa Afrika AU

Rais wa Rwanda ndiye mweyekiti wa Muungano wa Afrika

Tume ya amani na usalama katika muungano huo inasema kuwa ilichukua uamuzi huo kufuatia mauaji ya raia wasio na hatia nchini Sudan katika kipindi cha siku tatu zilizopita.

Muungano huo umetaka uchunguzi kufanywa kuhusu mauaji hayo ambayo yanadaiwa kutekelezwa na vikosi vya usalama.

Tume hiyo inasema kuwa marufuku hiyo ilikubaliwa na wanachama na itaanza kutekelezwa mara moja.

Vilevile imetishia kuchukua hatua dhidi ya watu binafsi katika baraza hilo la mpito iwapo jeshi litakataa kukabidhi mamlaka kwa raia.

Maamuzi hayo yaliafikiwa baada ya kikao cha dharura kilichofanyika kwa takriban saa tano.

Hatua hiyo inajiri huku waziri wa afya nchini Sudan akisema kuwa ni watu 46 pekee waliofariki katika ghasia za hivi majuzi madai yanayopingwa na kamati ya madaktari nchini humo ambao wamesema kuwa idadi hiyo inafika watu zaidi ya 100.

Hali ya wasiwasi imepanda nchini humo tangu Jumatatu wakati ambapo vikosi vya usalama vilianzisha msako dhidi ya waandamanaji wanaounga mkono demokrasia.

Kikosi cha kijeshi cha RPS kilichoshutumiwa kwa kutekeleza mauaji hayo kimekuwa kikipiga doria katika mji mkuu wa Khartoum.

Muungano wa Afrika umeipiga marufuku Sudan kushiriki katika shughuli zozote za Muugano huo hadi taifa hilo litakapounda serikali ya mpito inayoongozwa na raia.

Uamuzi huo unajiri baada muungano huo kuwapatia watawala wa kijeshi wa taifa hilo siku 60 kukabidhi mamlaka kwa raia la sivyo wapigwe marufuku.

Haki miliki ya picha Reuters

Onyo hilo lilijiri baada ya utawala wa jeshi nchini humo kupuuza makataa ya awali ya kujiuzulu katika kipindi cha siku 15 kilioafikiwa na AU mnamo tarehe 15 mwezi Aprili.

Baraza la amani na usalama la AU lilisema kuwa lilijutia hatua ya jeshi hilo kushindwa kukabidhi mamlaka kwa utawala wa raia , lakini likaongezea kwamba linawapatia wanajeshi muda wa siku 60 kufanya hivyo.

Muungano huo ulisisitiza kuwa serikali ya kijeshi haitakubalika na matakwa na mahitaji ya taasisi za kidemokrasia na mikakati yake mbali na kuheshimu haki za binaadamu na uhuru wa raia wa Sudan.

Jeshi lilichukua mamalaka nchini Sudan baada ya kumpindua kiongozi wa muda mrefu Omar al Bashir kufuatia miezi kadhaa ya maandamano dhidi ya serikali.

Iliamua kufanya uchaguzi baada ya miaka miwili lakini waandamanaji wamekataa hilo na kusalia katika barabara za mji mkuu wa Khartoum , wakitaka utawala wa kiraia mara moja.

Baraza hilo likiongozwa na jenerali Abdul Fattah al-Burhan limekuwa likijadiliana na viongozi wa maandamano kuhusu uundaji wa serikali ya mpito.

Lakini pande hizo mbili zimetofautiana kuhusu jukumu la jeshi ambalo limetawaliwa na wandani wa al-Bashir.

Wakati huohuo Maafisa nchini Sudan kwa mara ya kwanza wamethibitisha kuwa hali siku ya juma wamekanusha madai kuwa watu 100 waliuawa na wanajeshi wakati wa maandamano na kukiri kuwa ni watu 46 waliyouawa katika purukushani hilo.

Madaktari wanaohusishwa na vuguvugu la waandamanaji wanasema idadi ya watu waliouawa na vikosi vya usalama wiki hii imepanda na kufikia zaidi ya watu 100.

Walisema miili 40 iliopolewa kutoka mto Nile mjini Khartoum siku ya Jumanne.

Awali mamlaka ilikuwa kimya kuhusiana na suala hilo lakini,maafisa wa wa wizara ya usalama mapema siku ya Alhamisi ilisema idadi ya waliyofariki ni 46.

Wanaharakati wa upinzani nchini Sudan wamekataa wito wa kufanya mazungumzo na baraza la kijeshi, ukihoji kuwa baraza haliwezi kuaminika baada ya msako wa nguvu dhidi ya waandamanaji.

Wakaazi wameiambia BBC kuwa wanaishi kwa uwoga katika jiji kuu la Khartoum.

Naibu mkuu wa Bwaraza hilo la Jeshi amepinga madai ya ukandamizaji na kuongeza kuwa wahalifu na walanguzi wa dawa za kulevya walikuwa wamejipenyeza katikati ya waandamanaji hao kufanya biahara zao.

"Hatutakubali vurugu kutokea na kamwe hatutarejea nyumakatika msimamo wetu. Hatuwezi kurudi nyuma. Lazima tuhakikishe nchi inaongozwa kwa utawala wa sheria," alisema Mohammed Hamadan - ambaye pia anafahamika kama Hemedti - siku ya Jumatano.

Ripoti kadhaa kutoka mjini Khartoum zinaarifu kuwa kikosi maalum cha kijeshi kinachojulikana kama Rapid Support Forces (RSF), kimekuwa kikifanya msako katika barabra kadhaa za mji huo na kinawalenga raia.

Kikosi hicho zamani kilijulikana kama wanamgambo wa Janjaweed, na kinasadikiwa kuhusika na mauji na ukatili katika mzozo wa Darfur Magharibi mwa Sudan mwaka 2003.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Maafisa wa usalama walipelekwa katika makao makuu ya kijeshi kuwaondoa waandamanaji siku ya Jumatatu

Sudan imekua chini ya utawala wa kijeshi tangu Rais Omar al-Bashir alipopinduliwa mwezi Aprili.

Viongozi walioongoza vuguvugu la kutaka utawala wa kiraia kuongoza nchi hiyo, wamesema wamesitisha mawasiliano na serikali ya mpito ya kijeshi na kufanya mgomo.

Vikosi vya usalama vilifika maeneo ambayo watu walikua wakiandamana, mapema Jumatatu na sauti za risasi zilisikika kwenye picha za video.

Chanzo ni nini?

Waandamanaji wamekua wakikita kambi nje ya jengo la makao makuu ya jeshi tangu tarehe 6 mwezi Aprili, siku tano kabla ya kuangushwa kwa utawala wa Bashir.

Mwezi uliopita, waandaaji na majenerali watawala walikubaliana kuhusu muundo wa serikali mpya na muda wa mpito wa miaka mitatu kuelekea kwenye utawala wa kiraia.

Hawajaweza kuamua kuhusu ni upande upi hasa kati ya raia au jeshi kuchukua nafasi nyingi zaidi.

Huwezi kusikiliza tena
Idadi ya waandamanaji waliouawa Sudan yaongezeka

Mwezi uliopita, viongozi wa waandamanaji na majenerali wa jeshi walitangaza kuwa wamefikia muafaka wa muundo wa serikali ya mpito ya miaka mitatu ambayo itaandaa uchaguzi wa kiraia.

Lakini wamesema bado wanatakiwa kufanya maamuzi ya nani aingie kwenye baraza huru ambalo ndilo litakuwa na maamuzi ya mwisho kwenye kipindi cha mpito cha miaka mitatu.

Hapajaweza kufikiwa makubaliano juu ya upande upi baina ya raia na wanajeshi uwe na wawikilishi wengi kwenye baraza hilo.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Barabara za mji wa Khartoum

Safari ya mabadiliko

19 Desemba 2018 - Maandamano yanalipuka baada bei ya mafuta na mkate kupanda

20 Desemba 2018 - Waandamanaji jijini Khartoum waanza kuimba nyimbo dhidi ya serikali wakitaka "uhuru, amani, haki"

22 Februari 2019 - Rais Omar al-Bashir atangaza hali ya hatari na kuvunja baraza la mawaziri

24 Februari - Maandamano yanaendelea licha ya vyombo vya ulinzi kutumia silaha za moto kutawanya waandamanaji

6 Aprili - Wanaharakati waanza kukita kambi mbele ya makao makuu ya jeshi wakiapa hawataondoka mpaka Bashir ang'oke madarakani

11 Aprili - Majenerali wa jeshi wanatangaza kuwa Bashir ameng'olewa uongozini laki waandamanaji wasalia wakitaka serikali ya kiraia

17 Aprili - Bw Bashir anapelekwa jela jijini Khartoum

20 Aprili - Mazungumzo baina ya viongozi wa kijeshi na wawakilishi wa waandamanaji yanaanza

13 Mei - Shabulio la risasi nje ya makao makuu ya jeshi linasabisha watu sita kuuawa

14 Mei - Majenerali na viongozi wa raia wanatangaza mapatano ya kuunda serikali ya mpito ya miaka mitatu

16 Mei - Mazungumzo yanaahirishwa baada ya jeshi kutaka baadhi ya vizuizi kuondolewa

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii