Sakata la Korosho Tanzania: Rais John Pombe Magufuli ailaumu wizara ya biashara kushindwa kuuza shehena ya korosho

mAGUFULI Haki miliki ya picha IKULU, TANZANIA

Kama ulidhani sakata la manunuzi na mauzo ya korosho nchini Tanzania limefikia tamati, basi umekosea.

Hii leo, Juni 10, 2019 rais wa Tanzania John Pombe Magufuli ametaja mustakabali wa biashara ya zao hilo kama moja ya sababu kubwa za kumtimua kazi aliyekuwa waziri wa viwanda na biashara wa nchi hiyo Joseph Kakunda.

Kakunda alivuliwa wadhifa wake na rais Magufuli siku moja baada ya kukutana na wafanyabiashara Ikulu jijini Dar es Salaam Juni 7, 2019.

Katika mkutano huo wafanyabiashara na wawekezaji wa viwanda walielekeza lawama nyingi katika wizara hiyo wakidai imekuwa ni sehemu ya changamoto badala ya utatuzi wa masaibu yao.

Kakunda alipata wadhfa huo Novemba 12, 2018 akichukua nafasi ya aliyekuwa waziri wa viwanda Charles Mwijage.

Mwijage pamoja na aliyekuwa waziri wa kilimo, Charles Tizeba walitimuliwa kazi na Magufuli Novemba 10, 2018 wakati sakata la korosho likiwa limepamba moto.

Mzozo wa korosho ulianza mwaka jana baada ya wakulima kugomea bei mpya kati ya TSh1,900 mpaka TSh2,700 kwa kilo ikiwa ni anguko la kutoka wastani wa TSh 4,000 kwa kilo msimu wa 2017.

Tarehe 28 Oktoba 2018, Rais Magufuli alifanya kikao na wanunuzi wakuu wa zao hilo na kuwaeleza kuwa serikali inaunga mkono msimamo wa wakulima.

Wafanyabiashara hao walikubali kununua korosho kwa bei isiyopungua shilingi 3,000. Huku serikali pia ikikubali kuondosha baadhi ya tozo na vikwazo vitakavyopelekea wafanyabiashara kushusha bei.

Licha ya makubaliano hayo, wafanyabiashara hao waliendelea kusuasua katika manunuzi hali ambayo ilimpelekea Magufuli kuwatimua mawaziri wake wawili na kuwazuia wafanyabiashara hao kununua korosho kutoka kwa wakulima.

Baada ya hapo Magufuli akaagiza wizara ya kilimo kununua korosho hizo kwa kutumia jeshi ambalo lilizikusanya na kusafirisha mpaka maghalani, na kuiagiza wizara ya biashara kutafuta masoko.

Hii leo Magufuli amaebainisha kuwa wakati jeshi na wizara ya kilimo zilifanikiwa kununua tani zaidi ya laki mbili, wizara ya viwanda na biashara chini ya Kakunda imeshindwa kutafuta masoko ya nje.

"Unakuwa na wizara kama hii ya nini sasa?" alisema Magufuli huku akionekana kuwa ameghadibika. "Tani 223,000 zipo kwenye maghala, (wizara ya) viwanda na biashara wamebangua tani 2,000 tu. Hizi nyengine (zaidi ya laki mbili) zinamsubiria nani? Waziri ana vyombo vyote vya kufanyia biashara, vyote vipo pale."

Magufuli amesema korosho hizo zipo toka kipindi ambacho msimu wa mavuno wa Tanzania ndio ulikuwa pekee katika soko la dunia mpaka kufikia kipindi hichi amabacho kuna ushindani kutoka nchi nyengine ambazo ni wazalishaji wa zao hilo pia.

Serikali ya Tanzania iliingia mkataba na kampuni ya Indo Power ya Kenya ambayo ilidai kuwa na uwezo wa kununu tani 100,000.

Hata hivyo, mwezi uliopita Kakunda alitangaza kuwa mkataba huo umevunjwa kutokana na kampuni hiyo kushindwa kukamilisha masharti ya kisheria.

Kazi lazima iende kijeshi

Magufuli amemtaka mrithi wa Kakunda bwana Innocent Bashungwa kwenda kuinyoosha wizara hiyo. "Innocent watu wakupe pole wasikupongeze, maana nikiona mambo hayaendi natengua...nilitaka nipangua wizara yote juu mpaka chini...nenda usibembeleze mtu, nafuu wakuchukie mimi nikusimamie."

Rais huyo amesema hakuna namna nyengine zaid ya kufanya kazi kujeshi.

Amesema japo mawaziri wa Mambo ya Nje Prof Palamagamba Kabudi na Waziri wa Fedha Dkt Philip Mpango wamemzidi umri huwa anawafokea na mara kadhaa neno 'pumbavu' limekuwa likimtoka.

"Hii kazi si ya kubembelezana, lazima tuipeleke kijeshi. Mwanajeshi usiposonga mbele kupigwa risasi na mwenzako si tatizo, mpo kwenye vita. Sasa hatuwezi kuwa na vita halafu tukabembelezana maneno mazuri mazuri tu. Lazima tubalishe mwelekeo, watu wanaotuangalia hawana muda wa kusubiri," amesisitiza Magufuli.

Mada zinazohusiana