Benki ya Tanzania yasitisha ubadilishanaji wa fedha na Kenya kudhibiti fedha haramu

noti mpya za Kenya Haki miliki ya picha SIMON MAINA

Serikali ya Tanzania imetangaza kusitisha ubadilishanaji wa fedha za Kenya kwa sarafu ya nchini shilingi ya Tanzania.

Benki kuu Tanzania (BoT) imeeleza kwamba hatua hiyo imeidhinishwa kukabiliana na uingizaji wa pesa haramu nchini.

Kadhalika hatua hiyo imechukuliwa kuitikia hatua ya benki kuu ya Kenya kusitisha ubadilishanaji wa sarafu na kurudishwa nchini sarafu ya Kenya.

Haya yanafuata uzinduzi wa noti mpya Kenya mnamo Juni mosi.

"Benki kuu Tanzania imeshauriwa kuzuia akaunti ya ukusanyaji sarafu ya CBK mara moja" imeeleza taarifa ya Benki kuu Tanzania.

Lakini hatua hii ina maana gani?

Yoyote aliye na noti za zamani za sarafu ya Kenya katika nchi hizo mbili jirani itabidi ende nazo Kenya ili zibadilishwe kwa noti mpya zilizozinduliwa na zilizoanza kutumika nchini chini ya muongozo wa benkii kuu ya Kenya.

Wachuuzi wengi katika mataifa hayo hutumia sarafu za nchi hizo na huzitumia kubadilihsa kwa sarafu zinazotumika katika nchi wanazotoka.

Hivi karibuni Gavana wa benki kuu Kenya Patrick Njoroge, ameeleza kwamba ameshauriana na mabenki makuu katika eneo kuwa waangalifu kuhusu fedha zinazosafirishwa kutoka Kenya, kutokana na hofu kwamba watu wanaohodhi fedha huenda wakajaribu kuzibadilisha kwa sarafu za kigeni.

Kauli hiyo inatazamwa kama pigo kwa waendeshaji biashara haramu ya fedha, wanaodaiwa kusafirisha fedha nje ya nchi na kutarajia kuziingiza kiharamu kwa kutumia sarafu za kigeni.

Kadhalika inawaathiri pia wachuuzi na wafanyabiashara wanaotumia sarafu za kigeni kuendesha shughuli zao nchini Tanzania na katika taifa jirani la Uganda pia.

Haki miliki ya picha SIMON MAINA

Baadhi ya wafanyibiashara nchini Tanzania waliozungumza na BBC wamepokea hatua hiyo kwa hisia tofauti huku wakiongeza kuwa ni vyema taarifa itolewe ili kutoa muongozo kuhusu suala hilo.

''Ni vizuri wametuambia mapema kwa sababu kuna wafanyibiashara ambao wanakuja, wanatuletea hizo pesa na tunachukua lakini ni vizuri tukafanya matangazo zaidi ili watu wafahamu na ili wachukue hatua mapema kwa ajili ya kubadilisha hiyo pesa'' alisema Frunk Fundi mmoja wa wafanyibiashara hao.

Wengine walionekana kutokuwa na taarifa kuhusiana na hatua hiyo lakini wanasema ipo haja ya kuhamasisha raia pande zote mbili.

Kwa mfano Muhammed Issa anasema: ''Kama serikali ishatangaza kuhusiana na suala la kubadilisha fedha za kigeni, inamaanisha kuwa pande zote mbili zijue kwamba hii sarafu imebadilika na wenye nazo wanatakiwa wafikie ile huduma kupata kubadilisha ili kuepusha hasara kutokea zaidi na zaidi.''

Anaongeza kuwa hatua hiyo inastahili kuchukuliwa kwasababu inahusisha nchi mbili tofauti.

Nae Joseph Mung'ane wa Masoba ambaye ni mfanyabishara wa kubadilisha fedha za kigeni katika mpaka kati ya Kenya na Tanzania wa Isibania-Sirari anasema hatua hiyo imeathiri biashara katika eneo hilo la mpakani.

Bw. Mung'ane anasema jambo hili la kuzuia ubadilishaji wa fedha za kigeni mpaka mtu aende benki limeathiri sehemu kubwa kwasababu watu wengi wanashindwa kwenda benki kwasababu haziko karibu nao.

''Wanashindwa kwenda benki kwasababu wengine wanaishi vijijini na hawana namna ya kuweka pesa zao'' alisema.