Kenya: Mwanafunzi wa Chuo Kikuu akamatwa kwa kuingia Ikulu kinyume cha sheria

Ikulu ya rais Kenya Haki miliki ya picha TWITER
Image caption Ikulu ya rais, Kenya

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) nchini Kenya, Brian Kibet Bera, anauguza majeraha katika katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta baada ya kupigwa risasi na polisi kwa kuingia Ikulu ya Nairobi kinyume cha sheria.

Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 25, ambaye alikwea lango moja la Ikulu, alipigwa risasi na kujeruhiwa bega la kushoto na maafisa wa polisi wanaopiga doria kwenye lango hilo baada ya kuchomoa kisu alipoagizwa asimame.

Siku ya Jumapili Jioni Kibet aliandika katika mtandao wake wa Facebook kuwa ataingia Ikulu.

Kwa mujibu wa msemaji wa Ikulu, Kanze Dena-Mararo Kisa hicho kilitokea Jumatatu na mshukiwa alipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Kileleshwa na kusajiliwa katika Kitabu cha Matukio nambari 39 kabla ya kupelekwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta kwa matibabu.

''Tunachukua fursa hii kukumbusha umma kwamba Ikulu ni mahali polipotengwa kuwa chini ya ulinzi mkali kwa mujibu wa Sheria ya Maeneo Yanayolindwa (Protected Areas Act). Kwa sababu hiyo, hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kuingia Ikulu pasipo na ruhusa ya mamlaka yenye jukumu hilo.'' alisema Bi Kanze.

Ameongeza kuwa uchunguzi unaendelea kubaini nia yake ya mshukiwa huyo kuingia Ikulu kinyume cha sheria na hatua zifaazo zitachukuliwa baada ya uchunguzi kukamilika.

Kisa hicho kimezua mjadala mkali katika mitandao ya kijamii nchini Kenya huku baadhi watu wakihoji kwanini mwanafunzi huyo aliamua kuchukua hatua hiyo.

Wengine kama DiMacharia wanasema huenda alichukua hatua hiyo baada ya kutumia kileo fulani kwasababu mtu aliye na akili timamu hawezi kudhubu kufanya hivyo

Kuna wale walioamua kufuatialia mjadala huo katika mtando wa kijamii wa Twitter ambao wameshangazwa na baadhi ya maoni ya watu wanaompongeza mwanafunzi huyo.

Kwa mfano Danvas Nyabasa anasema KIbet sio mwendawazimu bali ana hasira kama mtu mwingine yeyote anaehisi kunyanyasika kutokana na hali ngumu ya maisha.

Nyabasa anasema rais atarajie wageni zaidi ikiwa hataingilia kati kuwasaidia Wakenya wanaozongwa na umasikini na kutoa wito kwa mamlaka kuingilia kati suala hilo.

Nae Cyrus Yegon anasema ''Hii ni ishara wazi kuwa vijana nchini Kenya wanakabiliwana msongo wa mawazo kutokana na ukosefu wa ajira.

Unafahamu nini kuhusu Ikulu ya rais wa Kenya?

  • Ikulu ya Nairobi ndiyo makazi rasmi ya Rais wa Jamhuri ya Kenya lakini awali ilitumika kama ofisi rasmi ya gavana wa Afrika Mashariki.
  • Ikulu ya Nairobi ilijengwa 1907 kama makazi rasmi ya gavana wa mkoloni Mwingereza aliyesimamia kanda ya Afrika Mashariki (British East Africa).
  • Ikulu ya Rais imekuwa makazi rasmi ya kiongozi wa taifa la Kenya tangu uhuru 1963.
  • Ramani ya Ikulu ilichorwa na msanifu majengo maarufu wa Uingereza Sir Herbert Baker anayetambulika kwa kuchora ramani za majengo ya serikali nchini India na Afrika Kusini.
  • Nyakati za ukoloni, Ikulu ilifahamika kama jumba la serikali (Government House) na ilitumika kama makazi rasmi ya magavana wa ukoloni waliotumwa kusimamia Kenya.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii