Mahakama ya Kisutu yatoa agizo la Wema Sepetu kukamatwa nchini Tanzania

Wema Sepetu

Mahakama nchini Tanzania imetoa agizo la kukamatwa kwa aliyekuwa malkia wa urembo nchini humo Wema Sepetu.

Uamuzi huo umetolewa na hakimu mkazi mwandamizi Maira Kasonde baada ya mshtakiwa kudaiwa kushindwa kufika mahakamani ili kusikiliza kesi inayomkabili.

Mlimbwende huyo alishtakiwa baada ya kanda ya video ya mahaba kati yake na mwanamume mmoja kusambaa katika mitandao ya kijamii nchini Tanzania.

Kulingana na gazeti la Mwananchi nchini humo kabla ya uamuzi huo, wakili wa serikali Silvia Mitanto alidai kwamba mshtakiwa pamoja na mdhamini wake hawakuwepo mahakamani ilihali walihitajika kuwepo wakati wa kusililizwa kwa ushahidi wa kesi hiyo.

Hatahivyo Ruben Simwanza ambaye ni wakili wa Wema amesema kuwa mteja wake alikuwemo mahakamani lakini aliugua na akalazimika kuondoka.

Lakini baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili , hakimu huyo alisema kuwa haiwezekani kwamba mshtakiwa alihudhuria kikao hicho na kwamba alihitaji kuielezea mahakama kabla ya kuondoka

"Kama amekuja mahakamani halafu akaondoka bila kutoa taarifa, mahakama itajuaje kama alikuja? Alishindwa nini

kutoa taarifa mahakamani, alisema"

Kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 4 mwezi Julai huku hakimu akitoa hati hiyo ya kukamatwa kwa Wema.

Kabla ya kesi hiyo mahakam hiyo ya Kisutu ilikuwa imempata na hatia bi Wema kufuatia kesi ya umiliki wa miahadarati iliokuwa ikimkakabili.

Inadaiwa kwamba mnamo tarehe 4 mwezi Februari 2017, Wema na wenzake walipatikana wakimiliki misokoto ya bangi katika eneo la Kunduchi Ununio.

Maafisa wa polisi nchini Tanzania walianzisha msako dhidi ya watu maarufu baada ya baadhi yao kuhusishwa na ulanguzi wa mihadarati.