Afcon 2019: Wachezaji maarufu waliotemwa Taifa Stars na Harambee Stars kombe la mataifa ya Afrika

Wachezaji wa Taifa Stars wakifanya mazoezi Haki miliki ya picha Tff/ Twitter

Huku kombe la mataifa ya Afrika likitarajiwa kuanza kuumiza nyasi mnamo tarehe 22 mwezi huu nchini Misri , mataifa yanayoshiriki yameanza kutoa orodha za wachezaji wao watakaobeba bendera za mataifa yao katika michuano hiyo.

Hatahivyo tayari minong'ono imeanza kuhusu wachezaji walioorodheshwa kushiriki katika kombe hilo ambalo ndio la hadhi ya juu barani Afrika.

Wengi hususan mashabiki wa timu za Afrika Mashariki wanadai kwamba wachezaji muhimu waliofaa kushirikishwa katika mechi hizo walitemwa kwa sababu moja ama nyengine huku wengine wakikosa sababu zozote za kutoshirikishwa.

Haki miliki ya picha Tff/Twitter

Walio nje Tanzania

Nchini Tanzania kwa mfano wakati benchi la kiufundi la timu ya Taifa stars lilipokuwa likitoa orodha ya mwisho ya wachezaji 23 watakaoshiriki katika fainali hizo za AFCON, kiungo mshambuliaji Shiza Kichuya, beki Kiraka Abdi Banda na mshambuliaji Shaban Chilunda ni mioingoni mwa nyota tisa walioenguliwa kikosini.

Kulingana na gazeti la Mwananchi, licha ya kuteuliwa kwenye kikosi cha awali, watatu hao wanaocheza soka la kulipwa katika nchi za Hispania, Afrika Kusini na Misri wameshindwa kupenya kwenye kikosi cha wachezaji 23 ambao kisheria ndio wanaopaswa kushiriki fainali hizo.

Kocha Emmanuel Amunike ameshindwa kumjumuisha Banda anayechezea klabu ya Baroka FC ya Afrika Kusini na badala yake ameamua kuwajumuisha kundini Ally Mtoni 'Sonso' wa Lipuli na nyota wa

Mbao FC, Vincent Philipo kulingana na gazeti la Mwananchi.

Kwa upande mwengine Kichuya anayechezea klabu ya ENPPI ya Misri, ameshindwa kufua dafu mbele ya Farid Mussa, Thomas Ulimwengu na Yahya Zayd, gazeti hilo limeongezea.

Vilevile hakukuwa na nafasi kwa mshambuliaji Shabani Chilunda ambaye hivi karibuni alivunja mkataba na klabu ya CD

Tenerife ya Hispania kwa kutopata nafasi ya kutosha ya kucheza, na badala yake kocha Emmanuel Amunike amemuita mshambuliaji aliyetimuliwa na klabu ya Botswana Defence Force XI, Rashid Mandawa.

Kwa upande mwengine benchi la ufundi la Taifa Stars lilimpatia nafasi mshambuliaji Adi Yussuf ambaye hivi karibuni alitia saini mkataba wa kujiunga na Blackpool inayoshiriki Ligi ya Daraja la pili Uingereza.

Hata hivyo, hakukuwa na nafasi kwa nyota wa timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 'Serengeti Boys', Kelvin John kama ilivyo kwa kipa wa timu ya Taifa chini ya umri wa miaka 20, Claryo Boniface.

Walioenguliwa Harambee Stars

Nchini Kenya Kocha wa Harambee Stars Sebastien Migne alimuacha nje kiungo wa kati wa klabu ya Zesco Anthony Akumu kutoka orodha ya wachezaji 23 watakaoshiriki katika michuano hiyo ya Juni 22 mjini Cairo.

Beki wa Afrika Kusini Brian Mandela tayari alikuwa amewekwa nje baada ya kupata jeraha , ikimaanisha kwamba kocha Migne alikuwa na wachezaji wengine watatu zaidi wa kuwatema kutoka kikosi chake cha wachezaji 27 ambacho kilikuwa nchini Ufaransa kutoka tarehe 30 mwezi Mei.

Winga Christopher Mbamba atalazimika kusubiri ili kuiwakilisha Kenya kwa mara ya kwanza.

Mchezaji wa Ureno Winga Clifton Miheso alikuwa mwathiriwa mwengine katika kikosi cha mwisho cha Migne ijapokuwa ni kutemwa kwa Akumu ambako kumewashanagazaa mashabiki wengi.

Kiungo huyo wa kati amekuwa kiungo muhimu katika klabu yake ya Zambia ijapokuwa hajakuwa akishirikishwa mara kwa mara katika mechi nne za kufuzu katika kipute hicho tangu mkufunzi huyo wa Ufaransa alipochukua hatamu.

Mchezaji Allan wanga ambaye amekuwa akiongoza katika ufungaji wa magoli katika ligi ya kenya pia ni miongoni mwa Waathiriwa wa shoka la kocha Migne .

Mbali na Wanga kipa wa kariobangi Sharks Brian Bwire ambaye licha ya kujumuishwa katika kikosi hicho hapo awali alizua mjadala mkubwa.

Hatahivyo alitemwa katika kikosi hicho pamoja na kiungo wa kati wa AF leopard Whyvonne Isuza.

Mchezaji Musa Mohammed ambaye alipata jeraha katika mechi ya kufuzu kombe la Afcon dhidi ya Madagascar siku ya Ijumaa ameorodheshwa katika orodha hiyo pamoja na Abud Omar ambaye pia alipata jeraha dogo kabla ya mechi hiyo kukamilika.