Bajeti 2019: Kenya, Uganda, Tanzania na Rwanda kutangaza makadirio ya matumizi ya fedha

Bajeti Afrika mashariki Haki miliki ya picha SOPA Images

Leo ni siku ya bajeti kwa nchi za Afrika Mashariki, ambapo mawaziri wa fedha wa nchi hizo watawasilisha bajeti za serikali za nchi zao kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Serikali ya Tanzania inapanga kutumia takriban $14.3 bilioni, katika mwaka wa fedha 2019/2020 ikiwa ni ongezeko , kutoka shilingi trilioni 32.5 za Kitanzania katika mwaka wa fedha 2017/2018.

Waziri wa fedha Philip Mpango, amesema sehemu kubwa ya makadirio hayo ya fedha katika bajeti zitatumika katika kuimarisha miundo mbinu ikiwemo reli barabara na kusambaza umeme katika maeneo ya vijijini.

Bajeti ya Kenya, inakadiriwa kuwa dola bilioni 30.2, ambayo ni kubwa kuliko bajeti zote za nchi zingine za afrika mashariki kwa pamoja.

Uganda kwa upande wake inakadiria bajeti ya dola bilioni 10.9 huku Rwanda dola bilioni 3.17.

Kwa upande wa Uganda, wakosoaji wanaiona nchi hiyo ikiendelea kutingwa na madeni, nakisi ya biashara na kuongezeka kwa kiwango cha umasikini.

Hata hivyo viongozi wa serikali ya nchi hiyo wanapinga na kueleza uchumi wa nchi hiyo ni imara na unaendelea kukua.

Deni la Kenya limezidi utajiri wake kwa 57%, sehemu kubwa ikitokana na wakopeshaji na wawekezaji wa kimataifa.

Kwa upande mwingine takwimu za madeni ya Rwanda, na Tanzania ni chini ya 40% ya pato jumla nchini.

Huku mapato yakishuka katika mataifa yote ya Afrika mashariki, inatazamiwa kwamba awamu nyingine ya malipo ya kodi na mikopo yataidhinishwa na mawaziri wa fedha katika bajeti ya mwaka huu.

Ina maana gani kwako?

Swali kubwa linaloulizwa ni Bajeti hizi zina maana gani kwa raia wa kawaida?

Hii ni fursa ya kuelewa serikali imelenga nini katika ugavi wa rasilmali na pia kusaidia kutathmini uzito inayoweka katika masuala ya maendeleo yanayomgusa na kumfaidi mwananchi.

Bajeti hizi pia zinatoa ufafanuzi wa iwapo umaskini unapungua katika mataifa.

Kipimo kinatokana na kuangalia iwapo mahitaji ya raia masikini yanazingatiwa kwa rasilmali za serikali au iwapo kodi zinazoidhinishwa zinawalemaza zaidi masikini.

BBC Swahili imezungumza na baadhi kuhusu matarajio yao katika bajeti ya mwaka huu Afrika mashariki:

Haki miliki ya picha Noel Shao

Noel Shao, Tanzania

Kwa maoni yangu sitegemei jambo jipya sana kwa sababu bado historia inaonyesha kwa miaka mingi kumekuwa na ukwamo wa utekelezaji wa bajeti kwa sababu ya uhaba wa fedha.

Wizara nyingi zinashindwa kutimiza malengo walio jiwekea kwa sababu fedha wanazo omba hawatimiziwi kwa kiwango kile walicho ainisha.

Na ni kwa bahati mbaya sana bajeti yetu kwa asilimia kubwa inategemea wahisani kuliko mapato ya Ndani.

Na kwa jinsi hii ni ngumu sana kuwa na bajeti inayo tekelezeka labda hadi Serikali itengeneza mazingira rafiki katika kutegemea vyanzo vyake vya ndani kuliko nje.

Kwa uhaba wa fedha Serikalini nategemea kuona uongezeko kubwa la bidhaa hasa mafuta jambo ambalo litasababisha mfumuko wa bidhaa sokoni, hivyo kusababisha ugumu wa maisha kwa wananchi.Ni matamanio yangu kuona makadirio ya fedha kwenye mfuko wa maendeleo ya jamii kuwa kubwa ili kuweza kugusa jamii moja kwa moja.

Takwimu tu kwenye karatasi hazitaweza kuondoa na kupunguza changamoto zinazo wakabili wananchi.

Vipengele muhimu kwa jamii ni Pamoja na afya, maji na elimu. Hapa ndipo panapo hitaji uangalifu kwani maeneo hayo ni msingi wa maisha hasa kwa wananchi wa kipato cha kati na Chini.

Bajeti itakuwa na lugha inayo sikika kama itagusa maeneo hayo.

Haki miliki ya picha Cornelius Kurgat

Cornelius Kurgat, Kenya

Mimi kama kijana ningependa kuona iwapo serikali imewatengea sehemu kubwa ya bajeti vijana kuwawezesha katika jamii, katika kuunda nafasi za kazi au ajira.

Vijana wengi wamemaliza kusoma katika vyuo vikuu, hawana ajira na wanahitaji kitu cha kufanya.

Pia tunavyosikia ni kuwa kuna ongezeko la bajeti karibu takriban trilioni tatu na hatujui fedha hizi zitatoka wapi.

Hili linatia wasiwasi kwasababu raia hawajuia fedha hizi zitatoka wapi.

Raia wana imani hatahivyo, kwamba hatua zitakazoidhinishwa na serikali zitakuwa kwa manufaa ya mwananchi wa chini.

Haki miliki ya picha Rogers Kigenza

Rogers Kigenza, Rwanda

Matarajio yangu kwenye bajeti hii yatajikita katika maeneo manne:

Kwanza uundwaji wa nafasi za kazi kwa vijana, natarajia kutakuwa na mikakati ya kuwatengea vijana nafasi za kazi katika sekta za uwekezaji na viwanda.

La pili ni miundo mbinu, kuimarisha sekta ya kutengeza barabara mpya, kusambaza umeme na hata maji.

Unaona miji inapanuka na kuna changamoto za hapa na pale za barabara nzuri zinazohitajika lakini sio tu mijini bali hata vijijini. Kwasababu barabara zinaozunganisha miji na vijiji zinahitjaika.

La tatu ni kilimo, tunajua kuwa hii ni sekta kubwa inayotoa kazi kwa watu wengi. Tunataka kuangalia je kilimo kimepewa kipa umbele kiasi gani?

La mwisho ni elimu.

Tunajua kuna changamoto katika elimu na tunataka tuangalie sekta hiyo imetengewa kiasi gani.

Kwasababu ya changamoto zinazoshuhudiuwa mfano vyumba vya madarasa, na pia uboreshaji wa ubora wa elimu inayotolewa katika shule mbalimbali za walimu.

Haki miliki ya picha Kheri Mbiro,

Kheri Mbiro, Tanzania

Tunategemea kwamba serikali itakuwa imeangalia katika maeneo ya biashara na uwekezaji katika kuimarisha nafasi zote zinazoweza kujitokeza.

Kutokana na malalamiko kwamba biashara na hali ya uchumi ya watu wengi imekuwa chini, tunaamini kuwa itawaangalia watu wa chini kwasababu uwekezaji, kilimo, biashara na viwanda unashirikisha asilimia kubwa ya watanzania katika sekta rasmi na zisizio rasmi.

Kwahivyo tunategemea kwamba Bajeti itatoa mianya kwa uwekezaji na viwanda sana, na ajira, kusaidia katika ufunguzi wa uchumi na kwa watu binafsi.

Pia nategemea kwamba itasaidia kupunguza kodi au katika kuboresha mfumo wa ajira na kuwafanya wafanyakazi wapate unafuu wa maisha hasaa katika wakati huu ambao watu waenalalamika kwamba hali sio nzuri.

Suala kubwa zaidi ni bidhaa, hapo ndipo kodi inajikita sana.

Na kusababihsa ugumu kwa hali ya maisha hususan kwamba hela imewakimbia wengi, tunategemea kwamba serikali itasoma kodi iliyopunguzwa kwa bidha ambali mbali kuwawezesha Watanzania kupata nafuu ya ununuzi wa bidhaa pamoja na kupunguza makali ya maisha.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii