Watoto waliolazimika kuwa kimya kuhusu baba zao wakutana na maaskofu jijini Paris

Anne-Marie Jarzac,binti wa Kasisi na mtawa Haki miliki ya picha Getty Images

Watoto wa makasisi wa kikatoliki ambao wanahisi ''kunyamazishwa'' na kanisa kwa miongo kadhaa wataeleza simulizi zao mbele ya maaskofu jijini Paris kwa mara ya kwanza.

Viongozi hao watakutana na muungano wa watoto walionyamazishwa yaani Les Enfants du silence siku ya Alhamisi.

Kwa maombi yao wenyewe, watoto wa kike na wa kiume wa makasisi watazungumza kuhusu baba zao, namna walivyotengwa na taabu wanazopitia.

Uwepo wao ni jambo linalotazamwa kwa karibu na kanisa, ambalo linategemea makasisi kutii sheria ya utawa.

Msemaji wa mkutano wa maaskofu mjini Paris,Vincent Neymon,amesema wakati umefika ''kujua kuwa watu wamepata taabu na wanaendelea kupata taabu''.

''Bila shaka masikio ya kanisa yako wazi zaidi leo.'' Alisema, akiongeza:"Kanisa linapaswa kutambua kuwa watu hawa wanaishi.''

'Kunyamaza '

Akizungumza kabla ya mkutano, Mtoto wa kike wa kasisi ambaye sasa ana umri wa miaka 50 na kupewa jina moja tu la Maya, ameiambia tovuti ya Franceinfo kuwa miaka yote alijisikia kuwa anapaswa kukaa kimya baada ya kujua nafasi ya baba yake akiwa na miaka saba.

''Unapoishi ukiwa mtoto wa kasisi,unalazimika kukaa kimya,'' alisema, akiongeza kuwa baba yake hakuwepo katika kipindi kirefu cha utoto wake,kama vile mtu anayetumia muda mwingi akiwa ''safarini''.

Maya alisema alinyamaza kimya kuilinda familia yake, akihofu kuchukuliwa kupelekwa kulelewa.

Haki miliki ya picha Getty Images

Marie-Christine Miquel, mtoto mwingine, alisema kuwa hakuwahi kumuona baba yake mpaka alipotimiza miaka tisa, wakati baba yake alipoacha ukasisi.

''Nilikua kama watoto wengine walioishi katika ukimya, sikuuliza maswali,''Alisema.

Mikutano ya siku ya Alhamisi huenda ikafichua simulizi zaidi za namna hii.

''Kwa mara ya kwanza kanisa limefungua milango kwetu, hakuna kukataliwa tena, isipokuwa kusikilizwa na kufahamisha maisha tuliyoishi,''Bi Jarzac, mtoto wa Kasisi na mtawa wa kike aliliambia gazeti la Le Monde.

Wafunguka kuhusu unyanyasaji wa kingoni katika kanisa katoliki

Changamoto kubwa inayomkabili Papa kwa sasa

'Maisha ya mtoto ni muhimu'

Akihojiwa na chombo cha habari cha Vatican mwezi Februari, Kadinali Benuamino Stella alieleza misingi ya kanisa akihusisha viongozi wa dini na watoto na kama wataondolewa kuhudumu nafasi zao.

''Kila kesi huchunguzwa kwa kutazama mazingira husika,'' alieleza.

Kadinali alisema ingawa baadhi ya makasisi huingia kwenye mahusiano yanayozaa mtoto, si lazima iathiri ''hali ya utawa wa kikasisi ambayo ni zawadi kwa kanisa la kilatini''.

''Suala muhimu ni kuwa Kasisi katika kukabiliana na ukweli wa mazingira yaliyojitokeza, anapaswa kuelewa kuwa jukumu lake kwa mtoto ni muhimu kwa ajili ya kanisa,'' aliongeza.