Bajeti ya Afrika Mashariki: Kenya, Tanzania na Uganda zajikita katika ufadhili wa miradi ya maendeleo

Bendera za mataifa ya Afrika mashariki Haki miliki ya picha EAC/Facebook
Image caption Bendera za mataifa ya Afrika mashariki

Mataifa ya jumuiya ya Afrika mashariki Rwanda, Uganda, Kenya na Tanzania yalifanya makubaliano kusoma bajeti zao kwa pamoja mwakani.

Nchini Kenya Waziri wa Fedha Henry Rotich aliwasilisha makadirio ya bajeti ya dola bilioni 31.5 kwa mwaka wa 2019 hadi 2020 ambayo inatajwa kubwa zaidi.

Waziri Rotich amesema kuwa bajeti hiyo imezingatia ndoto na azimio la Rais Uhuru Kenyatta kuwekeza katika sekta nne muhimu ili kuliendeleza taifa.

Sekta hizo ni pamoja na zile za Afya, Kilimo, Makaazi na Uzalishaji wa viwanda na sekta hizo zimepewa sehemu kubwa ya mgao wa bajeti.

Haki miliki ya picha K24 TWITTER
  1. Sekta ya Uzalishaji imepewa mgao wa dola milioni 12 ili kupanua viwanda vya kuzalisha na kutengeneza bidhaa ili kutengeza ajira.
  2. Sekta ya Nyumba imepokea bilioni 1 itakayotolewa kama mikopo kwa wakenya ili kuwawezesha kujenga.
  3. Sekta ya Afya mepata mgao wa dola milioni 800 zitakazotumika kuwaajiri madakatari na wauguzi zaidi kando na kununua vifaa vya matibabu.
  4. Sekta ya Kilimo ambayo inasadikiwa kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Kenya nayo imepokea dola milioni 550.

Lakini je fedha za kuwezesha miradi hii itatoka wapi?

Waziri wa Fedha Bwana Rotich anasema kuwa ushuru utalipia bilioni 21 huku pengo linalobakia likitegemea mikopo kutoka nje na ndani ya nchi.

Hali hii imembidi waziri Rotich kuongeza biashara ambazo hazikuwa zinatozwa ushuru hapo awali kuanza kufanya hivyo.

''Katika miaka iliyopita huku uchumi ukikua, kumekuwa na ongezeko la huduma zinazotolewa na biashara ingawa baadhi ya bashara hizo hazikua chini ya sheria inayoshurutisha kulipa ushuru.'' alisema Bw. Rotich

Alipendekeza kuwa sheria ibadilishwe ili kuongezea biashara hizo.

''Bwana Spika biashara zinazotoa huduma za usalama usafi upishi nje ya hoteli na migahawa usafirishaji wa bidhaa na mauzo''

Lakini wakenya wakawaida pia hawajasazwa katika nyongeza hiyo ya ushuru.

Waendeshaji biashara ya kamari sasa watatozwa 10% ya fedha zote wanazowekeza.

Pembo na sigara pia zimeongezewa ushuru wa ziada huku nao wandesha pikipiki maarufu Boda boda nao watalazimika kuchukua bimna itakayowakinga wao pamoja na abiria dhidi ya ajali nyingi zinazoshuhudiwa

Kenya ina deni ya jumla ya dola bilioni 54 za Marekani na mikopo ya mwaka huu itaongeza deni hilo hadi dola bilioni 60.

Kuna hofu ikiwa miradi inayofadhiliwa na bajeti hiyo ina uwezo wa kuleta faida ya kulipa deni hilo.

Wadadisi wa uchumi tayari wameonya kuwa hilo haliwezekani

Haki miliki ya picha BUNGE

TANZANIA

Bajeti ya serikali kwa mwaka 2019/2020 imewasilishwa leo mjini Dodoma na Waziri wa fedha na mipango Dokta Philip Mpango huku ikiwa na mapendekezo ya kufutwa kwa tozo tano pamoja na marekebisho ya baadhi ya sheria.

Katika Bajeti hiyo ya shilingi za kitanzania trilioni 33 serikali ya Tanzania imetenga shilingi trilioni 12.2 kwa ajili ya kugharamia mpango wa Maendeleo wa Taifa mwaka 2019/2020.

Kati ya fedha hizo shilingi trilioni 9.7 ni fedha za ndani na shilingi trilioni 2.5 ni fedha za nje.Fedha hizo za maendeleo ni sawa na asilimia 37 ya bajeti yote ya mwaka 2019/2020.

Bajeti hii imeweka msisitizo mkubwa katika kuendeleza ujenzi na ukarabati wa miundombinu hususani reli,bandari,nishati,barabara,madaraja na viwanja vya ndege pia kutekeleza uboreshaji wa mazingira ya biashara yawe rafiki na yenye gharama nafuu.

Bajeti hii imependekeza kufanya marekebisho ya mfumo wa kodi ikiwemo baadhi ya viwango vya kodi,tozo na ada zinazotozwa chini ya sheria mbalimbali na pia taratibu za ukusanyaji na usimamiaji wa mapato.

Dr Mpango amesema maboresho haya yamelenga:

Sheria ya usimamizi wa kodi

Sheria ya ushuru wa bidhaa

Sheria ya usalama barabarani

Sheria ya bajeti ya mwaka 2019

Katika sheria ya kodi ya ongezeko thamani Dokta Mpango amependekeza kufanya marekebisho 'kusamehe kodi ya ongezeko la thamani kwa wakulima wanaoingiza makasha yenye majokofu kwa ajili ya kilimo cha kisasa cha mbogamboga kwa wakulima watakaoingiza makasha hayo kutoka nje.

Pia amependekeza kusamehewa kodi kwa vifaa vya kukausha nafaka ili kuchochea ongezeko la kilimo cha nafaka.

Serikali imependekeza kurekebisha Sura ya 160 ya Sheria ya Usalama Barabarani ili kuongeza muda wa leseni za udereva kutoka miaka mitatu hadi mitano,na kupandisha malipo yake kukata leseni kutoka shilingi 40,000 hadi elfu 70 za kitanzania.

Lakini pia kuna ongezeko la ada ya usajili wa kadi za gari kutoka shilingi 10,000 za kitanzania hadi 50,000.,ambapo pikipiki za magurudumu matatu yaani bajaji kadi ya usajili kwa sasa imefikia shilingi 30 kutoka elfu kumi.

Bajeti 2019: Ina maana gani kwako?

Kwa nini Burundi inataifisha mali za wapinzani?

Pikipiki za kawaida usajili wa kadi zake umetoka shilingi elfu 10 hadi 20,000.

Lakini katika masuala ya urembo,serikali imependekeza ongezeko la ushuru wa nywele za bandia uwe asilimia kumi kwa zile zinazotengezwa ndani ya nchi na asilimia 25 kwa zile zinazotoka nje.

Dokta Mapngo amependekeza kupunguza kiwango cha kodi ya ongezeko la thamani kutoka asilimia 18 mpaka asilimia 0 kwenye huduma za umeme unaouzwa kutoka Tanzania bara kwenda Tanzania Zanzibar ili kuwapunguzia gharama za maisha wananchi .

Mikakati iliyowekwa kwa mwaka 2019-2020

  • Serikali imekusudia kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuwezesha kukamilisha miradi mikubwa kama miundombinu na huduma za jamii.
  • Kurekebisha viwango vya kodi kwa lengo la kuhamasisha uzalishaji na kulinda viwanda vya ndani dhidi ya ushindani kutoka nje.
  • Kuboresha mazingira ya kufanya biashara ili kuvutia wawekezaji na ukuaji wa biashara ndogo na za kati ili kupanua wigo wa kodi na mapato mengine ya serikali.
  • Kuboresha mazingira ya ulipaji kodi kwa hiyari upanuzi wa wigo wa kodi na matumizi ya TEHAMA katika usimamizi wa kodi.
  • Kuimarisha usimamizi wa sheria za kodi ili kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kupunguza upotevu wa mapato pamoja na kuweka mkazo zaidi katika kutoa elimu kwa mlipa kodi.
  • Kuimarisha makusanyo yasiyo ya kodi kwa kuhimiza matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA.
Haki miliki ya picha Twitter The spy Uganda

UGANDA

Bajeti ya Uganda ilipitishwa mwezi wa Mei lakini kwa ujumla waziri wa fedha wa Uganda Matius Kassaja ameangazia zaidi masuala ya ujenzi wa viwanda na alisema kuwa Bajeti ya mwaka wa fedha wa 2019 na 2020 inalenga hatua zinazokusudia kuongeza utajiri na na ustawi wa waganda wote.

'' Maudhui ya mwaka huu yanaendelea kuwa ujenzi wa viwanda kwa kubuni kazi na ustawi wa watu wote'' alisema Bw. Kasaja.

Pia ameongezea kuwa biashara baina ya Uganda na nchi za Afrika Mashariki imeongezeka hadi 59% ya bidhaa zote zilizosafirishwa mwaka 2018.

Anasema katika kipindi hicho soko la Afrika Mashariki liliendelea kuwa kubwa zaidi kwa mahuruji ya Uganda huku kipato cha Uganda kwa bidhaa zinazopelekwa Afrika Mashariki kikifikia dola milioni 469.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii